Wachumi wataka Pakistan kutekeleza kikamilifu mpango wa GSP
Ukiukwaji wa mikataba ya kimataifa na haki za binadamu nchini Pakistan unadaiwa kuitia doa nchi hiyo katika mpango maalumu wa upendeleo wa kibiashara unaotolewa na Umoja wa Ulaya kwa nchi zinazoendelea duniani (GSP).
Hayo yameelezwa na wachumi wakati wakihojiwa na mitandao wa Dawn, kuhusu mashaka ya wabunge wa ulaya na mashirika ya kiraia kuhusu ukiukwaji huo.
Katika mpango huo, umoja wa ulaya huondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zote zinazosafirishwa kutoka mataifa mbalimbali kwenda mataifa ya ulaya.
Sharti la utekelezaji wa mpango huo ni lazima nchi husika kuridhia na kutekeleza kwa vitendo mikataba 27 ya kimataifa ya haki za binadamu, haki za wafanyakazi, utunzaji wa mazingira na utawala bora.
‘’Licha ya faida kubwa za kiuchumi za mpango huo, Pakistan inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali za ukiukaji wa mikataba ya kimataifa, viwango dhaifu vya utawala, utekelezaji duni wa mageuzi ya kisheria na wasiwasi unaojirudia wa haki za binadamu, ‘’ alisema mmoja wa wachumi hao, Profesa Asif Bilal.
Mchumi mwingine, Dk Amna Khan alisema ingawa uchumi wa Pakistan haujaimarika sana kupitia mpango huo, ukiukwaji wa haki za binadamu unaliondolea uaminifu Taifa hilo kwa nchi za ulaya.
‘’Nchi inategemea mauzo ya nje kwa ajili ya mapato ya fedha za kigeni na utulivu wa uchumi. Katika GSP kuna marekebisho na mikataba imeongezeka hadi 32, hii inaiweka Pakistan katika wakati mgumu zaidi, sasa itakabiliwa na uchunguzi mkali zaidi kama haitofuata taratibu,’’ alisema Dk Amna.
Kupitia maboresho ya GSP, Pakistan imepewa kipindi cha mpito cha miaka miwili lakini mwendelezo wa makubaliano ya biashara ya siku za usoni utategemea matumizi mapya na utekelezaji unaoaminika unaolenga mageuzi.
‘’Mfumo uliorekebishwa unaashiria umoja wa ulaya unazidi kuwa na wasiwasi kuhusu utekelezaji wa masharti katika nchi zinazoendelea, huu ni mtihani mwingine kwa Pakistan,’’ alisema Bilal akiunga mkono hoja ya Dk Amna.