‘Wanafunzi Zanzibar wanapata mikopo kwa asilimia 100’

Muktasari:
- Wakati bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza ikiongezeka hadi kufikia Sh731 bilioni, wanafunzi wanaotoka Zanzibar wamekuwa wanufaika zaidi kutokana na kuwa na uhakika wa kupata asilimia 100 ya mikopo.
Dar es Salaam. Naibu Kamishna wa Michezo, Sanaa na Utalii kutoka Shirikisho la Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (Tahliso), Maimuna Kassim Yusuph amesema wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Zanzibar wana uhakika wa kupata mikopo kwa asilimia 100 jambo linalowapa amani katika masomo yao.
Ametoa kauli huyo wakati akifanya mahojiano katika kipindi cha Asubuhi Njema kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Morning Mwananchi ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ikiwa ni sehemu ya kuelekea majadiliano ya miaka mitatu madarakani ya Rais Hussein Ali Mwinyi.
“Sasa mtu anayepata mkopo nusu (asilimia 50) kupitia bodi ya mikopo ya elimu ya juu Tanzania anaweza kupata nyongeza kupitia bodi ya mikopo elimu ya juu Zanzibar," amesema Maimuna.
Wakati bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza ikiongezeka hadi kufikia Sh731 bilioni, wanafunzi wanaotoka Zanzibar wamekuwa wanufaika zaidi.
Akitolea mfano wa mtu aliyepata asilimia 75 ya mkopo, amesema Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar itampatia asilimia zinazobaki hivyo kumfanya kuwa na asilimia 100.
"Hii imekuwa ni neema kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kati kutoka Zanzibar, tunasoma kwa amani, hakuna tena hofu ya kulipiwa hela nusu imekuwa ni furaha sana," amesema Maimuna.
Akizungumzia kongamano hilo ambalo litakalofunguliwa na Rais Mwinyi, Msimamizi wa Miradi wa MCL, Edson Sosten amesema wakati wanaandaa jukwaa hilo waliangalia maeneo ya kuanzia.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni ya uchumi wa bluu, maendeleo ya miundombinu, Zanzibar kuwa kitovu cha teknolojia, afya, uwekezaji, vijana na utamaduni.
"Utamu zaidi wa jukwaa hili unaongezwa na mazungumzo ya moja kwa moja ya Rais na mkurugenzi wa Mwananchi, kupitia jukwaa hili ataelezea miaka yake mitatu ya alikotoka na anakoelekea," amesema Edson.
Amesema Mwananchi iko Zanzibar kuandika historia ya miaka mitatu ya Rais Mwinyi kwa kuwa tangu mwaka 2018, ilianza kuangalia fursa nyingine tofauti na kuandika.
Amesema vyombo vya habari vina kazi kuu tatu ambazo ni kuburudisha, kuelimisha na kuhabarisha.
"Tuliamua tusiishie kuandika, bali pia tujikite kwenye kutafuta suluhisho ya changamoto zinazoikabili jamii, tukaanzisha jukwaa la fikra linalowakutanisha wadau katika sekta husika na kujadili," amesema Edson.