Tamu, chungu miaka mitatu ya Dk Mwinyi Zanzibar

Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi

Muktasari:

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi ametaja mambo aliyofanikiwa katika miaka mitatu ya utawala wake na yale yanayompa wakati mgumu hasa ufanisi mdogo wa Bandari ya Malindi.

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi ametaja mambo aliyofanikiwa katika miaka mitatu ya utawala wake na yale yanayompa wakati mgumu hasa ufanisi mdogo wa Bandari ya Malindi.

Dk Mwinyi aliingia madarakani Novemba 2, 2020, akiwa na ahadi za kukuza uchumi, ajira, kuimarisha amani, umoja wa kitaifa na mshikamano.

Akizungumza katika mahojiano kati yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu ikiwa ni sehemu ya Jukwaa la Fikra (MTLF) lililoandaliwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) Unguja jana, Rais Mwinyi alisema, “azma yangu ya kwanza katika uongozi wa nchi, ilikuwa ni kuleta amani, kwa sababu mimi naamini bila amani haya yote hatuwezi kuyazungumza.

“Pili, ni kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (Suki), nikiwa na imani kwanza itatuletea umoja, amani na mshikamano. Haikuwa rahisi, kulikuwa na mijadala mingi, lakini tuliifikia.”

Hata hivyo, Rais Mwinyi alisema kitu kinachomnyima usingizi kwa sasa ni ufanisi mdogo wa Bandari ya Malindi na ndio maana ameanzisha mkakati wa kuipa sekta binafsi ili kuiboresha.

“Nikiri athari za bandari ni jambo linalonipa sonona. Leo kuna kilio cha bei ya bidhaa na hili linasababishwa na mambo kadhaa, kwa mfano Pakistan kulitokea mafuriko, India wamezuia kuuza mchele nje, ikija meli hapa ikakaa muda mrefu maana yake wanapandisha bei. Moja ya sababu ni ufanisi mdogo wa bandari yetu,” alisema Rais Mwinyi.

Pia, alisema katika maeneo anayoyapa kipaumbele ni miundombinu ya bandari kwa kuiboresha ya Malindi na kujenga nyingine katika eneo la Mangapwani.

“Tunapata changamoto kwa sababu Bandari ya Malindi ya muda mrefu, miundombinu sio rafiki hakuna nafasi ya kuhifadhi yale makasha na ndio maana tumekuja na Bandari ya Mangapwani, ambako kutakuwa na nafasi ya makontena, gesi na mafuta na kuna eneo la bidhaa za nafaka, ilimradi eneo kamilifu,” alisema Rais Mwinyi.

Kuhusu usafirishaji majini, alisema Serikali inakusudia kuboresha usafirishaji katika visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya Mombasa (Kenya), Tanga na Comoro.

Alitaja maeneo mengine ya kipaumbele ni mafuta na gesi akisema kuna kampuni iliyofanya utafiti na kugundua kiwango kikubwa cha gesi.

Uwekezaji

Akifafanua zaidi kuhusu uwekezaji, alisema sera ya uchumi wa visiwa vya Zanzibar inategemea katika uchumi wa buluu ambao ndani yake kuna sekta kuu tano za utalii unaotegemea fukwe za bahari, bandari, uvuvi na ukulima wa mwani, mafua na gesi pamoja na usafirishaji wa baharini.

“Tumeweka vipaumbele, kwanza tutake tusitake uchumi wetu unategemea utalii, asilimia 30 ya pato letu linategemea utalii,” alisema Rais Mwinyi.

“Mashirika ya ndege yanayoleta watalii Zanzibar yamekuwa mengi kuliko viwanja vyote Tanzania, kwa kuwa idadi ya ndege za kimataifa zimeongezeka.”

“Hoteli zilizopo zaidi ya 600, ukija kipindi cha Krismasi hupati chumba maana yake kuna uwekezaji umefanyika,” alisema Rais Mwinyi.

