Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Mwinyi awataka wahitimu kuwa viongozi wa mabadiliko

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika mahafali ya 63 ya Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), yaliyofanyika jijini Chennai, nchini India alipokuwa mgeni rasmi katika mafahi hayo.

Muktasari:

  • Amewataka wahitimu kuwa wabunifu na viongozi wa madiliko katika jamii

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema elimu na maarifa havitakuwa na maana iwapo havitatumika kutatua changamoto za jamii, kubadilisha maisha ya watu na kujenga mataifa yenye maendeleo endelevu.

Hivyo amewataka wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), kuwa wabunifu na viongozi wa mabadiliko katika jamii zao.

Dk Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 17, 2026 katika mahafali ya 63 ya Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), yaliyofanyika jijini Chennai, nchini India alipokuwa mgeni rasmi katika mafahi hayo.

"Elimu haipaswi kuonekana kuwa maandalizi ya kupata ajira pekee, bali ni nyenzo ya kujenga Taifa, kuimarisha jamii na kuandaa kizazi chenye maarifa, ujasiri na dhamira ya kuleta mabadiliko chanya," amesema.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar, Dk Mwinyi ameeleza kuwa mafanikio ya kweli hayapimwi kwa ukubwa wa cheo, nafasi ya kazi, utajiri au kutambuliwa binafsi, bali kwa maisha yaliyoguswa na kuboreshwa, fursa zilizofunguliwa kwa wengine, imani iliyojengwa na matumaini yaliyoachwa katika jamii.

Dk Mwinyi amewahimiza wahitimu kuzingatia uadilifu, unyenyekevu, huruma na utumishi kwa watu, akisisitiza kuwa ubunifu haupaswi kupimwa kwa ugumu wa teknolojia, bali kwa uwezo wake wa kuleta manufaa kwa wananchi.

Pia, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka elimu katika kiini cha Dira ya Maendeleo ya Taifa, ikiwa msingi wa ubunifu, ustawi wa wananchi, utawala bora na utekelezaji wa Ajenda ya Uchumi wa Buluu.

Ameongeza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji uwekezaji katika watu, hususan kuwawezesha vijana kuwa wazalishaji wa maarifa na teknolojia.

Akizungumzia Kampasi ya IIT Madras Zanzibar, Rais Mwinyi amesema kuanzishwa kwake kumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kielimu baina ya Tanzania na India, pamoja na kutoa fursa za kubadilishana maarifa, uzoefu na tamaduni baina ya wanafunzi wa Afrika na India.

Amesema dhamira ya Zanzibar ni kuifanya kampasi hiyo kuwa kituo cha umahiri katika elimu, utafiti, ubunifu na ujasiriamali kwa ukanda wa Afrika Mashariki, kitakachowakutanisha wataalamu kutafuta suluhisho za changamoto na kuibua fursa mpya za maendeleo.

Dk Mwinyi pia ameipongeza IIT Madras kwa mchango wake katika kuzalisha wahandisi, wanasayansi na wajasiriamali, pamoja na kuendeleza tafiti na ubunifu wenye mchango katika maendeleo ya jamii na uchumi duniani.

Katika hafla hiyo, Rais Dk Mwinyi ameshiriki kuwatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu ya juu, wakiwemo wa shahada ya kwanza na shahada ya uzamivu (PhD).

Pia, amekabidhiwa tuzo Maalumu na uongozi wa IIT Madras kwa kutambua mchango wake katika kuanzishwa na kuendelezwa kwa Kampasi ya IIT Madras Zanzibar.

Hafla hiyo pia iliambatana na uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kampasi mpya ya kudumu ya IIT Madras Zanzibar.

Rais Mwinyi aliondoka Zanzibar Julai 16, 2026, akiambatana na Mkewe Mariam Mwinyi, na ujumbe wake, kuelekea nchini India kwa ziara ya kikazi.