Prime
Watiania wakutana kero za majimbo na wajumbe
Muktasari:
- Waendelea kujinadi kata kwa kata wakikutana na wajumbe majimboni, wajibu maswali kuhusu kero sugu za wananchi kabla ya kura za maoni Agosti 4, 2025.
Dar es Salaam. Baada ya kuvuka hatua ya mchujo wa awali ndani ya CCM, watiania wa wameendelea kupita kwa wajumbe kuomba ridhaa yao, huku wakikumbana na maswali mazito kuhusu kero sugu za wananchi katika majimbo na kata wanazotaka kuwakilisha.
Katika maeneo mbalimbali, wameshuhudia changamoto zikiwamo za miundombinu, huduma za afya, mikopo kwa wanawake na vijana, maji, vivuko na masoko – ambapo wajumbe wamewataka kueleza kwa kina mikakati ya kuzitatua kabla ya kupigiwa kura ya maoni Agosti 4, 2025.
Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa na wajumbe katika utambulisho huo, ni mikakati ya ushughulikiaji wa kero hizo iwapo watapewa ubunge au udiwani.
Mikutano hiyo, haikuacha vituko kutoka kwa baadhi ya watiania, wengine wakizungumza kwa mikogo na wengine kushindwa kueleza sera zao na kujikuta muda waliopewa unaisha.
Hayo yameshuhudiwa leo, Alhamisi Julai 31, 2025 katika majimbo mbalimbali jijini Dar es Salaam na mikoa mbalimbali, wakati wa ziara za watiania hao kujitambulisha kwa wajumbe.
Wakiwa katika Kata ya Zingiziwa jimboni Ukonga wajumbe wamehoji kuhusu kivuko cha Lubakaya pamoja na barabara.
Kwenye eneo hilo watiania wa udiwani Maige Maganga, Abdillahi Mpate na Seleman Kaniki huku wa ubunge wakiwa Jerry Silaa, Vilote Mbele, Rajabu Nyangasa, Rangi Noma na Alawi Rwegoshora.
Katika hoja ya kivuko, iliyotolewa na Filbert Magulu, amehoji kwa nini baadhi ya wagombea waliokuwa madarakani kwa miaka mitano iliyopita hawakutatua kero hiyo.
Naye, Anna Thomas amesema daraja la Kwa Kichwa limekuwa kero hasa kipindi cha mvua, na kuwahoji wagombea waliokuwa viongozi katika kipindi kilichopita, ni nini wanawajibika nacho huku wakirejea kuwaomba kura.
Mjumbe mwingine, Mtiti Mbasa amezungumzia Barabara ya Zingiziwa kuwa imejaa mashimo na magari ya usafiri wa umma huharibika mara kwa mara, hali inayosababisha kupanda kwa nauli.
Ametaka kufahamu ni hatua gani wagombea watachukua kukabiliana na kero hiyo iwapo watachaguliwa.
Wakijibu maswali hayo Seleman Kaniki amesema kazi ya kushughulikia kivuko hicho ameanza kuifanya kabla ya kuwa diwani hadi kupewa jina la ‘Baba Vivuko’.
“Hivyo mkinichagua, ni wazi kasi hii nitaiongeza kwa kuwa sasa nitakuwa pia na ushirikiano wa karibu na halmashauri katika kuzisemea kero hizo,” amesema.
Mgombea anayetetea nafasi ya udiwani, Maige Maganga amesema: “Barabara karibu zote za Zingiziwa zimeshaombewa fedha na mpango wa eneo la Kwa Kichwa ni kuwekwa daraja kubwa na barabara kutandikwa lami.”
Akijibu kuhusu suala la mikopo, Vilote Mbele amesema atawasaidia wanawake kuondokana na mikopo umiza kwa kuwa kitaaluma yeye ni ofisa mikopo.
“Kwa kuwa mimi kitaaluma ni ofisa mikopo na pia nina taasisi yangu ya mikopo, naahidi nitawasaidia wanawake wa Zingiziwa kuondokana na mikopo hiyo, sio tu kuwapa mikopo, bali pia kuwapa elimu ya namna ya kuitumia,” amesema.
Kuhusu kivuko cha Lubakaya, Mbunge wa Ukonga anayetetea nafasi yake, Jerry Silaa, amesema kupitia mfuko wa jimbo alishapeleka Sh4 milioni kwa ajili ya kutengenezwa na kwa sasa kazi hiyo inaendelea katika ofisi za kata huku akitaka wajumbe hao kumpa nafasi tena ili kuwaletea wananchi wa kata hiyo maendeleo.
Wakati hali ikiwa hivyo Ukonga, Chamazi nako watiania saba wa ubunge walipita katika Kata za Charambe, Kilungule, Chamazi na Mianzini wakieleza mipango yao ikiwemo ujenzi wa miundombinu, soko na suala la afya kama alivyoeleza Zuhura Mazrui.
Kwa upande wake Meleckzedeck Hango, amesema kwa kuwa ana taaluma ya masuala ya fedha atatumia ujuzi wake kuwawezesha wananchi kupata mikopo nafuu.
"Changamoto ya wananchi wetu ni miundombinu, mikopo, maji na afya pamoja na soko, haya nitayafanyia kazi mkinichagua,” amesema.
