Polisi, ACT Wazalendo kutifuana taarifa za uhalifu Zanzibar

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Zanzibar limezungumzia tukio la mauaji ya kiongozi wa ACT-Wazalendo, Ali Bakari Ali. Hata hivyo, ACT-Wazalendo limeibuka na kuwajibu polisi

Unguja. Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad amesema viongozi wa Chama cha ACT Wazalendo wanatumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa za uzushi kuhusu kuwapo makundi ya uhalifu na kuwataka waache kuzusha hofu na kuleta taharuki kwa wananchi.

Hamad ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Aprili 2, 2024 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Amesema kwa kipindi cha hivi karibuni kumeshuhudiwa zikisambazwa taarifa kuhusu hali ya uhalifu na usalama kwa masilahi yanayoonyesha dhahiri yana malengo binafsi ya kisiasa akitolea mfano wa iliyotolewa na chama hicho kuhusu mauaji ya Ali Bakari Ali.

Ali ambaye alikuwa katibu wa chama hicho Jimbo la Chaani Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa mujibu wa taarifa ya polisi, anadaiwa kuuawa na watu wawili waliokuwa wanafanya naye biashara hivyo walishindwa kulipana madeni ndio wakachukuliana sheria mkononi.

Hata hivyo, katika taarifa chama hicho iliyotolewa na Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma, Salim Bimani Machi 30, 2024 amesema Bakari alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu baada ya kutekwa, kupigwa na kutupwa na watu wanaosadikika kuwa majambazi.

 “Mazingira ya kifo cha Ali Bakari ni muendelezo wa vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikitokea katika Mji wa Zanzibar, kuendelea kuwepo vitendo hivyo kunaashiria vikundi vya kihalifu bila kudhibitiwa,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma, Salim Bimani

 Pia, ACT ililitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha waliofanya tukio hilo la kinyama wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kisha kutoa taarifa kwa umma waliotenda kosa hilo.

 Hata hivyo, alipozungumza na Mwananchi Digital, Machi 30, 2024 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Gaudianus Kamugisha alisema waliotenda kosa hilo walikuwa wanadaina na Ali (marehemu), hata hivyo, wameshakamatwa na sheria itachukua mkondo wake.

 Aliwataja waliotenda kosa hilo kuwa ni Feisali Makame Khamis (19) ambao kwa pamoja walimshambulia Ali Bakari Ali (62) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali mkono wake wa kulia na shingoni. 

“Chanzo cha tukio hilo Bakari (marehemu) alikuwa anadaiwa na Khamis Nyange Sh1 milioni aliyomkopesha Februari ambapo wote walikuwa wakisambaza vyakula katika hoteli moja iliyopo maeneo ya Pwani Mchangani,” alisema Kamanda Kamugisha.


Kamishna Hamad

Katika taarifa yake kwa umma leo Jumanne Aprili 2 2024, Kamanda Hamad amesema:“Nitumie nafasi hii kuwaasa viongozi wa ACT Wazalendo hususan wanaotumia nafasi zao kusambaza taarifa za upotoshaji zinazoweza kuleta hofu na taharuki kwa jamii waache tabia hiyo.”

 Kamishna Hamad amesema, badala yake ACT watumie fursa walizonazo na majukwaa ya kijamii kukuza mijadala yenye msingi wa ukweli na sera zenye ushahidi ambazo zitasaidia kubaini vyanzo vya uhalifu na kushauri mikakati ya kuvishughulikia ili kuzuia uhalifu usitokee.

Amesema madai ya chama hicho ya kuwapo vikundi vya kihalifu vinavyojiimarisha kila siku bila Jeshi la Polisi kuonesha uwezo wa kudhibiti kwa kukinga au kufanya upelelezi unaosababisha wahusika kutiwa hatiani, ni upotoshaji.

Amesema madai hayo ni uthibitisho wa utamaduni endelevu wa baadhi ya viongozi wa chama hicho kutothamini juhudi za Serikali na taasisi zake katika kudumisha amani na utulivu. 

“Sote tunatambua athari kubwa za usambazaji taarifa potofu na za kutia chumvi kwenye jamii na kwa kutumia mitandao ya kijamii, zinaweza kuanzisha hofu na wasiwasi hata kama hatari halisi ya kutendewa uhalifu ni ndogo au haipo, kuchochea ubaguzi na mgawanyiko,” amesema Kamishna.

Kwa mujibu wa Kamishna, mmomonyoko huo wa kimaadili katika matumizi ya mitandao ya kijamii unaweza kuzuia juhudi za kushughulikia masuala ya uhalifu halisi kwa ufanisi na kwa ushirikiano baina jamii na vyombo vinavyotekeleza sheria. 

Ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi kwa jumla wana uwezo mkubwa wa kudhibiti uhalifu wa aina yoyote. 

Amewataka wananchi kuyapuuza madai ya chama hicho akisema hayana ushahidi wowote akisema kwamba wataendelea kuhakikisha ulinzi na usalama vinadumishwa kikubwa ni kutoa ushirikiano katika kudhibiti uhalifu huo.

ACT wajibu

Baada ya kauli hiyo, Mwananchi Digital limemtafuta Bimani kuhusu kauli za Kamishna Hamad ambaye amesema nia ya chama hicho hakina nia ya kuwatisha watu bali matukio ya kiuhalifu wamekuwa wakiyaripoti polisi wenye mara kwa mara.

“Haya matukio wamekuwa wakiripoti mara kwa mara, watu kuvamiwa, kupigwa na kuibiwa si kama ni mambo ambayo sisi tunayaleta, haja yetu Jeshi la Polisi lizidishe shughuli zake za kiintelijensia na shughuli za kulinda amani,” amesema Bimani na kuongeza:

“Sisi kama chama, kazi yetu ni kuishauri jeshi la polisi kwasababu vitendo vya kihalifu vimekuwa vikitokea na vikiripotiwa, sisi hatuna nia ya kutisha watu, haja yetu liendeleze taratibu hizo katika hali ya amani na usalama.” 

Hata hivyo, Bimani amesema Jeshi la Polisi linatakiwa kuwa wepesi kupokea ushauri.