Kuhusu sekta ya uvuvi na kilimo cha mwani, alisema Serikali imewekeza katika kilimo hicho, kikiwamo kiwanda cha kusanifu mwani ili kukuza uvuvi na kilimo cha zao hilo na kupata bei nzuri zaidi.

Rais Mwinyi, alipoulizwa kuhusu manung’uniko ya baadhi ya wananchi wasioridhishwa na uwekezaji hasa katika visiwa, aliwataka wananchi wasiwe na hofu.

Kauli ya Rais Mwinyi imekuja wakati kukiwa na minong’ono kuhusu kutolewa kwa baadhi ya visiwa kwa wawekezaji.

“Watu wamekuja kuwekeza Dola 100 milioni hawatakibeba kisiwa kile, miaka yote hoteli itabaki hapa, pale tutapata ajira, tutapata kipato na tutauza mazao yetu pale. Sasa kuna hofu kwamba kwa nini waje kuwekeza kwenye nchi yetu?,” alihoji Dk Mwinyi.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), hadi sasa kuna visiwa 17 vilivyotolewa kwa wawekezaji kati ya 52 vilivyopo.

“Lazima waje ili tunufaike. Kwa hiyo napenda kuwatoa hofu wananchi, kila tunapowekeza ni kwa manufaa mapana ya nchi yetu,” alisema Dk Mwinyi.

Hata hivyo, alisema Serikali imewekeza nguvu ili kuhakikisha kunakuwa na amani.

“Wawekezaji wengi wamepoteza fedha katika nchi zilizokuwa na vita, kwa mtu yeyote anapoleta fedha zake kwanza anaangalia amani,” alisema Rais Mwinyi.

“Pili, nchi hiyo ina sheria, ina sera, ina taratibu. Sisi tumefanikiwa kwa sababu sera zinatabirika. Tuna sera zinazotabirika, tunasheria za kumlinda mwekezaji.”

Uwajibikaji

Katika utawala wake, Dk Mwinyi alisema ameboresha taasisi za uwajibikaji ikiwamo Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya Kudhibiti Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca).

“Tunaisimamia vizuri kwa sababu tunataka value for money, ukipewa mradi wa kujenga hospitali ukasema ni Sh5 bilioni tunataka kuona thamani ya Sh5 bilioni,” alisema Rais Mwinyi.

“Lakini bila shaka watu wa namna hiyo hawakosi… wapo, vyombo vyetu vya usimamizi CAG, Zaeca kazi yao ni kuhakikisha mambo yanakwenda viruzi.”

Rais Mwinyi alipoulizwa anawezaje kujipima kiuadilifu katika utawala wake, alisema bado ni vigumu, lakini ameboresha mifumo.

“Kasoro zipo, kwa mfano nilipotembelea miradi nilikuta ipo nyuma na kuna makandarasi tumewafukuza,” alisema Rais Mwinyi.

Kuhusu uwajibikaji kwa watumishi wa umma na wananchi, alisema bado kuna changamoto ya watu kutopenda mabadiliko.

“Watu hawataki kuwajibika, hawataki kubadilisha mitazamo, hawapendi mambo mageni, lakini hatukati tamaa, tumeendelea kuleta mabadiliko na tumefanikiwa,” alisema Dk Mwinyi.

Alipoulizwa kuhusu mbinu anazotumia kufanikisha uongozi wake, alisema anatumia kanuni za utawala bora na kuwashirikisha wananchi badala ya kutumia nyundo (adhabu).

Umoja wa Kitaifa

Katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (Suki), alisema anatumia mbinu ya kusikiliza wanasiasa wenzake na kuwashirikisha.

“Tumesikiliza wenzetu wanachotaka hata katika chama ni lazima usikilize na hayo mambo tunayafanya sana,” alisema Rais Mwinyi.

“Tumefanikiwa kutokana na yale mambo watu wanayotaka, lakini changamoto hazikosi, kuna watu hawataki yale unayoamini, japo kwa kiasi kikubwa tumefanya yale wanayotaka.”

