Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajumbe waonya watiania CCM, Jimbo la Temeke si ‘shamba la bibi’

Muktasari:

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Agosti 2, 2025 na baadhi ya wajumbe, wakati watiania wanane wa ubunge Jimbo la Temeke walipofika kujitambulisha sambamba na kujinadi.

Dar es Salaam. Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Tandika wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam, wamewataka watiania ya ubunge kutolifanya jimbo hilo kama shamba la bibi.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Agosti 2, 2025 na baadhi ya wajumbe, wakati watiania wanane wa ubunge Jimbo la Temeke walipofika kujitambulisha sambamba na kujinadi.

Wajumbe hao mbali ya kueleza changamoto sita zinazowakabili ikiwamo ya mikopo kausha damu inayosababisha wengine kunyang’anywa mali zao, wamewataka watiania hao kutolifanya jimbo hilo kama shamba la bibi, yaani kupata na kuondoka.

Wametaja changamoto nyingine ni upendeleo katika utoaji wa mikopo ya halmashauri, wazee kupewa dawa za kutuliza maumivu pekee hospitalini, barabara mbovu, kukosekana kwa masoko na viongozi kutokuwa karibu na wananchi.

Akizungumza katika mkutano huo, mjumbe aliyejitambulisha kwa jina la Hadija Kiponga, amesema baadhi ya wananchi wa Temeke wamekuwa wakikopa vifaa mbalimbali na kutakiwa kulipa haraka, na wakichelewesha malipo, mali zao hupigwa mnada.

Kutokana na changamoto hiyo, Hadija ametaka watia nia hao waeleze ni kwa jinsi gani watawakwamua ili kuepukana na kero hiyo inayorudisha nyuma maendeleo yao.

Mjumbe mwingine, Eva Mwenda, ametaka mikakati ya watia nia hao kusaidia vijana ambao wanahangaika bila ajira kwa kipindi kirefu.

Naye Said Masai alihoji namna wabunge hao watarajiwa watakavyotatua tatizo la umasikini Temeke, akisisitiza kuwa Mfuko wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) umewatambua wananchi wenye vipato duni lakini hawajapata fedha hizo za Serikali.

Pia, amesisitiza kuwa suala la matibabu kwa wazee ni changamoto inayowakabili kwa muda mrefu na wamekuwa wakipewa ahadi za matibabu bure bila mafanikio.

Kwa upande wake, Omary Athumani alilalamikia Temeke kukosa mwakilishi aliye karibu na wananchi, akihimiza wajumbe kutokubali jimbo hilo kuwa shamba la bibi.

Watia nia katika jimbo hilo jumla yao ni wanane ambao ni pamoja na Shafi Dauda, Dorothy Kilave, Mariam Kisangi, Fadhili Said, Leah Mwampishi, Bernard Mwakyembe, Jasdeep Singh na Mussa Mtullya.


Majibu ya wagombea

Akijibu baadhi ya kero hizo, mgombea ubunge Temeke Mariam Kisangi amesema alikuwa mbunge wa viti maalumu na ameacha nafasi hiyo kwa sababu anataka kutafuta maendeleo kwa wananchi.

"Nikiwa UWT sina eneo maalum la kupeleka maendeleo,nikipata nafasi, nitatatua changamoto ya wafanyabiashara sokoni na miundombinu ya barabara.

Watu wanadhani ubunge ni rahisi, ubunge unahitaji uzoefu, nina uzoefu, naweza kuibua hoja na kutetea watu wangu wapate maendeleo," amesema.

Kwa upande wake, Mussa Mtullya amesema sababu iliyomshawishi kugombea ubunge ni fursa zilizopo Temeke, hivyo anataka ridhaa hiyo kuwaonyesha wananchi fursa kwenye elimu na mikopo ya halmashauri.

"Changamoto ya bima ya afya kwa wazee na wajawazito pamoja na ukosefu wa fedha za TASAF zote nitazifanyia kazi, brabara na maji nazo ni kero nitahakikisha tunaziondoa," amesema.

"Miundombinu kero ni kubwa, hasa maji na barabara, nikichaguliwa nitawatetea akina mama wajasiriamali na akina baba," ameongeza.

Naye mgombea Jasdeep Singh amesema akiwa diwani wa Kata ya Keko ameshirikisha sekta binafsi katika kuwaletea wananchi maendeleo, hasa ujenzi wa shule, miundombinu ya barabara, zahanati pamoja na kutoa bima ya afya kwa kaya zisizojiweza.

"Tumeboresha mazingira yetu ya uwekezaji. Tuna kiwanda Kata ya Keko kilichoajiri vijana 500, nombeni kura zenu nikawaletee maendeleo," amesema.

Aliyekuwa mbunge wa Temeke ambaye sasa anaomba kuongoza kwa awamu nyingine, Dorothy Kilave, ameomba kuaminiwa na wajumbe kwa mara nyingine ili akamilishe miradi ya maendeleo kwa wananchi.

"Kata ya Tandika kwa miaka mitano nimefanya mambo mengi kulikuwa na shule zenye uhitaji wa ukarabati, nilikuta Mtaa wa Nyambwela tumetengeneza barabara, nimechangia fedha za ujenzi wa Serikali za Mitaa," amesema.

Hoja za wajumbe zimejibiwa pia na mgombea Leah Mwampishi akisema anafahamu changamoto nyingi za Temeke kutokana na kukaa na wananchi kwa muda mrefu.

"Nina ujasiri wa kusimama mbele yenu kuomba kura zenu," amesema.

Mgombea mwingine, Bernard Mwakyembe, amesema Temeke yapo maeneo hayapitiki kutokana na maji kujaa barabarani wakati wa mvua, hivyo atatafuta majawabu ya changamoto hiyo.

"Najua tuna changamoto ukienda mtaa wa Maguruwe na Tamla, maji yanajaa wakati wa mvua,mkinichagua nitamaliza kero hii,

suala lingine ni mikopo kwa wajasiriamali ya asilimia 10 ambayo inatolewa kwa ujanja ujanja hii tutaisimamia," amesema.

Mikopo hiyo ilizungumziwa pia na Fadhili Mohamed akisema, "Mungu amenileta Tandika kutatua changamoto hiyo.

"Kuna mikopo ya asilimia 10 japo wanufaika ni wachache, nitahakikisha nakwenda kulipambania hili suala," amesema.

Mgombea ubunge Shafi Dauda amesema ni mzaliwa wa Temeke, hivyo anafahamu kuhusu masoko mabovu na kudorora kwa michezo katika jimbo hilo.