Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwinyi aeleza atakavyofungua Pemba

Mgombea urais kupitia CCM Dk Hussein Mwinyi akizungumza wakati wa kuzindua kampeni za chama hicho upande wa Pemba katika viwanja vya Gombani ya Kale Mkoa wa Kusini Pemba

Muktasari:

  • Asema awamu inayofuata inalenga mabadiliko makubwa kisiwa hicho, akiwahimiza wananchi kuendelea kuichagua CCM.

Unguja. Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, amesema Pemba inafunguka kupitia bandari na uwanja wa ndege wa kimataifa, ambao mwezi huu wanamkabidhi mkandarasi kuanza ujenzi.

Pamoja na miradi hiyo, Dk Mwinyi amesema neema inakwenda kuwashukia wakulima wa karafuu na mwani, kwani tayari Serikali inayoongozwa na CCM imeshaweka mikakati mikubwa ya kuinua mazao hayo, yatakayokuza uchumi wa wananchi.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Septemba 15, 2025, wakati akizindua kampeni za chama hicho kwa Upande wa Pemba katika viwanja vya Gombani ya Kale, Mkoa wa Kusini Pemba.

"Ndugu zangu, hakuna sababu kwa nini Pemba isifunguke. Septemba 25 tunamkabidhi mkandarasi kuanza ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Pemba. Pia kuna bandari zilizojengwa na zinaendelea kujengwa. Pemba itafunguka," amesema Dk Mwinyi.

Mbali na uwanja wa ndege, amesema pia mkandarasi huyo atakabidhiwa ujenzi wa barabara ya Chakechake, mkoani Pemba, itakayokuwa kiunganishi cha usafirishaji kutoka bandari ya mkoani kwenda maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho.

Amesema bandari za Mkoani na Shumba zinakwenda kubadilisha uchumi wa Pemba, kwani meli kubwa za kimataifa zitakuwa zinashusha mizigo yake moja kwa moja katika bandari hizo.

Akizungumza kuhusu karafuu, Dk Mwinyi amesema, licha ya zao hilo kuwa zao kuu la biashara kisiwani humo, wananchi walikuwa wamekataa tamaa na kuyatelekeza mashamba.

Hata hivyo, amewataka wakulima waanze kuyafufua mashamba yao, akisema neema inakuja kwani wanakwenda kuliweka mazingira mazuri.

"Zao letu la karafuu limekuwa likipata changamoto, na imefika hatua wakulima wakayatelekeza mashamba. Sasa nawaambia kila mwenye shamba lake alishikilie, tuyatunze, neema inakuja," amesema.

Mgombea urais wa CCM Dk Hussein Mwinyi akionyesha kadi za wanachama wa ACT Wazalendo aliowapokea leo na kuhamia chama hicho kisiwani Pemba

Kuhusu mwani, Dk Mwinyi amesema wanakwenda kuongeza vifaa kwa wakulima na tayari wamejenga kiwanda cha Manangwe, kitakachotumika kuchakata zao hilo.

"Tutaendelea kuwapa vifaa vya kisasa, tutanunua zao hilo kuchakata kiwandani, hivyo hakutakuwa na tatizo tena la soko. Haya ndio tunakwenda kuyamalizia," amesema Dk Mwinyi.

Amesema katika awamu ijayo, iwapo wakipewa ridhaa, wanataka kuleta mabadiliko makubwa hususani katika kisiwa hicho.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuendelea kuichagua chama hicho ili wakamilishe mambo mazuri waliyoyaanza, huku akitupa donge kwa wapinzani wake kwamba hawana sera.

"Msidanganywe na chochote. Kwanza, hao hawana sera. Haya tuliyoyasema hapa mmeshasikia wanayasema," amehoji huku wananchi wakimjibu kwa kusema hapana.

Awali, akimkaribisha Dk Mwinyi na kumwombea kura, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha Rose Migiro, amesema Serikali ya awamu ya nane inastahili kuungwa mkono kwa sababu imefanya mambo makubwa ambayo hayajawahi kufanyika.