Mfahamu Rais Aboud Jumbe wa Zanzibar-2

Katika toleo lililopita tuliona jinsi muungano wa vyama vya TANU na ASP ulivyoanza na nafasi ya Jumbe katika kuhakikisha hilo lengo ni kuvifanya kuwa na nguvu na kusimamia maslahi ya wananchi. Endelea

Muungano wa vyama hivyo ulifuatia baada ya muungano wa Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika wa mwaka 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni muungano wenye Serikali mbili, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Pia, Jumbe ndiye aliwezesha kuimarika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mwanasheria wake mkuu wa kwanza alikuwa Damian Lubuva aliyepewa na Mwalimu Nyerere na pia (Jumbe) aliishi Tanzania Bara hadi kifo chake, japokuwa alizikwa Unguja.

Kwa sababu iliyotolewa na Mwalimu Nyerere ambaye ndiye alishirikiana na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kuunda Muungano huo, ni kwamba muungano wa Serikali moja ungetafsiriwa ni kuimeza Zanzibar ambayo kwa wakati huo ilikuwa ni nchi ndogo yenye idadi ya watu takriban 200,000 tu.

Baada Muungano wa Serikali, Mwalimu Nyerere aliunganisha nguvu ya kisiasa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi kwa kuunganisha vyama vya TANU na ASP mwaka 1977 na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Haki ya kupiga kura Zanzibar

Leo tutazungumzia namna muungano wa Serikali na muungano wa vyama vya ASP na TANU ulivyowezesha kwa mara ya kwanza kuwapa wananchi wa Zanzibar mamlaka ya kuchagua Rais wao na wawakilishi kwenye majimbo yao.

Ni Jumbe ndiyo aliwezesha Wazanzibari kutumia haki yao ya kupiga kura tangu Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Uchaguzi wa kwanza wa Zanzibar ulikuwa Julai 1957 uliohusisha nafasi ya wajumbe wa Baraza la kutunga Sheria ulioshirikisha vyama vya ASP na Zanzibar Nationalist Party (ZNP).

Baada ya uchaguzi huo kuna uchaguzi uliofanyika Janurari 17, 1961, Juni Mosi 1961 na Julai 8-11, 1963. Kwa mujibu wa kitabu cha Elections in Africa: A Data Handbook (Ukurasa wa 872), baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume alitangaza kuwa “hakutakuwa na uchaguzi Zanzibar kwa miaka 60 ijayo.

Katika ukurasa wa 10,576 wa jarida la Congregassional Record: Proceedings and Debates of the…, Volume 115, Part 8, la Aprili 28, 1969, Sheikh Abeid Karume amekaririwa akisema “…Hakuna uchaguzi utafanyika Zanzibar kwa angalau miaka 60 ijayo. Uchaguzi ni chombo cha mabeberu cha kuwakandamiza wananchi.”

Maneno hayo yamekaririwa pia na kitabu cha Tanzania: The Story of Julius Nyerere Through the Pages of Drums cha waandishi Mohamed Amin, Annies Smyth na Adam Seftel.

Mwandishi William Edgett Smith katika ukurasa wa 181 wa kitabu chake We Must Run While they Work: A Portrait of African’s Julius Nyerere, ameandika kuwa Karume alitamka maneno hayo mwaka 1968 alipohojiwa na gazeti la Tanzania The Standard (Sasa Daily News).


Wazanzibari kuanza kupiga kura

Ni Jumbe wakati wa utawala wake ndiye aliyeasisi utaratibu wa kumpata Rais wa Zanzibar kwa njia ya kupigiwa kura na mchakato wake ulifanyika kupitia Kamati Maalumu ya Kamati Kuu ya CCM.

Na hii ni baada ya Jumbe kuimarisha Muungano ambapo kwa mara ya kwanza Wazanzibari waliwachagua Rais wa Zanzibar, Rais wa Muungano na wabunge baada ya kuanzishwa kwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kabla ya hapo kulikuwa na Baraza la Mapinduzi ndio lilikuwa likachagua viongozi.

Uchaguzi huo ni matokeo ya Jumbe kutia saini Katiba ya kwanza ya Zanzibar mwaka 1979 na mwaka 1980 wananchi wa Zanzibar walipata haki ya kuchagua viongozi wao.

Katiba mpya ya Zanzibar ilianzisha Baraza la Wawakilishi lililoshirikiana na Baraza la Mapinduzi linaundwa na Rais wa Zanzibar.


Muundo wa Baraza la Mapinduzi

Baraza la Mapinduzi linaundwa na Rais wa Zanzibar, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza, Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais, mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na wajumbe wengine walioteuliwa na Rais wa Zanzibar.

Pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar atahudhuria mikutano yote ya Baraza la Mapinduzi na atakuwa na haki zote za Mjumbe wa Baraza hilo.

Kazi za Baraza la Mapinduzi zitakuwa ni kumsaidia na kumshauri Rais katika masuala ya SMZ, kuratibu shughuli za Rais, Makamo wa Kwanza wa Rais na Makamo wa Pili wa Rais na wizara za SMZ katika utekelezaji wa majukumu yao


Baraza la Wawakilishi

Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar ni Bunge la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Tanzania inayojitawala katika mambo mengi ya ndani. Baraza la Wawakilishi lilianzishwa mwaka 1980. Kabla ya mwaka huo, Baraza la Mapinduzi lilikuwa na shughuli za Serikali na pia Bunge kwa muda wa miaka 16 baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Inaendelea kesho Jumatano Novemba 29, 2023