Dk Mwinyi kuimarisha sura ya Mji Mkongwe
Muktasari:
- Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aweka wazi mikakati ya kuendeleza na kuimarisha haiba ya Mji Mkongwe visiwani humo, kwa lengo la kuvutia wageni, kukuza sekta ya utalii kwa uchumi wa Taifa, lakini pia kulinda hadhi ya mji huo.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaweka mkazo katika kuyapa kipaumbele maeneo ya urithi hususani Mji Mkongwe, ili kuendana na makubaliano ya mkataba wa Kimataifa wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) wa mwaka 1972.
Kama kitovu cha historia, Mji Mkongwe umeandikishwa katika orodha ya Unesco ya Urithi wa Dunia.
Inaelezwa kuwa nyumba za mji huo, zimejengwa tangu mwaka 1830, wakati Sultani Sayyid Said alipohamisha makao makuu ya utawala wake kutoka Oman kuja Unguja, na kwa sasa mji huo unapokea watalii wengi kila mwaka.
Kauli ya Rais Mwinyi imetolewa leo Desemba 2, 2023; ikisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla kwenye sherehe ya siku ya Mji Mkongwe, iliyofanyika katika viwanja vya bustani ya Forodhani Zanzibar.
Katika hotuba hiyo, Rais Mwinyi amesema pato kubwa la nchi linategemea sana sekta ya utalii, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuutunza Mji Mkongwe ili kutanua wigo wa vyanzo vya utalii ikiwemo wa maeneo ya historia, ambao unaonekana kushamiri zaidi duniani katika miaka ya hivi karibuni.
Amesema katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Serikali imepanga kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kuyafanyia ukarabati majengo yote makongwe katika eneo la mji huo, sambamba na kuboresha maeneo yote ya wazi ikijumuisha bustani za Jamhuri garden, Victoria garden, African house pamoja na maeneo ya maegesho ya magari.
Aidha, Dk Mwinyi amesema Serikali ya Zanzibar imekusudia kutandaza upya mfumo wa maji na umeme chini ya ardhi ili kuondokana na mabomba ya maji na waya zilizotapakaa kila sehemu, ambazo zinaondoa haiba ya mji huo.
Ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikiiagiza wizara pamoja na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe, kuhakikisha wanaleta mapinduzi makubwa ya uhifadhi wa mji huo kwa kuupanga upya.
Hii ni pamoja na kudumisha usafi, kuziboresha bustani zote za mji huo, uondoaji wa biashara katika maeneo yasiyo rasmi pamoja na kuhakikisha usalama wa wageni.
Sambamba na hayo amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira bora kwa wafanyakazi na wajasiriamali kwa kujenga maeneo ya biashara yakiwamo masoko ya kisasa, kuleta mabasi maalumu yatakayotoa huduma ya usafiri katika eneo hilo la kihistoria.
Rais Mwinyi amesema lengo la kuleta mabasi hayo ni kupunguza msongamano wa vyombo vya usafiri ambao unahatarisha usalama wa majengo na kuleta usumbufu kwa watalii na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed Said amesema wataendelea kushirikiana na wananchi na wakazi wa Mji Mkongwe katika kuuendeleza kwa kuupanga na kutatua changamoto ili kuzidi kuupa hadhi yake.
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Undelezaji wa Mji Mkongwe, Ali Said Bakari amesema wamejipanga kuhakikisha mji huo unaendana na hadhi ya urithi wa miji kongwe ya dunia, sambamba na kulinda utamaduni wa Zanzibari ili uendane na matakwa ya Unesco.
Akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi Mkaazi wa Unesco nchini, Nanchy Mwaisaja amesema shirika hilo linaamini kuwa urithi wa Mji Mkongwe umeleta maendeleo makubwa na kukuza kipato kwa wananchi.