Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waogeleaji kunufaika na mafunzo ya kimataifa Dar

Dar es Salaam. Waogeleaji chipukizi nchini wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya kiwango cha kimataifa kupitia programu ya wiki tatu itakayofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza vipaji, kuimarisha uwezo wa makocha wa ndani na kuwajengea wazazi uelewa wa namna bora ya kuwaunga mkono watoto wao katika michezo.

Programu hiyo ya Tanzania Performance Development Series 2026, iliyoandaliwa na RaceBetter kwa ushirikiano na Monti AquaForce, itafanyika kuanzia Julai 28 hadi Agosti 14 katika Kampasi ya Mikocheni ya Shule ya Kimataifa ya Monti.

Mafunzo hayo yataongozwa na kocha wa kimataifa wa uogeleaji na mwanzilishi wa RaceBetter, Ben Lee, anayetarajiwa kuwasili nchini akitokea Marekani.

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Monti, Fatma Fernandes, amesema mpango huo unaweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu unaolenga kuinua mchezo wa uogeleaji nchini kwa kuunganisha utaalamu wa kimataifa na uzoefu wa makocha wa ndani ili kujenga mfumo endelevu wa kukuza vipaji kuanzia ngazi ya watoto hadi ushindani wa juu.

Amesema programu hiyo itaanza kwa warsha ya siku tatu ya kuwajengea uwezo makocha wa uogeleaji, walimu na viongozi wa vilabu kuanzia Julai 28 hadi 30, kabla ya kuendelea na kambi za mafunzo kwa waogeleaji wa makundi tofauti ya umri.

Pia kutakuwa na mafunzo ya bure kwa wazazi kuhusu lishe ya wanamichezo, urejeshaji wa nguvu, kujenga kujiamini na namna ya kuwasaidia watoto wao kufanikiwa ndani na nje ya bwawa la kuogelea.

Akizungumzia programu hiyo, Ben Lee amesema lengo si kuwajengea waogeleaji kasi pekee, bali kuwasaidia kuwa watu wenye uwezo, kujiamini na kujiandaa kukabiliana na fursa na changamoto za baadaye.

Amesema uzoefu wake wa kufundisha waogeleaji wa ngazi mbalimbali, kuanzia maendeleo ya awali hadi Olimpiki, utatumika kushirikiana na makocha wa Tanzania kuimarisha maendeleo ya mchezo huo nchini.