Mwinyi: Tumejipanga kutumia teknolojia malipo ya Serikali

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika Jukwaa la Fikra linaloangazia mafanikio, fursa na changamoto katika miaka 3 ya uongozi wake, linalofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, leo. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
- Dk Mwinyi amesema awali kulikuwa na uvujaji mkubwa wa mapato katika maeneo mbalimbali ikiwamo bandarini na uwanja wa ndege.
Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema wamejipanga kuanza kutumia teknolojia katika kufanya malipo ya huduma za Serikali na kuondoa matumizi ya fedha taslimu.
Kufanya hivyo kutasaidia kudhibiti upotevu wa fedha zilizokuwa haziingii serikalini ambazo sasa zitaweza kutumika katika utekelezaji wa miradi kwa kuongezewa nguvu na fedha zinazotokana na mikopo.
Ametoa kauli hiyo katika mahojiano ya ana kwa ana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL) Bakari Machumu katika kongamano la miaka mitatu ya Rais Mwinyi madarakati linalofanyika Zanzibar.
Dk Mwinyi amesema awali kulikuwa na uvujaji mkubwa wa mapato katika maeneo mbalimbali ikiwamo bandarini, uwanja wa ndege na hata katika upatikaji wa leseni za halmashauri.
Kutokana na kutambua hilo, moja ya eneo ambalo wamelipa msisitizo sasa ni la mageuzi ya kidijitali na matumizi ya teknolojia katika huduma zote zinazotolewa na Serikali.
Amesema itafika wakati mtu atakuwa hana haja ya kutumia fedha taslimu ikiwa anataka huduma mbalimbali ikiwamo kulipa kodi.
Rais Mwinyi amesema vitu hivyo vitakuwa vikifanyika kupitia njia ya mtandao na tayari upande wa kodi wameshaanza na sehemu nyingine iko njiani kufanya hivyo.
“Ukiweza kukusanya vizuri zile hela zinakupa uwezo wa kutekeleza bajeti yako. Eneo la pili tulilokuwa hatufanyi na sasa tunafanya ni pale unapotaka kujenga mradi wa Sh20 bilioni halafu unauwekea kila mwaka bajeti ya Sh2 bilioni mradi huo utakuchukua miaka 10 kumalizika, sisi tunasema tutafute fedha za mkopo halafu ile miaka kumi tulipe deni hilo,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema hiyo ndiyo sababu ya kuwapo kwa miradi mikubwa ikiwamo shule na hospitali kunatokana na kuchukua fedha wanazokuwa na uhakika wa kuzilipa kwa miaka kumi au mitano.
“Hakuna miujiza katika hilo ni mipango ambayo imekaa vizuri,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema katika utekelezaji wa mageuzi ya kidijitali na kuvutia uwekezaji katika upande wa teknolojia wameweka sera sahihi na kutenga eneo kubwa katika Mji wa Fumba ili kutengeneza kituo ambacho watu wenye nia ya kuwekeza katika teknolojia ya Tehama watatumia eneo hilo kuweka miradi mbalimbali.
Mbali na hilo amesema ili kuvutia wawekezaji wengi ni vyema kuhakikisha amani inakuwapo katika nchi kwa kuwa wawekezaji wengi kabla ya kuweka fedha zao wamekuwa wakitazama suala hilo.
“Mtu yeyote anayetaka kuleta fedha zake katika nchi anatazama hiyo nchi ina amani ndiyo maana tukasema tushughulikie migogoro ndani ya nchi, ambalo tumefanikiwa,” amesema Rais Mwinyi.
“Sisi tuna sera na sheria zinazotabirika, tuna kanuni zinazotoa vivutio vya uwekezaji, hivyo wanaokuja Zanzibar hawana wasiwasi wanajua mitaji yao iko salama,” amesema Dk Mwinyi.