Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

20 wapoteza maisha wakizama kwenye madimbwi ya mchanga, kokoto

Kaimu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Shariff Ali Shariff akijibu maswali barazani leo Alhamis Juni 18, 2026.

Muktasari:

  • Mbali na vifo, uchimbaji umesababisha uharibifu wa miti mbalimbali, ikiwemo minazi na miti ya matunda, hivyo kuathiri bioanuwai na mifumo ya ikolojia.

Unguja. Watu 20 wamepoteza maisha kati ya mwaka 2008 na 2023, wengi wao wakiwa watoto, kutokana na maji ya mvua kutuwama kwenye machimbo yaliyoachwa bila kurekebishwa baada ya shughuli za uchimbaji wa maliasili zisizorejesheka.

Taarifa hiyo imebainishwa katika Ripoti ya Athari za Kimazingira Zitokanazo na Uchimbaji wa Maliasili Zisizorejesheka ya mwaka 2023, iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar.

Matokeo ya ripoti hiyo yamewasilishwa leo, Alhamisi, Juni 18, 2026, katika Baraza la Wawakilishi wakati wa kipindi cha maswali na majibu, kutokana na swali la mwakilishi wa jimbo la Ziwani, Mohamed Ali Salim (ACT-Wazalendo), aliyetaka kufahamu matokeo ya utafiti kuhusu athari za shughuli za uchimbaji wa mchanga, ubanguaji wa kokoto na uchomaji wa mkaa kwa mazingira.

Akijibu swali hilo, Kaimu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Shariff Ali Shariff, amesema ripoti hiyo imeeleza kwa kina hali halisi ya shughuli za uchimbaji wa maliasili zisizorejesheka, changamoto zake pamoja na athari zinazojitokeza kwa mazingira na jamii zinazozunguka maeneo hayo.

Amesema moja ya athari kubwa zilizobainika ni uwepo wa mashimo makubwa yanayobaki baada ya uchimbaji, ambayo hujaa maji ya mvua na kuwa hatari kwa wananchi, hususan watoto.

 “Hatari ya maji kutuwama kwenye machimbo ni kubwa. Kati ya mwaka 2008 hadi 2023, watu 20 wamepoteza maisha, wengi wao wakiwa watoto, kutokana na maji ya mvua kutuwama kwenye machimbo yaliyoachwa bila kurekebishwa,” amesema Shariff.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jumla ya wananchi 2,925 katika maeneo ya Unguja na Pemba wanajihusisha na shughuli za uchimbaji wa maliasili zisizorejesheka.

Takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa sekta hiyo katika kujiongezea kipato kwa wananchi, lakini pia zinaibua haja ya kuimarisha usimamizi wa shughuli hizo ili kupunguza madhara kwa mazingira.

Ripoti hiyo pia imebaini uwepo wa machimbo 277, yakiwemo 233 Unguja na 44 Pemba, yenye ukubwa wa takribani hekta 2,144.

Mbali na vifo, shughuli za uchimbaji zimechangia uharibifu wa miti mbalimbali, ikiwemo minazi na miti ya matunda, hali iliyosababisha kupungua kwa bioanuwai, kuharibu mifumo ya ikolojia na kuathiri matumizi endelevu ya ardhi.

Shariff amesema Serikali inaendelea kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo kwa kuimarisha udhibiti wa shughuli za uchimbaji, kutafuta vyanzo mbadala vya maliasili kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuweka utaratibu wa matumizi mengine ya maeneo yaliyochimbwa ili yaweze kunufaisha jamii na uchumi wa nchi.