Dk Mwinyi: Tumuenzi Karume kuendeleza umoja wa kitaifa

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akisoma hotuba katika kongamano la sita la kumbukumbu ya Hayati Abeid Amani Karume lililofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Karume, Unguja.

Muktasari:

  • Stephen Wasira amesema historia ya Zanzibar bila kumuandika Abeid Amani Karume itakuwa butu.

Unguja. Wakati ikikumbukwa miaka 52 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema muasisi huyo wa Taifa alijenga upendo na umoja wa kitaifa, hivyo lazima kumuenzi kwa kuendeleza falsafa zake.

Amesema kuna mengi ya kujifunza kupitia maisha yake.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Aprili 4, 2024 katika hotuba iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla kwenye kongamano la sita la kumuenzi Karume lililoandaliwa na kufanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Unguja, Zanzibar.

"Mzee Karume alijenga upendo na umoja wa kitaifa, misingi bora ya kiuchumi, kuleta haki na kupambana na dhuluma, hivyo tuna wajibu wa kumuenzi kama ambavyo tunayathamini na kuyaenzi Mapinduzi matukufu, kwani yeye ndiye kinara," amesema Dk Mwinyi.

Amesema katika kipindi hiki cha miaka 52 bila Karume, wanapata kurejea hekima na falsafa zake kwa kujikumbusha misingi ya utendaji wenye kuacha alama katika maisha na mifumo mbalimbali katika Serikali.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, kupitia mikusanyiko kama hiyo iwe chachu kwa kila mmoja kuziishi fikra za Karume, ili kuendeleza na kukuza uzalendo kwa wananchi.

Amesema Mzee Karume hakuwa mtu mwenye hasira, bali alikuwa mwenye kupenda watu, mwenye bashasha, anayesaidia watu na ushirikiano kwa kila mtu.

“Kwa hakika hizi ni sifa muhimu kwa kila kiongozi kujipamba nazo katika usimamiaji wa majukumu yetu ya kila siku,” amesema.

Dk Mwinyi amesema katika kumkumbuka Karume ni vyema kurejea katika misingi ya falsafa za uwazi, uadilifu, ushirikishwaji, upendo amani na ubunifu kama ambavyo aliziishi katika maisha yake na ujenzi wa Taifa.

“Ni imani yangu tutaziishi tunu hizi alizotuachia Karume ambazo zitabadilisha fikra na mienendo na kuleta utendaji wenye kuboresha maisha ya wananchi,” amesema.

Amesema mambo aliyofanya Mzee Karume ni vyema kuyaweka kwenye vitendo kwa ajili ya ujenzi wa Taifa, na kwamba jina hilo haliwezi kusahaulika katika historia ya ukombozi wa visiwa vya Zanzibar.

Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Stephen Wasira amesema haiwezi kuandikwa historia ya Zanzibar bila kumuandika Karume, na iwapo kuna mtu akifanya hivyo historia hiyo itakuwa butu.

"Huwezi kuiandika historia ya Zanzibar ukaitenganisha na Karume, historia hiyo itakuwa butu," amesema.

Amesema historia ya Zanzibar inajengwa katika mambo makuu matatu aliyoyataja kuwa ni Zanzibar kabla ya Mapinduzi, Zanzibar wakati wa Mapiduzi na Zanzibar baada ya Mapinduzi.

Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha amesema kipindi cha ukoloni watu walidhulumiwa na kugawanywa katika matabaka matatu; Wazungu, watu wenye asili ya Asia na Waafrika.

Amesema baada ya Karume kuingia madarakani alikuta wananchi wamegawanyika, hivyo kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kuwaunganisha pamoja.

Amesema alitumia njia za kutoa elimu bure, afya na ardhi bure, akijenga makazi kwa ajili ya wananchi.

"Upo uhusiano mkubwa kati ya maendeleo na amani, penye amani maendeleo yatapatikana, hivi vitu haviwezi kutenganishwa kama ulivyo mjadala wa kuku na yai nani alianza," amesema.

"Tukiwa na Amani, umaskini utaondoka na umaskini ukitoweka maendeleo yatapatikana; lakini kinyume chake kama hakuna amani maendeleo hayatapatikana," amesema.

Profesa Palamagamba Kabudi amesema unapozungumzia uzalendo lazima ufungamanishe uraia na utambulisho.

Amesema uzalendo si kitu cha kutamka mdomoni badala yake unatakiwa kuishi nao.

Profesa Kabudi amesema ni lazima uwapende na kuwathamini viongozi na kushiriki shughuli za maendeleo.

Amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ndiyo Muungano pekee uliobaki katika miungano yote ya hiari iliyowahi kufanyika duniani, hivyo walioasisi muungano huo waliweka mikakati mizuri ambayo bado inatakiwa kuendelezwa hadi sasa.

Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila amesema pamoja na kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho ambazo ni zaidi ya 30, pia kinashirki kikamilifu katika kuendeleza amani na umoja wa kitaifa.

Amesema chuo hicho kinafundisha masuala ya uongozi na maadili na katika mitalaa yake kimeanzisha somo la maadili.

Amesema kuendeleza makongamano kuhusu kumbukizi ya Karume, ni kuwaleta pamoja, wazee wasomi na vijana kujikumbusha mchango wa Karume katika maendeleo ya elimu na uchumi.