ACT wataka tume ya uchunguzi mfumo wa utoaji ZAN ID
Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ndogo za Chama hicho Vuga, Zanzibar.
Muktasari:
- Hatua hiyo inalenga kulinda haki na hadhi ya Mzanzibari ndani ya Muungano kwa kile kinachodaiwa kuna utoaji holela wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi.
Unguja. Mjadala kuhusu haki za Wazanzibari, ulinzi wa utambulisho wao na mustakabali wa Muungano umechukua nafasi kubwa ndani na nje ya Baraza la Wawakilishi, huku masuala ya uraia na upatikanaji wa Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (Zan ID) yakizidi kuibua maswali kutoka kwa wadau mbalimbali.
Katika mazingira hayo, Chama cha ACT-Wazalendo kimezitaka Kamati za Baraza la Wawakilishi zinazoshughulikia sheria, utawala na Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali kuanzisha uchunguzi wa kibunge kuhusu mifumo yote ya utoaji wa Zan ID.
Kwa mujibu wa ACT-Wazalendo hatua hiyo itasaidia kubaini kama taratibu zilizopo zinalinda kikamilifu hadhi, haki na utambulisho wa Mzanzibari.
ACT Wazalendo kinasema uchunguzi huo ni muhimu ili kubaini kama mifumo iliyopo inalinda kikamilifu hadhi ya Mzanzibari na kuhakikisha utaratibu wa utoaji wa vitambulisho hivyo unazingatia sheria, kanuni na masharti yaliyowekwa.
Hoja ya ACT Wazalendo imekuja kufuatia kauli iliyotolewa hivi karibuni Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Idrissa Kitwana Mustafa, alipokuwa akijibu maswali kuhusu masuala ya Muungano na mchakato wa upatikanaji wa Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi (Zan ID) unaosimamiwa na wizara yake.
Katika ufafanuzi wake, Kitwana alisisitiza kuwa Muungano wa Tanzania hauwezi kuvunjika kwa kuwa haujajengwa katika misingi ya kisiasa pekee, bali unagusa maisha ya kila siku ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Kauli hiyo ilifungua mjadala mpana kuhusu masuala ya utambulisho wa Mzanzibari, masharti ya upatikanaji wa Zan ID na nafasi ya mfumo huo katika kulinda haki na hadhi ya wazawa wa Zanzibar.
“Katiba imeweka wazi kumtambua mzanzibari ni nani na iwapo mtu akiishi miaka 10 akiwa Zanzibar anaruhusiwa kupewa kitambulisho cha Zan ID, na ili awe Mzanzibari tayari anakuwa ni Mtanzania,” alisema Kitwana
Hata hivyo, kauli hiyo imezua mjadala mpana, huku ACT Wazalendo kikitaka kuwepo kwa tathmini ya kina ya mifumo ya utoaji wa Zan ID, wakidai suala hilo linagusa moja kwa moja masuala ya uraia, utambulisho wa Mzanzibari na usimamizi wa haki za wananchi.
Akizungumza leo Juni 24, 2026 na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Vuga Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omar Said Shaaban amesema hakuna Muungano wenye afya unaojengwa kwa kufuta hadhi na haki za washirika wengine.
“Tunaitaka kamati ya Baraza la Wawakilishi inayohusika na masuala ya sheria au inayosimamia ofisi za viongozi wakuu wa serikali kuanzisha mara moja uchunguzi wa kibunge na kupitia mifumo yote ya utoaji wa Zan ID na vitambulisho vya wageni,” amesema na kuongeza;
“Kuulinda Uzanzibari ndio kuulinda Muungano wenyewe, maana huko ni kulinda hadhi na heshima ya mmoja wa wazazi wa Muungano huo yaani Zanzibar. Huwezi kuwa na nchi yenye maisha ndani ya Muungano ikiwa unajenga utaratibu unaoyaangamiza maisha,” amesema
Kwa muibu wa Shaaban, utaratibu wa kulinda hadhi ya uenyeji upo hata Tanzania Bara “iweje hapa Zanzibar ikiongelewa inaonekana ni fitina? Amehoji.
Amesema kauli ya Waziri huyo inarahisisha jambo ambalo kisheria lina mlolongo mkali akitaja kifungu cha nne cha sheria ya Mzanzibari namba tano ya mwaka 1985 kwamba kipo wazi ambapo haisemi ukiishi Zanzibar miaka 10 basi unakuwa Mzanzibari moja kwa moja.
“Ili anayeishi Zanzibar apewe hadhi ya Uzanzibari kwa njia ya kuishi, lazima akidhi masharti yote ya kifungu cha nne kwa pamoja ambayo ni pamoja.
“Awe ameishi Zanzibar mfululizo kwa muda uliowekwa kisheria, awe na uwezo wa kutosha wa kuandika na kusoma lugha ya Kiswahili, awe na tabia nzuri inayokubalika katika jamii, awe ameingia Zanzibar kihalali na awe na nia thabiti ya kuendelea kuishi Zanzibar,” amesema.
Amesema kurahisisha utaratibu huo na kuufanya uonekane ni suala aliliita la kuhesabu miaka tu, pasipouchunguzi wa vigezo vyote vyenye kulinda hadhi ya nchi ni ukiukwaji wa dhamira wa sheria husika.
Kutokana na hali hiyo, Chama kimeitaka kamati ya Baraza la Wawakilishi inayohusika na masuala ya sheria au inayosimamia ofisi za viongozi wakuu wa Serikali kuanzisha uchunguzi wa kibunge na kupitia mifumo yote ya utoaji wa Zan ID na vitambulisho vya wageni.
Pia, chama hicho kimewataka viongozi wa Serikali kuishi ndani ya viapo vyao, kwani waliapa kulinda sheria na maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari.