Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Washindi Tuzo ya Kiswahili ya Safal kujulikana Ijumaa

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Alaf Limited, Hawa Bayumi (katikati) akitangaza orodha fupi ya waandishi waliofanikiwa kutinga fainali ya Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika 2025. Wengine kutoka kushoto ni Ofisa Huduma kwa Wateja Tito Maliyalabu, Meneja Msaidizi wa kitengo cha Rasilimali watu Nyamizi Malatu, Meneja Mauzo ya Miradi, Tom Mwita na Ofisa Uhusiano kwa Wateja, Grace Gabriel.

Muktasari:

  • Tuzo hiyo, inayodhaminiwa na Safal Group kupitia kampuni zake tanzu za Mabati Rolling Mills (Kenya) na Alaf Tanzania, ilianzishwa mwaka 2014 na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma wa Ngugi kwa lengo la kuendeleza uandishi wa fasihi za Kiafrika na kuhamasisha utafsiri wa kazi hizo katika lugha nyingine za asili za Afrika.

Dar es Salaam. Washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika kwa msimu wa 10 wanatarajiwa kutangazwa Ijumaa, Julai 24, jijini Dar es Salaam, baada ya waandaaji kutangaza orodha fupi ya miswada tisa iliyofuzu katika vipengele vya riwaya, ushairi na hadithi fupi.

 Tuzo hiyo, inayodhaminiwa na Safal Group kupitia kampuni zake tanzu za Mabati Rolling Mills (Kenya) na Alaf Tanzania, ilianzishwa mwaka 2014 na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma wa Ngugi kwa lengo la kuendeleza uandishi wa fasihi za Kiafrika na kuhamasisha utafsiri wa kazi hizo katika lugha nyingine za asili za Afrika.

Tuzo hiyo imekuwa ikitolewa kila mwaka, isipokuwa mwaka 2020 iliposimamishwa kutokana na janga la Covid-19 duniani.

Akizungumza Julai 20, 2026 wakati wa kutangaza orodha fupi ya walioingia fainali, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa ALAF Limited, Hawa Bayumi amesema :“Tunapotangaza orodha hii fupi, tunayo furaha kuadhimisha miaka 10 ya tuzo hii. Hii ni hatua kubwa iliyofikiwa na Safal Group kupitia kampuni zake tanzu za Alaf Tanzania na Mabati Rolling Mills ya Kenya.”

“Tunawashukuru wadau wetu wote ambao mmekuwa na sisi katika safari hii. Ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kushirikiana na sisi huku Kiswahili kikiendelea kukua duniani.”

Amesema washindi wa tuzo hizo watajinyakulia  zawadi ya  fedha kulingana na vipengele watakavyoshinda.

Amesema mshindi wa kwanza wa riwaya na ushairi ataondoka na Dola 5,000 za Marekani kila mmoja, huku washindi wa pili katika vipengele hivyo wakipata Dola 2,500 kila mmoja. Mshindi wa kipengele cha hadithi fupi atatunukiwa Dola 2,500 za Marekani.

Aidha, ameeleza kuwa washindi watapata fursa ya kazi zao kuchapishwa na kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota Publishers.

"Tayari tumeshatoa zaidi ya Dola 150,000 kwa waandishi zaidi ya 40, mchango ambao umewawezesha kuchapisha zaidi ya vitabu 20 hii ikiwa ni hatua kubwa katika kutangaza lugha ya Kiswahili duniani,” amesema Bayumi.

Amesema mbali na zawadi hizo, machapisho yaliyoshinda pia yatapata fursa ya kuchapishwa kwa Kiswahili na kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota iliyoko nchini Tanzania, ambapo mashairi yaliyoshinda yatatafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kuchapishwa na Mfuko wa Vitabu vya Ushairi wa Kiafrika (APBF).

Kwa mwaka huu, jumla ya kazi 230 kutoka mataifa saba ziliwasilishwa kwa ajili ya kuwania tuzo hizo.

Akitangaza uamuzi wa majaji kuhusu tuzo hizo, Mwenyekiti wa jopo la majaji wa mwaka huu, Profesa Rayya Timammy kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, amesema ushindani wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika 2025 ulikuwa mkubwa kutokana na ubora wa kazi zilizowasilishwa.

Profesa Timammy amesema hali hiyo ilisababishwa na wingi wa kazi zilizowasilishwa zikiwa na vipaji vya hali ya juu na ubunifu wa kipekee ulioonyeshwa na waandishi.

 Majaji wengine walioshiriki katika mchakato wa kusoma na kuteua kazi zitakazoshindanishwa katika tuzo za mwaka 2025 ni Dk Masoud Mohammed wa Chuo Kikuu cha Zanzibar na Profesa Austin Bukenya, aliyewahi kuwa mfanyakazi wa Chuo Kikuu cha Makerere.

Miswada iliyoteuliwa kuingia orodha fupi pamoja na waandishi wake kwa upande wa riwaya ni Ziaka Imetoboka ya Mathew Theuri Maina (Kenya), Mwanamkasi Ndio Basi  ya Salim Hussein Ng’anzi (Tanzania) na Shamba la Mawe ya Dickson Damas Mtalaze (Tanzania).

Kwa upande wa ushairi ni Diwani ya Vizikwa Vya Kale  ya Ali Hilal Ali (Tanzania),  Zigo la Kichwa  ya Maimuna Hashim Maalim (Tanzania) na Rima la Miiko na Balaa ya Lenard Barnaba Mtesigwa (Tanzania).

Katika mikusanyiko ya hadithi fupi ni imo Mbunge Mtarajiwa na Hadithi Nyingine  ya Dominic Maina Oigo (Kenya),  Koti la Karani na Hadithi Nyingine  ya Stallone Joyfully (Tanzania) na Siri ya Mama na Hadithi Nyingine ya Sophia Said Puta (Tanzania).