Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi upimaji ardhi Zanzibar kumaliza migogoro, kuongeza imani ya wawekezaji

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mradi wa mfumo wa usimamizi na usajili wa ardhi Zanzibar (Laris) katika uwanja wa ndege wa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Mradi huo wa Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Ardhi Zanzibar (Laris) utatumia ndege maalumu kukusanya na kuchakata taarifa za ardhi katika maeneo tisa, huku vipande vya ardhi 25,000 vikitarajiwa kupimwa.

Unguja. Wakati Zanzibar ikizindua mradi wa upimaji ardhi kwa njia ya anga, mradi huo umeelezwa kuwa mwarobaini wa migogoro ya ardhi katika visiwa hivyo na kuongeza imani kwa wawekezaji.

Pia, unatarajiwa kuimarisha mazingira ya biashara, kuongeza mapato ya Serikali, kuwezesha wananchi kupata mikopo kwa kutumia hati za haki ya matumizi ya ardhi kama dhamana na kusaidia ujenzi wa miji endelevu ya kisasa pamoja na makazi bora.

Mradi huo wa Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Ardhi Zanzibar (Laris) utatumia ndege maalumu kukusanya na kuchakata taarifa za ardhi katika maeneo tisa, huku vipande vya ardhi 25,000 vikitarajiwa kupimwa.

Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo leo, Julai 27, 2026, katika Uwanja wa Ndege wa Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, Rais Dk Hussein Mwinyi amesema wameweka msingi wa mageuzi ya utawala na usimamizi wa ardhi.

“Kupitia mradi huu tunatarajia kuboresha kwa kiwango kikubwa huduma za upangaji wa matumizi ya ardhi, upimaji, utambuzi na usajili wa ardhi kwa njia ya kidijitali,” amesema Dk Mwinyi.

Mradi huo utakaogharimu Euro milioni 37.4 (sawa na Sh115 bilioni), utahusisha upigaji picha za anga na uandaaji wa ramani za msingi, ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Taarifa za Ardhi na ujenzi wa vituo vya utoaji huduma Unguja na Pemba.

Pia, utaandaa mipango ya matumizi ya ardhi, ubadilishaji wa kumbukumbu za ramani kutoka mfumo wa kawaida kwenda kidijitali, ujenzi wa mfumo wa kielektroniki wa kuhifadhi na kusimamia taarifa za ardhi, pamoja na kufanya utambuzi wa maeneo.

Amesema mfumo wa ukusanyaji, uhifadhi na matumizi ya taarifa za ardhi umekuwa ukitegemea mbinu za zamani ambazo husababisha ucheleweshaji wa huduma, upungufu wa taarifa na kuzalisha migogoro ya ardhi inayohusisha umiliki, mipaka na matumizi ya ardhi.

Dk Mwinyi amesema huduma nyingi za ardhi zimeendelea kutolewa katika ofisi chache za makao makuu mjini, hali inayowalazimu wananchi kutumia muda na gharama kubwa kuzifuata huduma hizo.

Kutokana na kukabiliwa na changamoto hizo, amesema baadhi ya wananchi hufanya uamuzi usio rasmi ambao huongeza migogoro na matumizi holela ya ardhi.

Hivyo, Serikali kwa makusudi imeamua kuchukua hatua kadhaa kuimarisha utawala na usimamizi wa ardhi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha sera na sheria za ardhi na kuanzisha mfumo huo ambao unakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto hizo.

Rais Mwinyi, mfumo walionao kwa sasa si rahisi kupata kwa wakati taarifa sahihi kuhusu ukubwa wa ardhi iliyotengwa kwa makazi, kilimo, viwanda, uwekezaji au maeneo ya hifadhi kwa kukusanya taarifa kwa njia za kawaida.

Ameishukuru Serikali ya Ufaransa kwa kuiwezesha Kampuni ya IGNFI kusimamia utekelezaji wa mradi huu, pamoja na Benki ya Uwekezaji ya Ufaransa (BPI) na Benki ya CRDB ya Tanzania kwa kufadhili mradi huo hadi utakapokamilika.

Hata hivyo, amesema teknolojia pekee haiwezi kuleta mabadiliko bila ya matumizi sahihi na dhamira thabiti ya kuitumikia jamii na nchi kwa ujumla.

Akitoa taarifa za kitaalamu, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo Bakari, amesema kupitia mradi huo wa miaka miwili wanatarajia kupima vipande vya ardhi 25,000.

Amesema mkataba wa Laris ulitiwa saini Agosti 7, 2024, baina ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Kampuni ya IGNFI kutoka Ufaransa.

Hata hivyo, amesema mkataba huo ulichelewa kutekelezwa kutokana na kusubiri masharti ya mkataba wa kifedha kukamilika, ambapo ulisainiwa Oktoba 27, 2025, kati ya Wizara ya Fedha na Benki ya CRDB, na CRDB na Benki ya Uwekezaji ya Ufaransa (BPI).

Amesema gharama za mradi huo ni Euro milioni 37.4 (Sh115 bilioni) bila VAT, na Euro milioni 43.117 (Sh130 bilioni) ikijumuisha VAT. Muda wa utekelezaji wa mradi huu ni miezi 24, na miezi 24 mingine itatumika kwa matengenezo na uendelezaji wa mfumo wa ardhi utakaotengenezwa.

“Ndege itakayotumika itatumia miezi mitatu kupiga picha za anga kwa saa 36 angani, hii ni kutegemeana na vibali vya anga,” amesema.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Gallos Nyimbo, amesema wameshirikishwa vya kutosha na wananchi wapo tayari kutekeleza mradi huo, kwani unakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto za ardhi Zanzibar.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali, amesema huo ni ubunifu utakaoikomboa Zanzibar katika mpangilio na upimaji ardhi.

“Mradi huu una faida nyingi, moja ni kuondokana na migogoro, kutakuwa na matumizi yaliyopangwa na wawekezaji watakuwa na imani na sisi, maana nao wakati mwingine wanaingia kwenye migogoro ya ardhi,” amesema.

Amesema kwa sasa ardhi ya Zanzibar imepimwa kwa asilimia 20 tu.