Dk Mwinyi ahimiza hofu ya Mungu kwa watumishi wa umma

 Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi

Muktasari:

 Dk Mwinyi amesema hayo aliposhiriki kongamano la kiimani kwa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) lililofanyika leo Aprili 6, 2024 Unguja

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi  amewahimiza viongozi na watumishi wa umma kubadilika na kutekeleza majukumu yao wakiwa na hofu ya Mungu ili kulitumikia Taifa kwa haki na uadilifu.

Dk Mwinyi, ametoa kauli hiyo aliposhiriki kongamano la kiimani kwa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) lililofanyika leo Aprili 6, 2024 Unguja.

Amesema matarajio yake baada ya kongamano hilo ni kuona mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa watumishi na wateule aliowapa majukumu ya kumsaidia kwenye utendaji na weledi wa kufanya kazi za kuwatumikia wananchi.

"Ni matarajio yangu tutatoka na kitu tofauti hapa baada ya kongamano hili kwa  kuwa limemgusa kila mmoja wetu, kazi iliyopo mbele ni muhimu kujitathmini na kurekebisha upungufu uliopo.”

Akizungumzia masuala ya utawala bora, nidhamu na maadili kwenye utumishi wa umma alieleza, ni msingi imara wa kutengeneza njia sahihi badala ya kufanya yasiyofaa.

Amesema baadhi ya watendaji wanakosa nidhamu ya utumishi wa umma na kuwataka wabadilike na kujenga uaminifu.

Kuhusu masuala ya usimamizi wa kodi, Dk Mwinyi amesisitiza haja ya kuzisimamia kwa haki na uadilifu wa hali ya juu pasipo kudhulumu watu.

Amesema, kodi ni muhimu katika kufanikisha huduma bora za jamii na kueleza umuhimu wake umetajwa kwa kina hata kwenye vitabu vitukufu vya dini.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema kongamano hilo ni darasa lililowafunza viongozi wengi na kuwakumbusha kwenye wajibu wao wanaopaswa kutumikia umma kwa uadilifu kila siku.

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi,  Zena Saidi amewataka watumishi wa umma kwendana na mabadiliko na wao kujihisi kama sehemu ya jamii wanayoitumikia.

Said amesema suala la uadilifu ni pamoja na kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa saa zote zilizopangwa na kufanya vinginevyo ni kwenda kinyume na sheria.

Hivyo, amewaeleza viongozi za Serikali na watumishi wa umma kujitafakari na kujitathmini wanapovunja uaminifu kwenye utendaji wao sambamba na kuwaeleza kuwa wanabeba dhima kubwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kutokuwa waadilifu kwenye kazi zao.

Sheikh Muhamad Al Hajir na Sheikh amesema utumishi wa umma unahitaji nidhamu ili kwenda sambamba na matakwa ya Mungu.

Kongamano hilo la kiimani kwa viongozi na watendaji wakuu wa SMZ  lilitayarishwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kuratibiwa na Ofisi ya Mufti, Zanzibar pamoja na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.