Hamidu Bobali amesema anafahamu kero wanayopitia wananchi wa Jimbo la Chamazi wakati wa mvua, hivyo ni wakati wake kuaminiwa kuondoa kero hizo.
Naye, Mariam Kambi amesema dhamira yake ni kuwanyanyua wananchi kiuchumi na atakuwa kiongozi bora pamoja na kuhakikisha soko la kisasa Chamazi linajengwa ili kuondoa usumbufu wa wananchi kwenda kufanya manunuzi Kariakoo.
Mbunge wa Mbagala aliyemaliza muda wake, Abdallah Chaurembo amesema kero ya maji, barabara mbovu na huduma za afya atazimaliza akipewa nafasi ya kuwa mwakilishi wao kwa mara nyingine.
"Mna changamoto ya umeme tunakwenda kumaliza tatizo hili na tutajenga shule ili ziwe karibu na wananchi," amesema.
Huku, Munir Adam akiwahakikisha wananchi wa Jimbo la Chamazi kumaliza kero ya maji, ubovu wa barabara ndani ya awamu yake ya uongozi endapo wajumbe watamwamini.
Ahadi hiyo ni sawa na aliyoitoa Mohamed Lubuva aliyeahidi kutatua kero ya maji, umeme, afya na ukosefu wa mikopo kwa wanawake na vijana.
Katika Jimbo la Kigamboni, wagombea sita wameendelea kujinadi mbele ya wajumbe, wakiahidi kuimarisha vivuko, kuendeleza uvuvi wa kisasa, kuboresha miundombinu na kuifanya Kigamboni kuwa kitovu cha utalii wa ndani.
Licha ya ahadi hizo, wajumbe hawakuwapigia makofi wala kuwauliza maswali.
Wagombea hao ni Mponela Matei, Mchange Mchange, Haran Sanga, Cynthia Henjewele, Ally Mandai na Francis Mwakitalu.
Awali, baada ya kufika Pemba Mnazi, shughuli iliyoanza ni kwa wagombea udiwani kujinadi ambao ni Abdulmalick Ally, Lyoba Yamringa, Ahamed Dau na Akiba Simba kwa kila mmoja kupewa dakika tatu.
Baada ya watiania wa udiwani kujitambulisha, ilifikia zamu ya wanaoutaka ubunge, ambao kila mmoja wao alipewa dakika tano kujieleza.
Kama ilivyokuwa kwa Dar es Salaam, katika Jimbo la Simanjiro watiania ni James Ole Millya, Lenganasa Soipey, Timothy Mollel, Mathayo Londross, Mwajuma Bakari na Lekoko Ngitiri walijinadi kwenye tarafa ya Moipo.
Ole Millya ambaye alishawahi kuwa mbunge wa Jimbo hilo mwaka 2015/2020, amesema anaomba ridhaa ili aendeleze maendeleo kwa kuwa alishiriki kwenye ujenzi wa barabara ya lami Mirerani, kuleta maji Orkesumet na mengineyo.
Lenganasa amesema kupitia CCM atahakikisha rasilimali ya madini ya Tanzanite inawanufaisha wananchi wa eneo hilo kwa kuweka mazingira rafiki.
Mollel amesema yeye ndiye kijana mdogo kuliko wote kati ya wagombea, hivyo wananchi wamchague yeye kwani anatumika.
Mwajuma amesema japokuwa yeye ni mwanamke pekee anayegombea, anaomba nafasi kwani kupitia uwezo wa elimu aliyonayo ataweza kuwatetea.
Lekoko amesema akichaguliwa atahakikisha Simanjiro mpya ya maendeleo inapatikana wakati Mathayo amesema yeye ni kijana msomi mwenye uwezo wa kuwaongoza wana Simanjiro na anasikika kiurahisi.
Katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, watiania sita wamejikita katika hoja za miundombinu, maji na kilimo cha kahawa.
Enock Koola, mmoja wa wagombea, ameahidi kuwa daraja kati ya wananchi, Serikali na chama, huku akilenga kuboresha kilimo cha kahawa na kutafuta masoko ya uhakika ya ndizi.
Mgombea mwingine, Prosper Tesha amejikita kwenye suala la ajira kwa vijana, akiahidi kila mwaka atawachukua vijana kati ya 200 hadi 500 kuwapeleka kwenye shughuli za kujipatia kipato, ili kuwaepusha kujiingiza kwenye ulevi.
Kwa upande wake Yuvenal Shirima ameahidi kujenga mahusiano bora kati ya wananchi, chama na Serikali huku, Charles Kimei akiomba nafasi nyingine ili kukamilisha ahadi alizowahi kutoa.
Katika Jimbo la Missenyi, wajumbe wameendelea kutoa ahadi zao huku, Assumpter Mshama, aliyewahi kuwa mbunge wa Nkenge (sasa Missenyi), akiahidi kuanzisha kiwanda cha kutengeneza taulo za kike, mawigi, biskuti na mikate kwa kutumia zao la ndizi maarufu aina ya gonja za Kyaka.
"Natamani kuona Missenyi ikizalisha bidhaa zetu wenyewe kwa kutumia rasilimali zetu. Nitahakikisha wanawake na vijana wanapata mikopo ya riba nafuu kupitia benki ya mikopo nitakayoianzisha," amesema Assumpter mbele ya wajumbe katika kata mbalimbali ikiwemo Kashenye, Kanyigo, Gera na Mtukula.