Vodacom yaonyesha nguvu ya teknolojia kuinua uchumi wa kidijitali
Muktasari:
- Ubunifu wa simu janja, M-Pesa na suluhisho za kidijitali waibua fursa zaidi za ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa kidijitali, huku kampuni ikijizolea tuzo mbili za maonesho.
Dar es Salaam. Vodacom Tanzania PLC imeendelea kuonyesha nafasi yake katika kuendeleza uchumi wa kidijitali nchini kupitia teknolojia na huduma bunifu zinazorahisisha maisha ya wananchi, huku ikisisitiza dhamira ya kupanua ujumuishi wa kidijitali kwa Watanzania.
Katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), kampuni hiyo imeonyesha huduma mbalimbali zikiwemo simu janja zinazopatikana kwa gharama nafuu, huduma za mawasiliano, M-Pesa na suluhisho nyingine za kidijitali zinazolenga kuwawezesha wananchi, wafanyabiashara na taasisi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Mbali na kuonesha ubunifu wake katika maonesho hayo, Vodacom pia ilitunukiwa tuzo ya nafasi ya tatu kwa mshindi wa jumla wa maonesho hayo pamoja na tuzo ya nafasi ya pili ya udhamini, ikiwa ni utambuzi wa mchango wake mkubwa kama mshirika muhimu wa Maonesho ya Sabasaba.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, alisema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, teknolojia bunifu na huduma zinazomweka mteja katikati ili kuongeza fursa za maendeleo kwa Watanzania.
"Dhamira yetu ni kuwaunganisha Watanzania na fursa za kesho. Tunaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali, teknolojia bunifu na huduma jumuishi zinazowezesha watu wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali," alisema Besiimire.
Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara na Masoko, Brigita Shirima, alisema maonesho ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa kampuni hiyo kuwasogezea wananchi bidhaa na huduma zinazoboresha maisha kupitia matumizi ya teknolojia.
Alisema kupitia simu janja, huduma bora za mawasiliano, M-Pesa na suluhisho nyingine za kidijitali, Vodacom inaendelea kufungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii kwa Watanzania.
Mbali na kuonyesha ubunifu wake, Vodacom Tanzania ilitunukiwa Tuzo ya Nafasi ya Tatu kwa Mshindi wa Jumla wa Maonesho hayo pamoja na Tuzo ya Nafasi ya Pili ya Udhamini, ikiwa ni utambuzi wa mchango wake katika maendeleo ya maonesho hayo na sekta ya teknolojia nchini.
Katika ufunguzi wa maonesho hayo, Rais wa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akiwa ameambatana na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, walitembelea banda la Vodacom na kupata maelezo kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali za kidijitali zinazotolewa na kampuni hiyo kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Philip Besiimire.