Petroli yapaa, dizeli ikishuka Zanzibar

Muktasari:
- Kwa Juni, lita moja ya petroli iliuzwa kwa Sh2,968, ikilinganishwa na Julai ambapo bei hiyo imeongezeka hadi Sh2,996. Hili ni ongezeko la Sh28 kwa lita, sawa na asilimia 0.94. Ongezeko ambalo linaweza kuathiri gharama za usafirishaji na maisha ya kila siku kwa wananchi.
Unguja. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), imetangaza kupanda kwa bei ya petroli kwa Sh29 huku bei ya dizeli imeshuka kwa Sh255 kulinganisha na mwezi uliopita.
Zura imetangaza kuwa kuanzia leo, Julai 9, 2025 bei ya petroli itakuwa Sh2,996 kwa lita, ikilinganishwa na bei ya Juni ya Sh2,968.
“Ongezeko hilo ni Sh29 sawa na asilimia 0.94 linalotokana na mafuta hayo kupanda katika soko la dunia na changamoto ya usafiri,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ambayo imethibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa mamlaka hiyo, Mbarak Hassan Haji.
Mbaraka kwenye taarifa hiyo iliyotolewa leo Julai 9, 2025 amesema mafuta ya dizeli yatauzwa kwa Sh2,907 kwa mwezi huu kutoka Sh3,162 sawa na punguzo la Sh255 sawa na asilimia 8.06.
Ameeleza kwa upande wa mafuta ya taa yamepungua kwa Sh150 ambapo kwa Julai lita moja itauzwa kwa Sh3,000 ikilinganishwa na Sh3,150 iliyouzwa Juni sawa na asilimia 4.76.
Mafuta ya ndege yamepungua kwa Sh151, kutoka bei ya Juni ya Sh2,521 hadi Sh2,370 kwa lita moja itakayouzwa Julai mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 5.99.
Hata hivyo, Zura imeeleza sababu ya kupungua kwa bei za mafuta ya dizeli, taa na mafuta ya ndege kwa mwezi huu ni kupungua kwa bei ya ununuzi katika soko la dunia, kupungua gharama za uingizaji mafuta kutoka katika soko la dunia hadi Zanzibar na mabadiliko ya fedha za kigeni.
“Zura hupanga bei hizo kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani.
“Mambo mengine ni gharama za uingizaji mafuta katika bandari ya Dar es salaam na Tanga, gharama za mabadiliko ya fedha za kigeni zinazotumika kununulia mafuta, za usafiri, bima na premium hadi Zanzibar, tozo za Serikali na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja,” imeeleza taarifa hiyo.
Maoni ya wadau
Baadhi ya watumiaji wa nishati hiyo wamependekeza Serikali iweke akiba ya kutosha ya mafuta ili kupunguza athari za uagizaji wa mara kwa mara na kuhimili mabadiliko ya bei sokoni.
Hamid Yussuf Said, mkazi wa Kijangwani na dereva wa teksi, amesema kuwa ikiwa kutakuwa na uhifadhi wa mafuta wa kutosha, itasaidia kupunguza changamoto za kupanda na kushuka kwa bei ya nishati hiyo.
“Binafsi ningeshauri kama kuna uwezekano tukawa na mafuta mengi ya kutosha ili kupunguza changamoto hii, angalau yakiagizwa mafuta ya miezi hata mitatu,” amesema.
Kuhusu akiba ya mafuta, Mkurugenzi Mkuu wa Zura, Mbaraka amesema kuwa Zanzibar bado haina uwezo wa kuhifadhi mafuta kwa kipindi cha angalau miezi mitatu, na kwa sasa kuna uwezo wa kuhifadhi yanayotosha kwa matumizi ya takriban mwezi mmoja pekee.
Hata hivyo, amesema tayari kuna mpango wa kuimarisha mfumo wa uhifadhi wa mafuta, na baadhi ya wawekezaji wameshajitokeza kuunga mkono juhudi hizo.
Amesema mamlaka inatarajia kuwa ndani ya miaka miwili ijayo, Zanzibar itakuwa na uwezo wa kuhifadhi mafuta ya kutosha kwa muda mrefu, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa kila mwezi.
Aidha, amewahimiza wananchi kununua mafuta katika vituo halali na kudai risiti za kielektroniki kila wanaponunua nishati hiyo, ili kuepuka udanganyifu na kuchangia kuongeza mapato ya Serikali.