Tatizo la maji pasua kichwa Zanzibar, sababu zatajwa

Wananchi wakichota maji katika moja ya eneo ambalo wanagawa maji kusaidia upungufu wa huduma hiyo katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Uzalishaji wa maji haujafikia mahitaji, na wananchi wanalazimika kutumia vyanzo visivyo salama.

Unguja. Pamoja na Kisiwa cha Zanzibar kuzungukwa na maji ya bahari kila eneo, bado wananchi wake wanahangaika kupata huduma ya maji safi na salama.

 Zanzibar ina ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya 2600 ikiwa na idadi ya watu milioni 1.8 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kutoka watu milioni 1.3 wa sensa ya mwaka 2012.

Uzalishaji wa maji umefikia asilimia 67 kwa Unguja na Pemba, huku Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ikitaka kufikia mwaka 2025 uzalishaji uwe umefikia asilimia 85.

Kwa mujibu wa hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Waziri wa Maji, Nishati na Madini mwaka wa fedha 2023/24, mahitaji ya maji nchini ni lita za ujazo 240.4 milioni kwa siku na uzalishaji ni lita 146.9 milioni kwa siku sawa na upungufu wa lita 93,538,782 kwa siku. 

Hata hivyo, maji yanayopatikana mengi hayapo katika mfumo rasmi wa Mamlaka ya Maji (Zawa), wananchi wanatumia visima vya asili, mito, madimbwi madogo na vyanzo vingine vya maji ambayo yanaeleza kuwa na chunvi.

 Licha ya maeneo mengi kutokuwa na huduma hiyo, upatikanaji wake unatofautiana kati ya eneo moja na lingine, huku mikoa ya Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Pemba ikiwa na changamoto zaidi.

 Katika Kijiji cha Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja wananchi wa eneo hilo wanasema tangu Mapinduzi yawepo Januari 12, 1964 hawajawahi kupata huduma ya maji safi na salama, badala yake hupata maji yao kununua kutoka maeneo mengine kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, hususan ya kunywa.

 Kama inavyojulikana kiwango cha joto Zanzibar kipo juu wastani wa nyuzi setigrade 32, hivyo na matumizi ya maji kwa ajili ya kunywa yanakuwa juu.

 “Maji tunanunua Sh500, tunanunua kutoka Pongwe zaidi ya kilometa 20, yanafuatwa na gari, kama hujupata hayo tunatumia maji ya chunvi,” amesema mkazi wa kijiji hicho, Mwanaisha Juma. 

 Mkazi mwingine Huwaida Hemed amesema: “Tunapata shida kweli kila siku ndoo kichwani, kwa siku unaweza kununua maji hadi madumu sita kwa ajili ya matumizi, kila siku tunaeleza shida yetu ya maji lakini hatuoni utekelezaji wake.”

 Mkurugenzi wa Taasisi inayosaidia upatikanji wa maji Zanzibar (Zac), Mahfoudh Shabani Haji amesema hakuwezi kuwa na uzalishaji wa kutosha iwapo hakuna maji, kwani mazao na binadamu wanategemea huduma hiyo.

 Kiongozi wa kamati ya shehia ya Kihengwa, Naftar Hussein amesema wameshaomba kwenye mamlaka iwapo kuna harakati nyingine zinaendelea za kupata maji, ni vyema wakasaidiwa wapate hata angalau maji ya mapangoni ambayo yatawasaidia angalau kufua, kuogea na huduma zingine za kawaida.

 Katika Kijiji cha Matwemwe Kigomani ambacho kina wakazi zaidi ya 4,349 wao wanapata maji mara moja kwa wiki ambayo yanatoka usiku, hivyo inakuwa ni nadra kupata huduma hiyo kwani wanakuwa wamelala.

 Mwajuma Makame Haji, amesema maji yanakuja usiku wakati wamelala, huku wakitumia gharama kubwa kufuata huduma hiyo kwenda Kijiji kingine cha Mkwajuni.

 “Wengine ni walemavu, wagonjwa hawana uwezo wa kutafuta maji, mimi hata mke wangu ni mgonjwa na hatuna watu wa kuagiza maji,” amesema Kesha Makungu, mkazi wa Kigomani akiiomba Serikali iwaangalie kwa jicho la pekee.

 Kauli hiyo inaungwa mkono na mkazi mwingine wa Kijiji hicho, Othman Haji akisema hata yanapotoka hawana uwezo wa kuyafuata bombani, kwani usiku unatisha na mazingira ya kijiji hicho ni ya kuogofya.

 Madai ya wananchi hao yanathibitishwa na Tanu Muhamed Haji, Sheha wa Shehia ya Kigomani anayesema wamefuatilia suala hilo, lakini hawapati mrejesho unaoeleweka kutoka kwenye mamlaka. 

 Wanaoangaika kwa asilimia kubwa ni wanawake na watoto, hivyo hali hiyo inaathiri maendeleo yao na jamii inayowazunguka.

 Kutokana na hali hiyo wanawake wanatumia muda mrefu kusaka huduma hiyo, hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na watoto wakati mwingine kuwa na mahudhurio hafifu shuleni.


