Dk Mwinyi kuboresha masilahi ya walimu Zanzibar

Muktasari:
- Mazingira magumu ya kufanyia kazi ni kilio cha muda mrefu cha wa watumishi hao kiasi cha kuathiri utendaji kazi.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameahidi kuboresha mazingira na masilahi ya walimu visiwani humo, huku akisema kwa muda mrefu walimu wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu ambayo yalikuwa na changamoto kwao.
Ametoa kauli hiyo katika ufunguzi wa Skuli ya Mwembeladu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Dk Mwinyi amesema juhudi za walimu ndizo zinazoleta matokeo chanya kwa wanafunzi hivyo ni wakati mwafaka kwa wao kuona matunda ya uvumilivu wao.
"Walimu mmenifurahisha sana, mnafanyakazi nzuri kwani muda mrefu mmekuwa mkifanya kazi katika mazingira magumu, wakati umefika wakukupeni mazingira bora ikiwa ni pamoja na kuwa na watoto wachache darasani na kuwawezesha kufundisha bidii na umakini," amesema Dk Mwinyi.
Amesema mafanikio ambayo yamepatikana yametokana na juhudi zao kwani namba haziwezi kusema uongo tofauti na wanasiasa wanaoweza kupiga maneno ndiyo maana watu wanaambiwa wasisikilize maneno badala yake, wasikilize namba.
Amesema juhudi za walimu zimefanikisha kuongeza ufaulu kwa wanafunzi hivyo anaangalia maslahi yao kwa lengo la kuyaboresha zaidi.
Sambamba na hayo amesema alikuwa anajiuliza maswali juu ya uamuzi wa kujenga skuli hiyo kama ni sahihi au amekosea lakini jibu lake ni sahihi kwa uamuzi huo kwa sababu yana faida kwa jamii.
Amesema, yapo maeneo mengi mazuri kwa ajili ya uwekezaji ila majengo ya shule ni chakavu na kwamba hayaridhishi hivyo ni bora kujenga shule za kisasa kwa lengo la kutengeneza mazingira rafiki kwa wanafunzi.
"Tutaendelea kufanya maamuzi sahihi yenye faida kwa nchi yetu, kwa hivyo wale wanaotusema na kutupiga vijembe, ninasema hadharani wala usingizi sikosi, nitaendelea kuyajenga maghorofa haya ya Skuli mpaka watoto wote wakae katika mazingira mazuri," amesema Dk Mwinyi.
Ameeleza kuwa anachotaka ni kuona walimu wanafundisha wakiwa katika madarasa ambayo wanafunzi wake hawazidi 45 na kwamba hapo ndipo msingi wa elimu unapoanzia kwa sababu huwezi kufundisha watoto 200 katika darasa moja.
Amesema Waziri wa Elimu na Mafunzo Amali inahitaji madarasa 5,000 ambapo kwa sasa madarasa 3,000 yameishajengwa na ndani ya kipindi kifupi kijacho, watakamilisha idadi ya madarasa yanayotakiwa.
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo Amali Zanzibar, Lela Mohammed Mussa amesema jumla ya wanafunzi 6,662 wa darasa saba wamefaulu masomo yao katika mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo waliofaulu wanafunzi 2197.
Kwa mujibu wa Lela, jengo hilo lina jumla ya madarasa 39, vyoo 54 na litachukua wanafunzi 1,755, pia litatoa wataalamu wenye sifa na viwango vya juu.