Wanadiplomasia waiweka kati Pakistan
Wanadiplomasia nchini Pakistan wameitaka nchi hiyo kupambana na matukio ya watu kutekwa, kuuawa ili iwe na haki ya kupatanisha mataifa mengine yenye migogoro.
‘’Nchi sasa ipo katika mchakato wa upatanishi wa vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Ni jambo jema lakini tunapaswa kwanza kutibu yanayotusibu sisi na mataifa mengine, doa la Kashmir bado halijatibiwa na hakuna ripoti iliyowekwa wazi,’’ alisema kiongozi wa wanadiplomasia hao, Ilqar Khan.
Wametoa kauli hiyo wakati wakizungumzia kuelekea kumbukumbu ya mwaka mmoja ya shambulio katika eneo la kitalii la Pahalgam, Kashmir inayoongozwa na India lililotokea Aprili 24, mwaka jana na kusababisha vifo vya watu 26.
Shambulio hilo mbali na kukosolewa na mataifa mengi duniani, limevuruga sekta ya utalii na kuongeza mvutano wa kijeshi na kidiplomasia kati ya India na Pakistan zilizoshambuliana kwa siku nne baada ya shambulio hilo eneo la Kashmir.
‘’Kuna watu wamepoteza ndugu na jamaa pale Kashmir, kuna mgogoro katika jimbo la Baluchistan, bado kuna mvutano kati ya Pakistan na Afghanistan na sasa nchi inageuka mpatanishi wa vita ya mashariki ya kati, sisi tunaona si sawa,’’
‘’Tunadhani sasa ni wakati muafaka wa kushughulikia mambo yetu ili tuwe sawa…, na tatizo la kutoshughulikia mambo yetu ndio msingi wa kutokwisha kwa matukio ya watu kutekwa na kuuawa,’’ alisema Khan.
Aliongeza, ‘’Islamabad inajaribu kubadilisha taswira yake ya kimataifa kutoka ile ya tatizo la usalama hadi ile ya mtoa suluhisho. Lakini mkakati huu mara kwa mara unagongana na utata wa ndani wa nchi.’’