Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viongozi Chadema Kilwa Masoko walalamikia ukosefu wa ofisi, fedha za uendeshaji

Kilwa. Baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Kilwa Masoko, mkoani Lindi, wamelalamikia kile walichodai ni ukosefu wa fedha za uendeshaji wa chama katika wilaya hiyo, hali wanayosema imeathiri shughuli za chama na uhamasishaji wa wanachama.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Julai 27, 2026, viongozi hao walisema ofisi za chama katika wilaya hiyo zipo katika hali isiyoridhisha kutokana na kutofikishwa kwa fedha zinazochangwa kwa ajili ya uendeshaji wa chama.

Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Kilwa Masoko, Sadick Lionjo, alisema hali hiyo inazorotesha juhudi za viongozi wa ngazi ya chini za kuimarisha chama na kuongeza idadi ya wanachama.

"Ni aibu kwa wilaya kukosa ofisi ya chama licha ya ahadi mbalimbali zilizowahi kutolewa na viongozi wetu kuwa tutajengewa. Hadi sasa hakuna kilichotekelezwa," alisema Lionjo.

Alidai pia kuwa wanachama wameendelea kusikia taarifa zinazodai baadhi ya viongozi wanatumia vibaya fedha za michango ya chama, jambo alilosema linapaswa kuchunguzwa ili ukweli ujulikane.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Wilaya ya Kilwa Masoko, Hamis Liunde, alisema viongozi wa wilaya hiyo hawana nia ya kuichafua taswira ya chama, bali wanataka kuwepo kwa uwazi kuhusu masuala yanayozungumzwa ndani ya chama.

Alisema ni muhimu viongozi wanaotuhumiwa kuhusu matumizi ya fedha wakapisha uchunguzi ili kutoa nafasi kwa ukweli kubainika na kurejesha imani ya wanachama.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema Jimbo la Kilwa Kusini, Fatuma Kahewa, alisema fedha zinazotengwa kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi za chama zinapaswa kuwafikia walengwa kwa wakati ili kuwawezesha viongozi kutekeleza majukumu yao katika mazingira bora.

Kahewa pia aliwataka viongozi wa juu wa chama kusikiliza maoni ya wanachama na viongozi wa ngazi za chini badala ya kuyatafsiri kama uasi, akisema kufanya hivyo kutasaidia kuimarisha umoja na kukinusuru chama.