Mfahamu Rais Aboud Jumbe wa Zanzibar-1

Aboud Jumbe Mwinyi ni Rais wa pili wa Serikali ya Zanzibar baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliyouondoa madarakani utawala wa Sultani na Serikali yake.

Jumbe aliyefariki dunia Agosti 14, 2016 akiwa na umri wa miaka 96, ndiye Rais wa kwanza na pekee wa Zanzibar aliyeamua kuishi eneo la Mjimwema, Kigamboni jijini Dar es Salaam huku akifanya kazi ikulu ya Zanzibar. Alikuwa akisafiri kwa ndege kila siku asubuhi kwenda ofisini Unguja na kurejea Dar es Salaam jioni.

Kiongozi huyo aliongoza Zanzibar kwa miaka 14, kuanzia Aprili 11, 1972 akimrithi Rais wa kwanza wa visiwa hivyo, Abeid Amani Karume, aliyeuawa Aprili 7, 1972. Aliongoza hadi Januari 30, 1984, alipolazimika kujiuzulu.

Jumbe alizaliwa mwaka 1920 huko Mpitimbi mkoani Ruvuma, Tanganyika na wazazi wake walihamia Makunduchi, Unguja mwaka 1925, wakati Jumbe akiwa na miaka miaka mitano.

Kuna wakati Jumbe kwenye ziara za kiserikali mikoa ya kusini mwa Tanzania akiwa makamu wa Rais wa Serikali ya Muungano, alinukuliwa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma akisema alikuwa akitafuta asili yake wilayani humo.

Inaelezwa Jumbe alisoma shule Zanzibar mjini kuanzia mwaka 1930 hadi 1942. Alisoma diploma ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, nchini Uganda kuanzia mwaka 1943 hadi 1945.

Kuanzia mwaka 1946 hadi 1960, Jumbe ambaye tayari alikuwa ameoa na ana watoto, alifundisha katika shule ya wavulana ya Zanzibar kuanzia mwaka 1946 hadi mwaka 1960. Baadaye alijizulu ualimu na kuendelea na siasa alizokuwa ameanza hawapo awali.

Mwaka 1953 Jumbe alijiunga na chama cha Zanzibar National Union na mwaka 1960 alihamia Chama cha Afro-Shirazi (ASP) na mwaka 1961 alichaguliwa mbunge na hapo ndipo aliingia kwenye siasa za muda wote.

Mwaka huohuo wa 1961 baada ya kuchaguliwa mbunge kupitia chama cha ASP, aliteuliwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na alihudhuria mazungumzo ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanyika London nchini Uingereza kuanzia mwaka 1962 na 1963.

Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwenye Serikali ya Abeid Amani Karume. Pia, alishika nyadhifa zingine kama Waziri wa Afya na Bima kwa Jamii.

Pia, baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na kuzaliwa Tanzania Aprili 26, 1964, Jumbe aliteuliwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akishughulikia mambo ya Muungano, nafasi aliyoishika kwa miaka minane.

Waangalizi wa kidiplomasia walimuona Jumbe kama kiongozi mwenye msimamo wa kawaida kulinganisha na mtangulizi wake Abeid Amani Karume, kutokana na jitihada zake za kutafuta ushirikiano na watu wa kada zote wa Kiafrika, Waarabu na Waasia.


Nafasi ya urais

Jumbe aliteuliwa na Baraza la Mapinduzi kushika wadhifa wa Rais Aprili 7, 1972 baada ya kuuawa kwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Kuteuliwa kwa Jumbe kuwa Rais wa Zanzibar kulichangiwa zaidi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Tanu kwa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama na Serikali.

Mwalimu aliwaeleza viongozi wa Tanu na ASP kwamba pamoja na kuuawa kwa Karume, mwasisi mwenza wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Muungano huo lazima uendelezwe bila kuyumba na mtu pekee aliyefaa, kwa maoni ya Nyerere, ni Aboud Jumbe Mwinyi, kwa sababu kuu tatu.

Alizieleza sababu hizo kuwa ni pamoja na usomi wake pia ni mwanasiasa mkongwe mwenye kuzielewa vyema siasa na migongano ya jamii ya Kizanzibari.

