Kiama wasiofuata sheria ya habari chaja

Katibu mtendaji tume ya utangazaji Zanzibar Suleiman Abdulla akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja. Picha na Muhammed Khamis
Muktasari:
- Tume ya Utangazaji Zanzibar imetoa onyo kwa wasiofuata sharia za utangazaji na kuwataka kusajili vituo vya habari ili iwe njia itakayoweza kuwanusuru na mkono wa sheria.
Unguja. Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Suleiman Abdulla Salim, amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kufuata sheria sambamba na kufanya kazi zao kwa uadilifu na umakini, hivyo kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.
Ameyasema hayo leo Novemba 15, 2023 wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja.
Ukaguzi uliofanywa hivi karibuni na tume hiyo umebaini wapo baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari vya utangazaji kuwa wanafanya kazi zao bila ya kufuata sheria na miongozo jambo hilo ni kinyume na matakwa ya Serikali.
“Katika tathimini yetu fupi iliyofanywa hivi karibuni, tumebaini kuwepo kwa baadhi ya vituo vya utangazaji hasa vya maudhui ya mtandaoni (online tv), zimeanzishwa bila ya kufuata utaratibu hivyo Tume inatoa muda wa wiki mbili kwa wale wenye hizo online waje kuzirasimisha ili wawe salama katika kazi zao,” ameonya.
Amesema kuwa mujibu wa sheria ya tume ya utangazaji namba saba ya mwaka 1997, kifungu cha 11 kinapiga marufuku kwa mtu yeyote kurusha au kwa namna yoyote kuendesha huduma za utangazaji pasi na kuwa na leseni inayotambulika.
Amefahamisha kuwa tume imepewa mamlaka ya kuhakikisha wanasajili watoa huduma za utangazaji Zanzibar ikiwemo Online, Televisheni na Radio hivyo haitakuwa na muhali kwa kituo chochote cha utangazaji kitakachobainika kuwa na kosa hilo.
Aidha amesisitiza kuwa tume ya utangazaji Zanzibar inaendelea kufuatalia pia matangazo ya vituo vya utangazaji kwa kutumia mitambo ya kitaalamu kwa ajili ya kuhakikisha habari zinazotolewa zinakuwa ni za ukweli na kulinda maslahi ya taifa na hazimuumizi mwengine endapo zitakapotoka sambamba na kuhakikisha usalama wa nchi unabaki ulivyo na utamaduni wa nchi unalindwa.
Mrajisi wa Tume hiyo, Mohamed Said Mohamed, amesema watahakikisha wanaendelea kushirkiana na wadau wa sekta ya utangazaji ili kuona wanafanya kazi kwa mujibu wa maombi yao wanayoyafikisha katika Tume kwa mujibu wa sheria na kanuni na miongozo inayoruhusu shughuli za utangazaji Zanzibar.