ACT Wazalendo mguu sawa uchaguzi 2025, yajivunia Pemba

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Juma Duni Haji akisistiza jambo alipokua akizungumza na viongozi wa chama hicho katika ofisi za Jimbo Mtambile Pemba. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Amesema umoja na mshikamo unaoneshwa na wananchi wa Pemba umekua nguzo muhimu ambayo itakipelekea Chama hicho kuibuka washindi katika uchaguzi mkuu 2025.

Pemba. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Juma Duni Haji amesema uongozi imara wa chama hicho kisiwani Pemba, ni nguzo muhimu na kwamba anaamini chama chao kitaibuka na ushindi katika Uchaguzi Mkuu 2025.

Duni ameyasema hayo leo Novemba 18 wakati akizungumza na viongozi wa chama hicho Wilaya ya Mkoani, katika ukumbi wa Jimbo la Mtambile.

Amesema kuendelea kuimarika kwa chama hicho kila leo kunatokana na umoja na mshikamano ambao viongozi wamekua wakionesha kwa miaka yote.

"Nataka niseme leo kuwa Pemba itabakia kuwa ngome yetu na CCM hawataambulia chochote labda watumie nguvu ya dola kwenye Uchaguzi Mkuu 2025,” amesema Duni

Pia amesema kuna haja wananchi walio wengi kuendelea kukiunga mkono chama hicho wakijua kuwa ndio mkombozi wao.

Pamoja na hayo mwenyekiti huyo amesema Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kupiga hatua zaidi kimaendeleo kuliko ilivyo sasa iwapao itakua na uwezo wake wakujiamulia mambo yake kama nchi huru.

Katika hatua nyengine Katibu wa Mipango na Chaguzi katika chma hicho, Omar Ali Shehe amewataka wanachama wao kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji lililotangazwa na Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC)

Amesema uandikishaji wapiga kura wengi zaidi ni jambo muhimu ambalo linapaswa kuratibiwa hivi sasa.

"Ni lazima mfahamu uchaguzi ni namba ushindi hasa wa uchaguzi upo kwenye uandikishaji hivyo natoa wito wote tujitokeze mapema sana tukajindikishe" alisisitiza.

Awali Mwenyekiti wa mkoa huo kichama, Rashid Abdallah (Habuba) amewataka wanachama na viongozi wenzake wote kuacha woga na kusimamia haki kwani vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa katiba.