Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wamiliki wa shule zisizo za Serikali walia na tozo

Mtendaji Mkuu wa TAMONGSCO, Benjamin Nkonya, akizungumza na waandishi wa habari Arusha kuhusu tozo

Muktasari:

  • Wamesema kuwa baadhi ya halmashauri nchini bado zinaendelea kuendelea kukusanya baadhi ya kodi na michango ambayo haipo katika mwongozo wa Serikali Kuu, hali inayozua sintofahamu na kuongeza gharama za uendeshaji wa taasisi za elimu binafsi.

Arusha. Wamiliki wa shule zisizo za Serikali nchini wamezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kusitisha ukusanyaji wa kodi na tozo zilizofutwa na Serikali kuu.

Wamesema kuwa baadhi ya halmashauri nchini bado zinaendelea kuendelea kukusanya baadhi ya kodi na michango ambayo haipo katika mwongozo wa Serikali Kuu, hali inayozua sintofahamu na kuongeza gharama za uendeshaji wa taasisi za elimu binafsi.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, viongozi wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO) wamesema shule binafsi zinakabiliwa na mzigo wa kodi na tozo mbalimbali zinazofikia zaidi ya 11.

Tozo hizo zinatajwa kujumuisha ushuru wa huduma (Service Levy), gharama za uchapishaji wa mitihani, ada za mabango ya shule pamoja na michango inayohusiana na mashindano ya michezo ya wanafunzi.

Mtendaji Mkuu wa TAMONGSCO, Benjamin Nkonya, amesema baadhi ya makusanyo yanayofanywa na halmashauri hizo yanakinzana na maelekezo ya Serikali Kuu na yamekuwa yakiongeza mzigo mkubwa kwa watoa huduma za elimu binafsi.

Amesema pamoja na ushuru wa huduma, shule hizo pia hulazimika kuchangia gharama za mitihani na mashindano ya michezo kama UMITASHUMTA na UMISSETA, ambazo baadhi ya michango hiyo haina manufaa ya moja kwa moja kwa taasisi zao.

“Tunachopinga si ulipaji wa kodi halali, bali namna ya ukusanyaji wake.

"Inashangaza kuona mgambo wenye silaha wakiingia shuleni kudai kodi zilizoshasamehewa na mbaya zaidi wengine kutishia kufunga shule"

"TRA imekuwa ikitoa elimu kwa walipakodi na kuwapa muda wa kutekeleza wajibu wao, lakini baadhi ya halmashauri zinatumia nguvu hata katika madai ya kodi ambazo tunaamini zilishafutwa na Serikali,” amesema Nkonya.

Amesema endapo hali hiyo itaendelea bila kupatiwa ufumbuzi, baadhi ya shule binafsi zinaweza kushindwa kuhimili gharama za uendeshaji na hivyo kuathiri utoaji wa huduma za elimu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMONGSCO Kanda ya Kaskazini, Leonard Mao, alisema suala hilo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu, lakini juhudi za kupata ufafanuzi kutoka kwa mamlaka husika bado hazijatoa majibu ya kuridhisha.

“Tunaomba Serikali itoe mwongozo mwingine wa wazi kuhusu kodi na tozo zinazostahili kulipwa na shule binafsi.

"Vilevile, tunasisitiza kuwa halmashauri zifuate taratibu za kisheria badala ya kutumia mabavu katika ukusanyaji wa mapato"

Mao alibainisha kuwa TAMONGSCO tayari imewasilisha barua kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu mamlaka ya halmashauri kuendelea kukusanya baadhi ya kodi na tozo zinazodaiwa kufutwa na Serikali Kuu.

“Tunatarajia kupata majibu rasmi yatakayoweka bayana misingi ya kisheria inayotumika na kama halmashauri zina mamlaka ya kuendelea kudai makusanyo hayo,” amesema.