Gari likiwa limepakia madumu ya maji katika Shehia ya Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja. Dumu moja la maji linauzwa kwa Sh500. Picha na Jesse Mikofu 



Kauli ya Zawa

Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa) inakiri kuwapo kwa changamoto hizo. Hata hivyo, inasema hali ni tofauti na kipindi kilichopita na zipo jitihada mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha tatizo hilo linapungua.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Salha Mohamed Kassim amesema nia ya Zawa ni kuhakikisha maji yanapatikana kwa asilimia 100 na kutokana na mipango waliyonayo wana imani itafanikiwa.

 Anasema kazi wanayoifanya ni kuendeleza walipoachia watangulizi na ndani ya miaka mitatu sasa wametekeleza miradi mikubwa ya maji ambayo uzalishaji wake unaweza kushinda uzalishaji wa zile awamu zote saba zilizopita.

 Maji ya Zanzibar yanapatikana chini ya ardhi, kwa hiyo kazi wanayoifanya ni kuchimba ambayo ndani yake wanapata maji, wanayasafisha, wanayahifadhi kisha wanayapeleka kwa wananchi.


Mradi wa Benki ya Exim

Amesema kuna miradi mikubwa inatekelezwa sasa kuhakikisha tatizo hilo linaondoka ukiwemo wa Benki ya Exim wenye thamani ya Dola  milioni 92.18 za Marekani (Sh232 bilioni).

 Dk Salha amesema katika mradi huo, wamechimba visima vikubwa 64 vyenye uwezo kuzalisha maji lita za ujazo 177 milioni kwa siku.


Kabla ya miradi hiyo, walikuwa wanazalisha maji lita 143 kutoka kwenye visima 308 vidogo. 


Anasema wametumia njia ambayo ni nzuri, zamani maji yalikuwa yakitoka kwenye kisima yanakwenda moja kwa moja kwa wananchi, lakini kwa sasa wamejenga matangi kwa ajili ya kuhifadhi maji hata ikitokea hitilafu huduma inaendelea kawaida.


Kwa mujibu wa Zawa, kuna skimu saba ambazo kuna jumla ya matangi 15 zote kwa pamoja zina uwezo kuhifadhi maji lita 134 milioni.


“Mradi wa Kwarara ndio una matangi matatu kubwa la chini lina uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 32.5 milioni, juu kuna tangi mbili na kila moja lina uwezo wa kuhifadhi lita 5.5 milioni kwa hiyo kwa Kwarara peke yake kuna uhifadhi lita 43 milioni,” amesema. 


Kwa sasa hatua inayoendelea ni kuwafungia wananchi maji wapate majumbani kwao, mradi utahudumia shehia 36.


Katika mradi huo, wananchi wote watafungiwa mita za maji, kwa awamu zote za utawala ilifunga mita kwa wananchi 20,000 “kwa hiyo kwa sasa tutapima jinsi gani mwananchi anatumia maji.”


Kutokana na fedha za ahueni ya Uviko-19, Zawa walipata Sh34.2 bilioni hivyo waliongeza visima vipya 38 na kutengeneza skimu 10 kwa kujenga matangi mengine 10, matano Pemba na mengine Unguja kila tangi lina ujazo wa maji lita milioni moja.

  

Pia Zawa imeendeleza visima 36, imeweka pampu na kuweka mashine, pia imebadilisha pampu visima vya zamani 49 ambapo jumla ya pampu 123 zimenunuliwa.


Katika fedha hizo Zawa imejenga vibanda vya kuhifadhia pampu 52, 26 Pemba na vingine Unguja kadhalika yamenunuliwa magari mawili kuchimbia na kulaza mabomba kilometa 319.


Kwa mujibu wa Zawa, kuna miradi mikubwa ipo kwenye mipango ya kutekelezwa ambayo ikikamilika watafikia asilimia 100 na huduma hiyo kupatikana kwa saa 24.


Alichokisema Waziri

Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaib Hassan Kaduara amesema Serikali inapambana kuwaondolea wananchi changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote ya mjini na vijijini.

Amesema sekta ya maji inakumbwa na ongezeko la mahitaji ya maji kunakochochewa na ongezeko la idadi ya watu, kukua kwa miji pamoja na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo uwekezaji na utalii, mabadiliko ya tabianchi, uvamizi wa vyanzo vya maji.

Pia uchakavu wa miundombinu ya maji na mwitikio mdogo wa wananchi kuchangia huduma ya maji, vyote hivyo vinaipa changamoto kubwa sekta ya maji. 

Amesema katika kutatua changamoto hiyo, wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo ujenzi wa visima na matangi vya maji.

“Serikali tutahakikisha tunaondosha changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yote ya Mjini na Vijijini katika visiwa vya Unguja na Pemba,” amesema Kaduara.

Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi Yahya Rashid Abdalla hivi karibuni kamati hiyo ikikagua miradi ya maji Pemba, aliitaka Wizara ya Maji Nishati na Madini kuwajibika ipasavyo, ili kuwaondeshea shida ya maji wananchi wa kisiwa hicho.


“Wizara ya Maji mnapaswa kuchukua jitihada za makusudi katika kuhakikisha mnawaondoshea shida ya huduma ya maji safi na salama wananchi wa kisiwa hiki,” amesema.