Mwalimu Nyerere aliendelea kumwagia sifa Jumbe kuwa ni mtu ambaye hakuwa na majungu wala makundi yenye kuhasimiana na wadhifa wake wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Mambo ya Muungano) kwa muda mrefu, ilikuwa ni sifa ya ziada iliyompa uzoefu na uwezo wa kuendeleza na kudumisha Muungano.

Hoja ya Mwalimu Nyerere ilipita na Jumbe akawa Rais wa pili wa Zanzibar. Akiwa madarakani, ndipo Mwalimu Nyerere akaleta wazo kwamba Tanzania iwe nchi ya chama kimoja cha siasa, ingawa ndani yake kuna vyama viwili vya Tanu na ASP.

Oktoba 1976, maridhiano yalifikiwa ya kuunda chama kipya, Chama cha Mapinduzi’ (CCM), kilichozaliwa Februari 5, 1977, tarehe na mwezi sawa na ilipozaliwa ASP mwaka 1957.

Jitihada za Jumbe kuimarisha Muungano zilianzia hapo kwa kukubali kuunganisha Tanu na ASP na kuzaliwa kwa CCM.

Jumbe ndiye alifanikisha CCM izaliwe tarehe na mwezi sawa ilipoanzishwa ASP -- Februari 5, 1957 na alifanikisha kubakiza neno ‘Mapinduzi’ yaliyoleta uhuru wa nchi hiyo Januari 12, 1964, liwe sehemu ya jina la chama kipya -- Chama cha Mapinduzi bila kuwa na tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza.


Kinara wa muungano

Kama tulivyoona, CCM ilizaliwa Februari 5, 1977 kutokana na kuvunjwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (Tanu Afro-Shirazi Party (ASP)

Tendo hilo la kihistoria lilikuwa la kuendeleza utamaduni uliokuwa umeanza huko nyuma wa kuunganisha nguvu kwa lengo la kujiimarisha katika mapambano.

Kwa mfano, ASP kwa upande wa Zanzibar ilitokana na kuungana kwa vyama vya African Association (AA) na Shirazi Association (SA), tendo ambalo liliunganisha nguvu za wanyonge katika mapambano ya kuundoa usultani na utawala wa kikoloni wa Kiingereza.

Kwa upande wa Tanzania Bara, TANU ilitokana na kujibadilisha kwa Tanganyika African Association (TAA) kutoka jumuiya ya kutetea masilahi ya kijamii na kuwa chama cha siasa.

Kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika Desemba 9, 1961 na ule wa Zanzibar kupitia Mapinduzi Januari 12, 1964, kulifanya Tanu na ASP viwe vimekamilisha jukumu la ukombozi wa nchi hizi kutoka makucha ya ukoloni na usultani.

Hata hivyo, vyama vya siasa hivi viliendelea kukabiliwa na majukumu ya kuendeleza mapambano ya ukombozi katika Afrika na kote duniani; kujenga Tanganyika na Zanzibar huru kiuchumi na kijamii na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Katika mazingira ya ubeberu duniani wakati huo na hali ya unyonge wa mataifa haya machanga, yakielewa kuwa ‘umoja ni nguvu’, Tanganyika na Zanzibar zilibaini umuhimu wa muungano, hivyo ziliamua kuungana Aprili 26, 1964.

Muungano huo ndio uliowezesha kuzaliwa kwa Tanzania.

Chini ya Muungano huo na iliendelea kuwa na vyama vya siasa viwili, yaani Tanu na ASP katika mazingira ya chama kimoja cha siasa.

Vyama hivi vilitambua fika kwamba vinahitaji chombo madhubuti cha uongozi katika kutekeleza majukumu yake ya ukombozi kwa ukamilifu hivyo uamuzi ulifanywa rasmi wa kuvunja Tanu na ASP na kuundwa kwa CCM Februari 5, 1977.

Muungano wa Tanu na ASP chini ya Nyerere na Jumbe ndio uliowezesha CCM kuwa chama chenye nguvu, imara na madhubuti.


Inaendelea