Rais Mwinyi awatoa hofu wananchi kuhusu uwekezaji

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited, Bakari Machumu waliposhiriki Jukwaa la Fikra linaloangazia mafanikio, fursa na changamoto katika miaka 3 ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, linalofanyika leo katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
- Rais Mwinyi amesema wananchi wamechagua viongozi kwa ajili ya kufanya uamuzi utakaowaonesha njia, hivyo dhamira njema aliyonayo kwa wananchi ni kuleta matokeo sahihi kwao.
Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema uwekezaji ni hali ya watu kuleta miradi katika nchi husika.
Hata hivyo, amewatoa hofu wananchi kuhusu uwekezaji akisema wanufaika ni wananchi wenyewe ikiwamo kupata fursa za ajira.
Dk Mwinyi amesema hayo leo Oktoba 31, 2023 katika Jukwaa la Fikra la kuangazia miaka mitatu ya uongozi wake katika upande wa mafanikio, fursa na changamoto.
Akizungumza katika ukumbi wa Golden Tulip amesema ndani ya miaka mitatu wamejitahidi kutekeleza yote waliyodhamiria kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.
Pia, amewahamasisha wananchi wa ndani wasiogope kuwekeza kwa kuwa watapatiwa unafuu katika uwekezaji huo.
Amesema katika kuwatumikia wananchi mitihani ni sehemu ya maisha lakini lengo kuu ni kuleta amani na ndio sababu ya kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kisiwani hapa.
Hata hivyo, amesema changamoto iliyopo ni utendaji wa baadhi ya viongozi ambao hawataki mabadiliko lakina hakukata tamaa na amepiga hatua.
"Katika uongozi lazima uwe na utawala bora utakaofuata Katiba na sheria na kuwashirikisha watu katika kufanya uamuzi wenye tija ndani yake," amesema Rais Mwinyi.
Pia, amesema wananchi wamechagua viongozi kwa ajili ya kufanya uamuzi utakaowaonesha njia hivyo dhamira njema aliyonayo kwa wananchi ni kuleta matokeo sahihi kwao.
Ameeleza kuwa uongozi bora lazima utoe fursa ya kusikiliza na kushirikisha wananchi katika kuleta mabadiliko
"Katika kuhakikisha uongozi bora nimeondoa hali ya upendeleo wa makabila kwa nchi kwa kuwa hali hii itawezesha Zanzibar kufikia ile sehemu nzuri ambayo kila mmoja ataweza kunufaika na lengo ni kuondoa matabaka," amesema Mwinyi.
Akizungumzia manufaa ya utalii visiwani hapa, amesema wana mipango ya kujenga maeneo ya makumbusho ili kuongeza thamani ya watalii na kuwafanya kumalizia mahitaji yao yote kisiwani hapa.
Pia, amesema vyanzo vikuu viwili wanavyotumia kukusanya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ni fedha zilizokuwa zikipotea pamoja na kupata fedha za mkopo wanazotumia kutekeleza miradi hiyo.