Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yaliyotikisa mjadala wa bajeti Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu ambaye ni Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk Saada Mkuya

Unguja. Wakati Baraza la Wawakilishi likihitimisha siku 47 za mjadala wa bajeti na kupitisha makadirio ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Sh8.5 trilioni, si takwimu za fedha ndizo zilizoacha alama kubwa kwa wananchi, bali mijadala miwili iliyogusa moja kwa moja masuala nyeti ya Muungano, ajira na afya.

Hoja hizo ziliibuka kwa nyakati tofauti zikitokana na kauli ya Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum, kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) haiwezi kugharamia matibabu kwa watu wasio Wazanzibari.

Pia, hoja nyingine ilitokana na kauli ya Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh, aliyesema kuwa idadi kubwa ya wafanyakazi katika sekta ya hoteli visiwani humo si wazawa.

Kauli hizo za mawaziri ziliibua mjadala hadi kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambapo baadhi ya wabunge nao walizungumzia hoja hiyo, huku Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba akiwasihi viongozi kuepuka kauli zinazoweza kuwagawa Watanzania.

Mbali na hilo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, akitoa hotuba ya kuahirisha kikao cha Baraza la Wawakilishi Juni 23, alitoa ufafanuzi kuhusu masuala ya ajira na matibabu, akisisitiza kuwa huduma zitatolewa kwa watu wote wenye sifa bila ubaguzi.

Pia alisema Muungano utaendelea kulindwa kwa nguvu zote kwani manufaa yake yanaonekana wazi, akionya dhidi ya watu wanaotumia fursa hiyo kujitafutia umaarufu wa kisiasa na mitandaoni.

Alisema pande zote za Muungano zina sheria mahsusi za matibabu kupitia bima, na iwapo mwananchi ana bima inayotambulika, atapata huduma upande wowote wa Muungano bila changamoto. Aliwataka wananchi kujisajili kwenye bima hizo ili kuepuka changamoto za kukosa matibabu.

“Tunapenda kuwafahamisha wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwamba suala la fursa za ajira na huduma zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kwa watu wote waliomo ndani ya visiwa vya Zanzibar bila kuangalia rangi, kabila, dini wala siasa,” alisema.

Awali, Dk Saada alipokuwa akijibu maswali barazani kuhusu matibabu bure kwa watu wasiokuwa wazawa ilhali Wazanzibari wakikosa huduma hiyo, alihoji mwenendo wa wageni kutibiwa visiwani humo kupitia kadi ya matibabu, ambayo ni maalumu kwa Wazanzibari.

Alisisitiza kuwa bajeti ya Zanzibar ya Sh8 trilioni haiwezi kubeba gharama za matibabu kwa watu milioni 60, kauli ambayo iliibua mjadala mkubwa, hasa kwa wananchi wa Tanzania Bara waliopokea kauli hiyo kama ya kibaguzi.

“Bajeti yetu ya trilioni 8 tutaweza kuwatibu watu milioni 60? Tumeona wengine si Wazanzibari wanatibiwa kwa kutumia kadi ya matibabu, hili haliwezekani,” alisema Waziri Saada bungeni.

Vilevile, Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hassan Khamis Hafidh maarufu (Diaspora), wakati akichangia bajeti ya wizara yake, alisema Zanzibar ina hoteli 1,184 (sio takwimu rasmi) zilizosajiliwa, lakini wafanyakazi wengi katika hoteli hizo si Wazanzibari, akisema ni lazima kufanyika “mapinduzi”.

Alitoa mfano wa hoteli moja aliyoitembelea yenye wafanyakazi 157, ambapo kati yao ni 27 pekee waliokuwa Wazanzibari, na wengine wageni, hivyo akaomba wajumbe waunge mkono bajeti ili kuongeza ajira kwa wazawa.

Hata hivyo, alifafanua kuwa changamoto hiyo inatokana na baadhi ya vijana wa Kizanzibari kupendelea zaidi kazi za serikalini kuliko sekta binafsi, hivyo akawataka wawakilishi kushirikiana na wizara kubadili mtazamo huo.


Mijadala mtandaoni

Pamoja na mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii, hoja hizo ziliendelea kutawala pia ndani ya Baraza la Wawakilishi wakati wa michango ya wajumbe katika kujadili bajeti za wizara na bajeti ya Serikali.

Mwakilishi wa nafasi za Wanawake, Jabu Kame Juma (ACT-Wazalendo), alisema licha ya Muungano kuwepo, kila upande unatakiwa kuheshimiana, akidai Zanzibar imekuwa ikikumbwa na changamoto za “kudharauliwa” ndani ya Muungano.

“Zanzibar imekuwa koloni kwa muda mrefu ndani ya Muungano,” alisema.

Naye Mwakilishi wa Ziwani, Mohamed Ali Salim (ACT-Wazalendo), alisema hata ajira chache zilizopo zinachukuliwa na watu wa upande wa pili, akiongeza kuwa kukosoa hilo huonekana kama kupinga Muungano.

“Mie kama mwakilishi wa Ziwani naendelea kutetea na kuwaombea vijana. Na kama hii ndiyo sababu ya kuvunjika kwa Muungano, basi uvunjike, kwa sababu ajira ninazoziomba ni halali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, ingawa tafsiri zinatofautiana,” alisema.

Akichangia mjadala huo, Mwakilishi wa Kwahani ambaye pia Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mohammed Sijamni Mohammed, alionya dhidi ya kauli alizodai kuwa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wawakilishi ndani ya chombo hicho.

“Kama kuna watu wanaonufaika ndani ya Muungano ni sisi Wazanzibari. Ifike hatua tuseme ukweli, sisi sasa tunalalamika nini? Tunyamaze badala yake tutumie fursa hii kuwaelimisha watu wetu badala ya kupotosha,” alisema Sijamni.

Naye Mwakilishi wa Amani, Masoud Amour Masoud (CCM), alisema kuna mafanikio makubwa ya Muungano kutokana na ushirikiano na mwingiliano mkubwa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, akionya dhidi ya wanaoubeza Muungano kwa kutaka kuleta chokochoko. Alisema changamoto kubwa ni kwa Wazanzibari kuchagua kazi.

Kuhusu upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi vinavyosimamiwa na wizara yake, Kitwana alisema suala hilo lipo wazi kikatiba.

“Katiba imeweka wazi kumtambua Mzanzibari ni nani, na iwapo mtu akiishi miaka 10 akiwa Zanzibar anaruhusiwa kupewa kitambulisho cha ZAN ID, na akitambuliwa hivyo tayari anakuwa ni Mtanzania,” alisema.