Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwinyi ataja mgongano wa kimaslahi Simai kujiuzulu

Muktasari:

  • Januari 25, 2024 aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed Said alitangaza kuwa amejiuluzu na kwamba amemuandikia barua Rais Dk Hussein Mwinyi kuhusu uamuzi huo

Unguja. Siku chache baada ya aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed Said kujiuzulu, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametoa angalizo wanaofanya hivyo kuwa wakweli na wataje sababu za kujiuzulu badala ya kuudanganya umma.

Amesema kujiuzulu ni njia ya kuwajibika, hivyo iwapo kuna waziri anaona kuna sehemu hakubaliani na Serikali katika uamuzi ni vyema akasema na ataheshimika zaidi akisema, “Mawaziri tukilazimika kujiuzulu au kuwajibika, tuwajibike.”

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Februari mosi, 2024 wakati akiwaapisha mawaziri watatu na manaibu waziri watatu katika viwanja vya Ikulu, Zanzibar aliowateua Januari 26, 2024 siku moja baada ya Simai kujiuzulu.

Rais Mwinyi amesema kuna jambo la kukumbushana “wakati unawajibika, lazima uwe mkweli na ukweli ninaousema hapa lazima kama kuna mgongano wa maslahi uutangaze.”

Katika kulifafanua jambo hilo ametoa mfano; “kama mtu una imani ya dini, halafu Serikali ikasema hatutaki kusikia adhana inatupigia kelele kwa hiyo vyombo visitumike kutangaza na wewe una imani ya dini, unawajibu kujiuzulu kwa sababu utesema Serikali imefanya jambo hili kutokana na imani yangu.”

Amesema ikiwa kuna sababu yoyote inayomfanya mtu ajiuzulu anawajibika kuwa wazi na kusema “kama tumezuia kitu na wewe una biashara hiyo tangaza, sema ukweli, sema hapa kuna mgongano wa maslahi mimi ni muagizaji wa kitu fulani na nyie mmezuia, kwa hiyo tuwe wakweli.

“Sasa ukitoka na ukaaminisha watu mambo tofauti yasiyo ya kweli, unapaswa uwajibike huku ukiwaambia watu kilichokufanya uwajibike,” amesema.

Amesema ameamua kusema hayo kwa sababu uwaziri si nafasi ya kukaa maisha, akisema ama mtu ataondolewa au kujiuzulu.

“Lazima tujue yanaweza yakatokea matatizo na wala si yako yakakufanya uwajibike na pale ambapo hukubaliani na Serikali sema tutakuheshimu zaidi, kama una baa watu wamezuia pombe, sema mimi nina baa inaingiliana na maslahi yangu, kuwa muwazi,” amesisitiza.

Katika taarifa yake ya kujiuzulu, Simai bila kufafanua sababu, alisema ni kutokana na mazingira magumu, lakini siku mbili kabla ya kuchukua uamzui huo alikutana na wadau wa utalii akazungumzia changamoto za uhaba wa vileo akilalamikia bodi ya vileo kubadili kampuni za kuingiza vinywaji hivyo na kuweka nyingine mpya.

Katika hotuba yake ya takribani dakika 14 na sekunde 39, Rais Mwinyi ametaja mazingira mawili ambayo yanaweza kumfanya waziri ajiuzulu, huku akiwataka watambue nafasi hizo si za kudumu ni za muda, hivyo wakati wowote mtu anaweza kuondoka au kuondolewa.

“Kunaweza kukawa na scenario (mazingira) mbili za waziri kujiuzulu, ya kwanza unaweza kuwa katika sekta unayosimamia kumetokea tatizo, na wewe kama waziri unawajibika kwa changamoto ile si lazima uwe umesababisha wewe, kwa sababu wewe ndio msimamizi wa sekta,” alisema huku akirejea ajali ya meli ya Spice.

Dk Mwinyi ameongeza: Sio utaratibu, utaratibu unatakiwa umwambie aliyekuteua akubali ndio utangaze.”

Sababu ya pili aliyoitaja inayoweza kumfanya waziri ajiuzulu ni pale Serikali inapoamua jambo, lakini waziri hakubaliani nalo.

“Wewe kama mwenye sekta, tumeamua jambo tunalileta kwenye sekta, tunasema uamuzi ni huu, wewe ukasema hukubaliani na uamuzi huo, unatoka unajiuzulu kwa sababu hukubaliani na uamuzi uliotolewa na Serikali,” amesema.

Kutokana na hilo amefichua siri alivyotaka kujiuzulu wakati akiwa Waziri wa Ulinzi baada ya kulipuka mabomu katika kambi ya Jeshi Gongo la Mboto, lakini Rais wa wakati huo Jakaya Kikwete akakataa.

Katika hafla hiyo, walioapishwa ni Mudrik Ramadhan Soraga kuwa Waziri wa Utalii, Ali Suleiman Ameir, Ofisi ya Rais Ikulu na Shaaban Ali Othman, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi.

Juma Makungu Juma ameapishwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Salha Mohamed Mwinjuma kuwa Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, huku Zawadi Amour Nassor akiapishwa kuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini.