Serikali yakiri kutofanya tafiti za chanzo ugonjwa wa mtoto wa jicho

Muktasari:
- Katika kukabiliana na ugonjwa huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya imeweka mikakati ya kupambana na tatizo hilo ikiwemo kuendesha kambi za uchunguzi wa magonjwa ya macho na matibabu yake.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeeleza kuwa haijawahi kufanya utafiti rasmi kuhusu chanzo cha ugonjwa wa mtoto wa jicho, japokuwa inatambua uwepo na athari za ugonjwa huo miongoni mwa wananchi.
kupitia Wizara ya Afya Zanzibar imeeleza kuwa mtoto wa jicho ni miongoni mwa changamoto kubwa za afya ya macho zinazowakumba wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini.
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, kati ya watu 14,500 wanaosumbuliwa na matatizo ya macho, takribani 9,000 hukabiliwa na ugonjwa huo.
Hayo yameelezwa leo, Jumanne, Juni 17, 2025 na Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui.
Dk Mohammed alitaka kufahamu kama Serikali ilishawahi kufanya utafiti a chanzo cha ugonjwa wa mtoto wa jicho na mkakati wa kupata tiba kwa wagonjwa hao, kwa kuwa unaonekana kuwa ni moja ya matatizo makubwa ya macho, yanayoathiri wananchi Zanzibar na kuhusishwa na imani za kishirikina.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri amesema tafiti mbalimbali duniani zilizofanyika na matokeo ya tafiti yake, yameonyesha kuwa mtoto wa jicho husababishwa na mabadiliko ya kimaumbile ya lenzi ya jicho, ambayo yanaweza kuletwa na sababu mbalimbali.
Miongoni mwa sababu hizo, ni umri mkubwa kuanzia miaka 40, magonjwa ya kisukari, maambukizi ya macho, urithi na matumizi ya muda mrefu ya dawa za 'steroid'.
Hafidh amesema, katika kukabiliana na ugonjwa huo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya, imeweka mikakati ya kupambana na tatizo hilo ikiwemo kuendesha kambi za uchunguzi wa magonjwa ya macho na matibabu yake.
Pia, amesema Serikali inatoa elimu kwa wananchi kuhusu njia sahihi za kujikinga na ugonjwa wa macho pamoja na kupunguza imani potofu za kishirikina, zinazoweza kuchelewesha matibabu.
Vilevile, imesema inaimarisha uwezo wa watendaji na miundombinu ya hospitali na vituo vya afya kuhakikisha huduma za macho zinapatikana kwa urahisi.
Aidha, Serikali imesema inaendelea kusomesha madaktari bingwa wa macho na wataalamu wa upasuaji wa mtoto wa jicho, ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma bora.