Kuhusu madai ya upendeleo katika teuzi zake, Dk Mwinyi alisema ameondoa hali hiyo.

“Suala la kaskazini na kusini sasa halipo, suala la Unguja na Upemba halipo, suala la Uarabu na Ungazija halipo. Kwa kiwango kikubwa tumejitahidi kuondoa hayo matabaka,” alisema Dk Mwinyi.

Sekta ya fedha

Akifafanua kuhusu soko la fedha visiwani hapa, alisema awali, hazikupewa kipaumbele katika kuchangia uchumi wa nchi.

“Awali, walikuwa wakikopesha wafanyabiashara wakubwa, safari hii tumewataka waikopeshe Serikali na tumepata mkopo mkubwa kwa kutambua uwezo wa kulipa upo,” alisema Dk Mwinyi.

“Pili, tuna miradi mikubwa, tutaendelea kufanya, hivyo kwa kutumia sekta mbalimbali. Kuna benki na kuna mifuko ya hifadhi ya jamii ambazo kuna fedha kule,” alisema.

Kuhusu mkakati wa kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha mapinduzi ya nne ya viwanda, alisema mpango huo upo na wameshaanza kuweka miundominu ya mawasiliano ya mkongo (fiber system) katika eneo la Fumba.

Miradi mikubwa

Kuhusu ujenzi wa miradi mikubwa, Dk Mwinyi alisema tangu alipoingia madarakani, watu hawakuelewa walipoona maeneo mengi yamezungushiwa mabati.

“Nchi zilizoendelea, utaona crane kwenda juu…ghorofa 80, 90 ghorofa ngapi…, sasa unaambiwa katika nchi zenye crane nyingi duniani ni Hong Kong na Dubai: Yale ni maendeleo. Sisi hatuendi mbali lakini yale ni maendeleo.

“Maana yake sasa wananchi wameshaelewa kwamba ukiona mabati maana yake kuna mradi unakuja na bila shaka utakuwa mkubwa,” alisema Dk Mwinyi.

Ahadi ya ajira

Kuhusu ahadi ya kuleta ajira 300,000 aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2020, Rais Mwinyi alisema ametekeleza kero tatu za wafanyabiashara wadogo ambazo ni mazingira bora ya biashara, mitaji na kodi.

“Kwa hiyo nilivyopata madaraka, nilifurahi kusema tumeweka ujenzi wa masoko makubwa katika maeneo mbalimbali. Soko la Mwanakwerekwe litakuwa na ukubwa mara tatu ya soko la Kariakoo (Dar es Salaam).

“Kuna soko la Jumbi na kuna masoko maeneo mbalimbali, maana yake kuna mazingira bora ya kufanya biashara,” alisema Dk Mwinyi.

Pia, alisema Serikali yake imetoa Sh3 bilioni kwa Benki ya CRDB ili kuwakopesha wafanyabiashara wadogo, huku kukiwa na mfuko unaoitwa Khalifa Fund kutoka Abu Dhabi.

Awali, Mkurugenzi wa MCL Bakari Machumu alisema kongamano hilo limetokana na changamoto waliyopewa na Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM Zanzibar, Khamisi Mbeto alipotembelea MCL Dar es Salaam Machi mwaka huu.

“Alitupa changamoto akisema hatutoi nafasi kubwa kwa habari za Zanzibar hasa kwa masuala ya maendeleo, na kusema, hatuwalazimishi mumsifie Rais wala chama chetu, bali andikeni mazuri yanayofanyika na changamoto mtuambie,” alisema Machumu akimnukuu Mbeto.

Alisema kongamano hilo ni mbinu za utoaji wa habari unaowezesha kujadili changamoto na kuzitafutia suluhisho.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZBC, Ramadhan Bukini alisema wamekuwa wakishirikiana na MCL kufanya vipindi vinavyowahusisha mawaziri na maofisa wa Serikali kuhusu mafanikio na changamoto za miaka mitatu ya Rais Mwinyi.