Mwinyi aendeleza juhudi za kukuza utalii Zanzibar

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi (Kulia) akisalimiana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu alipotembelea banda la maonyesho la benki hiyo kwenye mkutano wa pili wa wadau wa sekta ya utalii Zanzibar (Z -Summit) unaofanyika mjini Unguja.


Muktasari:

  • Inaelezwa kuwa jitihada zinazofanywa na Serikali za kuboresha sekta ya utalii Zanzibar, zinapaswa kuzaa matunda ili wananchi wafaidike kiuchumi.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amethibitisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, umeme, maji na viwanja vya ndege ili kuandaa mazingira yanayolenga kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii visiwani humo.

Aidha, Rais Mwinyi ametoa wito kwa wananchi  visiwani humo kuchangamkia fursa mbalimbali za utalii kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali,  kukuza na kuboresha sekta hiyo.

Akizungumza leo Jumatano Februari 21,2024 katika Mkutano wa pili wa wadau wa sekta ya utalii Zanzibar (Z -Summit) unaoendelea visiwani hapa, Rais Mwinyi amesema jitihada zinazofanywa na Serikali za kuboresha sekta hiyo zinapaswa kuzaa matunda ili wananchi wafaidike kiuchumi.

Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na Jumuiya ya Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (Zati) na Kili Fair huku Benki ya Exim Tanzania ikiwa ni mdhamini mkuu.

“Zaidi katika kuthibitisha dhamira hiyo ni hivi karibuni tu tumepitisha Sheria mpya ya Uwekezaji ya mwaka 2024 ambayo imeongeza vivutio vingi katika sekta ya utalii na maeneo mengine. Kupitia sheria hii, wawekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo  ya utalii wanalindwa vema, na zaidi sheria hii inaambatana na vivutio kwenye eneo la kodi,’’ amesema Rais Mwinyi.

Awali, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga amesema Serikali imejipanga kukuza maendeleo jumuishi na endelevu katika sekta ya utalii, sambamba na kuwasaidia wawekezaji wadogo na wakubwa katika nyanja hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Ofisa Mtendaji wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu amesema wamejipanga  kuhudumia wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.

Amesema lengo ni kuunga mkono juhudi na kwenda sambamba na kasi na dhamira ya Serikali ya kuchochea ukuaji wa sekta hiyo muhimu.

 “Udhamini wetu mkuu kwenye mkutano huu ikiwa ni mara ya pili mfululizo ni uthibitisho wa wazi kabisa wa  dhamira yetu ya kuunga mkono juhudi za Serikali kukuza sekta ya utalii. Kupitia ushirikiano wetu na  Zati tumeweza kutoa suluhisho za kifedha kwa wanachama wake.” “Ushirikiano huu unadhihirisha msaada endelevu wa Benki ya Exim kwa sekta muhimu za uchumi ikiwamo ya utalii ya Zanzibar,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Zati, Rahim Bhaloo amesema mkutano huo uliohudhuriwa na wadau zaidi ya 600 unaofanyika kwa mara ya pili visiwani humo, unalenga kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya utalii wakiwemo watoa huduma na watumiaji wa huduma hizo, ili kuongeza wigo wa Zanzibar katika jukwaa la utalii kimataifa.