Dk Mwinyi aitaka PBZ kutobweteka kwani hawajafika malengo
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika kilele cha miaka 60 ya benki ya watu wa Zanzibar(PBZ) kilichofanyika Golden Tulip, Uwanja wa Ndege.
Muktasari:
- Kauli hiyo ameitoa leo Juni 30, 2026 katika kilele cha sherehe za miaka 60 ya uaminifu ya benki hiyo, kilichofanyika, Golden Tulip Uwanja wa Ndege mjini Unguja.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeitaka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) isibweteke kwani hawajafika wanapotakiwa licha ya kujivunia kuwa taasisi ya kifedha yenye msaada katika ukuzaji uchumi wa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 30, 2026 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika kilele cha sherehe za miaka 60 ya uaminifu ya benki hiyo, kilichofanyika, Golden Tulip Uwanja wa Ndege mjini Unguja.
Amesema walipo sasa bado hawajafika kwa maana hiyo kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanasonga mbele.
“Mimi ni miongoni mwa watu tunaotaka kuiona benki ya PBZ kutoka nafasi ya sita ilipo sasa hadi tuzungumzie nafasi ya kwanza au ya pili na uwezo huo upo kwani Serikali ipo tayari kutoa kila aina ya msaada kwao,” amesema Dk Mwinyi.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika kilele cha miaka 60 ya benki ya watu wa Zanzibar(PBZ) kilichofanyika Golden Tulip, Uwanja wa Ndege.
Vilevile, Dk Mwinyi amesema katika kufanikisha hayo, PBZ inapaswa kuimarisha mtaji wake, kupanua huduma za kidijitali, kuongeza ubunifu, kuendelea kuwawezesha vijana na wanawake, kukuza uwekezaji katika rasilimali watu, kuimarisha utawala bora na usimamizi na kuendelea kuwa mshirika wa Serikali katika ajenda za maendeleo.
Amesema mafanikio ya benki hiyo yanadhihirisha kuwa uwekezaji wa Serikali unaweza kuleta matokeo makubwa pale patakapokuwa na uwajibikaji, ubunifu na usimamizi madhubuti.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza dira ya maendeleo yenye lengo la kujenga uchumi wa kisasa, jumuishi na shindani.
Hivyo, katika kufanikisha utekelezaji wa maendeleo sekta ya fedha imeendelea kuwa muhimili wa kuchochea mafanikio hayo kwani hawawezi kuwa na uchumi bora bila ya kuwa na taasisi za kifedha imara.
Akitoa maelezo mafupi katika sherehe za kilele hicho, Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ, Fahadi Soud Hamid amesema wanajivunia mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa benki hiyo.
Amesema PBZ imeishi kwenye maono ya marais wote waliopita wenye lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Amefafanua kuwa benki hiyo imetoka katika taasisi changa hadi kuwa benki kubwa ya Tanzania yenye ushawishi inayoshika nafasi ya sita kwa rasilimali.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi PBZ, Dk Juma Hassan.
Amesema katika miaka 60 iliyopita PBZ imebadilika kutoka taasisi changa ya kifedha hadi kuwa benki kubwa Tanzania kwa kuyaishi maono ya kuanzishwa kwake, ambapo sasa ni benki ya sita kiukubwa kwa rasilimali za Sh3 trilioni na kutengeneza faida ya Sh110 bilioni.
Mbali na hilo, amesema benki hiyo imeweza kupanua wigo kwa kuongeza idadi ya matawi zaidi ya 50 Tanzania nzima ambapo mafanikio hayo yasingewezekana bila kuwa na maendeleo chanya nchini.
Naye, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Hamad Omar Bakar amesema PBZ inaendelea kuwa mshirika muhimu kwa Serikali kwani inachangia maendeleo ikiwemo kukuza biashara, ajira na uwezeshaji wananchi.
Amesema wakati wakiadhimisha kilele hicho ni matarajio yao kuiona PBZ inakuwa kinara wa ubunifu kwa kupanua huduma za teknolojia, kutanua wigo na kuongeza kasi ya utendaji kazi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PBZ, Dk Juma Hassan Reli amesema wananchi wa Tanzania wanaiona benki hiyo kuwa yao kama lilivyo jina lake na imekuwa na mchango mkubwa kwao.