Idadi ndogo wajitokeza kujiandikisha Micheweni

Maofisa wa uandikishaji wakiendelea kusajili wapiga kura wapya katika kituo cha Micheweni Shehia ya Majenzi mkoa wa kaskazini Pemba. Picha na Muhammed Khamis.

Muktasari:

  • Wamesema idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kujiandikisha Micheweni inatokana na watu wengi kutokuwepo eneo hilo huku baadhi yao wakihofia kupoteza muda.
Pemba. Wakati hatua ya kwanza uandikishaji wapiga kura wapya ikifikia tamati leo hii katika wilaya ya micheweni mkoa wa Kaskazini  Pemba kumekua mwitikio mdogo wa wananchi wanaojitokeza.

 Mwananchi Digital imefika katika vituo vyote vya Wilaya ya Micheweni na kushuhudia maofisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wakisubiri waandikishaji kwa muda mrefu.

Mwananchi Digital imezungumza na mawakala wa vyama tofauti na kusema idadi ndogo ya wananchi inatokana na watu wengi kutokuwepo maeneo yao.

Hamad Bakari wakala wa ADC anasema vijana wengi wa Wilaya ya Micheweni kwa sasa hawapo wengi wao wapo masomoni.

"Micheweni ya sasa siyo hile ya zamani hivi sasa vijana wengi wanasoma na wengi wao wapo vyuoni ndio maana hawapo sasa hapa," amesema.

Maimuna Zuberi ni miongoni mwa wananchi waliofika kituoni hapo kujiandikisha.

Anasema ameamua kwenda kujiandikisha kutekeleza haki yake ya kikatiba na hataki kuwa kama wengine.

Amesema licha ya yeye kujitokeza lakini katika shehia yake wapo wengi ambao wamegoma wakidai wamechoka na hawapo tayari kupoteza muda.

"Yalitokeao 2020 katika Uchaguzi Mkuu nadhani ndiyo yanayofanya wengi wasijitoze wakiamini kuwa hakuna mabadiliko yatakayotokea.

Akizungumza na Mwananchi Digital Mkurugenzi wa uchaguzi kutoka (ZEC), Faina Idarous amesema uandikishahi huo utakuaja tena kwa awamu nyengine kabla ya Uchaguzi Mkuu 2020 na kuwataka wale wote watakaokosa awamu ya mwanzo kujitokeza tena mara nyengine.