Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkakati wasukwa kuwawezesha wanafunzi kuongeza ufaulu

New Content Item (1)

Baadhi ya wanafunzi wanaotoka katika familia duni wakivaa viatu baada ya kukabidhiwa katika uzinduzi wa programu ya kuimarisha elimu jimbo la Chaani Mkoa wa Kaskazini, Unguja

Muktasari:

  • Mpango huo ambao unahusisha wanafunzi walio kwenye madarasa ya mitihani ya kitaifa kwa kuwapa vifaa na vyakula kwa ajili ya kambi za masomo.

Unguja. Ili kuinua kiwango cha elimu, imezinduliwa programu maalumu itakayowawezesha wanafunzi wa msingi na sekondari kufaulu mitihani yao ya kitaifa.

Programu hiyo inalenga kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bila kujali uwezo wa kipato wa mzazi, hali ya ulemavu na umbali wa kufuata elimu katika maeneo tofauti jimbo la Chaani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Wakizungumza wakati wa kuzindua programu hiyo iliyoandaliwa na mbunge wa jimbo hilo Juni 30, 2026, Ayoub Mohmed Mahamoud na mwakilishi wajimbo hilo, Juma Usonge Hamad kwa kushirikiana na taasisi ya Mimi na Wewe Foundation, wazazi na wanafunzi katika maeneo hayo wameeleza faraja yao namna inavyoweza kubadilisha.

Ashura Jabir Ali, mwanafunzi sekondari ya Kinyasini amesema kutokana na uwezo mdogo wa familia wanafunzi walikuwa wakishindwa kuhudhuria masomo ya ziada hivyo kuwafanya waendelee kushindwa kufia malengo yao.

Nao baadhi ya wazazi akiwemo Sultani Shekhe Haji amesema kutokana na umaskini wa wananchi katika ukanda huo, ilikuwa vigumu kuwasimamia watoto kupata elimu bora.

“Unakuta una watoto watatu, sasa kuna fedha za masomo ya ziada kila mmoja Sh15,000 uwezo wa kulipa hauna maana hata chakula nyumbani hakuna, kwa hiyo ilikuwa changamoto,” amesema.

Akizungumza kuhusu programu hiyo, Ayoub ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amesema ni miongoni mwa vipaumbele vitatu wanavyotaka kuvitekeleza ndani ya kipindi cha miaka mitano lakini elimu ikiwa ni namba moja.

Sehemu ya vifaa vikiwemo vyakula vilivyokabidhiwa kwa shule katika jimbo la Chaani ikiwa ni mpango wa kuinua kiwango cha Mkoa wa Kaskazini, Unguja

Amesema katika matokeo ya ufaulu kwa shule za msingi ni asilimia 30 kwa shule tisa zilizopo katika jimbo hilo na asilimia 25 kwa sekondari tatu, hivyo lengo lao ni matokeo yajayo kwa shule za msingi yawe angalau asilimia 60 na sekondari asilimia 55.

“Programu hii itatumia Sh425 milioni kwa kuanzia kwa kipindi cha miaka miwili, lakini leo hii tunakabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh187 milioni.”

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na tani 25 za chakula, ukiwemo mchele, maharage, sukari na mafuta na magodoro kwa ajili ya wanafunzi wanaokwenda kujisomea makambini.

Vingine vimekabidhiwa viti mwendo 10 kwa watoto wenye mahitaji maalumu na zaidi ya wanafunzi 1,000 wakipewa viatu vya shule wakiwemo watoto yatima na wengine ambao wazazi wao hawajiwezi kabisa kimaisha huku zikitolewa taulo za kike kwa zaidi ya wanafunzi 600.

Katika hatua nyingine amezikabidhi kamati za shule Sh10 milioni ili wazirejeshe kwa wazazi ambao tayari walikuwa wamekwishachangia kwa ajili ya masomo ya ziada ya watoto wao.

Naye Mwakilishi wa jimbo hilo, Usonge amesema wanatekeleza waliyoahidi wakati wa kampeni hivyo wanatarajia kuona ufaulu unaongezeka na asiwepo mtoto hata mmoja kukosa elimu kisa kashindwa kupata mahitaji muhimu.

Naye Mkuu wa Sekondari Kinyasini, Hamza Ali Hamdu amesema tangu aanze kazi ya ualimu miaka 30 sasa, hajawahi kuona mipango mizuri ya kuinua elimu katika eneo hilo kama inayofanyika sasa.

“Bila elimu hakuna maisha, bila kuwekeza kwenye elimu hakuna liwalo, hakika tunaweza kuona mabadiliko makubwa, ila niwasihi wazazi kutoa ushirikiano kwani kuna wakati wanalalamikia elimu ila ukiwaita shuleni hawaji,” amesema.

Kwa upande wake Katibu wa Mimi na Wewe Foundation, Zuberi Mwinchumu amesema lengo ni kuboresha matokeo kwa kuendesha kambi za masomo kwani katika utafiti wao walibaini kuna changamoto kubwa katika shule hizo.

“Tunawajengea vijana mazingira mazuri ya kusoma, nidhamu, kujiamini na kuwapa lishe bora ili mwanafunzi asiwe na mawazo mengine ya njaa badala yake afikirie masomo pekee,” amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali ambaye alikuwa mgeni rasmi, Lela Mohamed Mussa amesema Serikali inaweka kipaumbele katika sekta ya elimu na kuongeza bajeti yake kila mwaka ambapo kwa mwaka huu imefikia Sh1.1 trilioni.

“Watoto someni, wazazi wasimamieni watoto wenu, na walimu hakikisheni mnatimiza wajibu wenu kufundisha kwa mujibu wa ratiba na sio msubiri vipindi vya ziada ndio mkimbilie huko kwa sababu kuna posho, hakikisha unafundisha darasani kisha yale masomo ya jioni yawe ni kufanya marudio,” amesema.