LIVE: Sababu kufanyika Jukwaa la Fikra Zanzibar

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Bakari Machumu
Muktasari:
- Amesema kwa mara ya kwanza jukwaa la fikra linafanyika Zanzibar, huku likilenga kuwaleta wananchi pamoja kujadili changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa maslahi ya watu wa Zanzibar.
Unguja. Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Bakari Machumu amesema kampuni hiyo imeamua kuongeza nguvu Zanzibar kutokana na matakwa ya wadau kulingana na uhitaji wa maudhui.
Ameyasema hayo leo Oktoba 31, 2023 wakati akifungua Mwananchi Jukwaa la Fikra katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, kongamano ambalo limehudhuriwa na wadau mbalimbali likiongozwa na mgeni rasmi ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Amesema mwananchi kama chombo cha habari kina wajibu wa kuzitafuta fursa na kuzifanyia kazi kwa lengo la kuwahabarisha wananchi lakini pia kuanzisha makongamano maalumu ambayo yanalenga kugusia zaidi maendeleo ya Zanzibar.
Amesema kuanzishwa kwa mijadala ya aina hii ambayo kwa mara ya kwanza umefanywa na Mwananchi hapa Zanzibar leo ina tija kubwa pamoja na kukuza maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.
Amesema kongamano hili la Jukwaa la Fikra ni la 14 lakini ni la kwanza kufanyika hapa Zanzibar na lengo siyo tu kuwaleta watu pamoja wajadili matatizo yao lakini pia kutatoa fursa kutafuta suluhisho la matatizo ambayo yakitatuliwa yataleta faida kwa wote.