Vijana 110 wafundwa uwajibikaji Zanzibar

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Jumuiya inayojihushisha na Changamoto za kuwakabili vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Abdalla Ali Abeid amesema kuna kundi kubwa la vijana wanaopaswa kujengewa uwezo kuisaidia Serikali katika kukuza uchumi wa nchi.

Unguja. Mkurugenzi wa Jumuiya inayojihushisha na Changamoto za kuwakabili vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Abdalla Ali Abeid ameeleza umuhimu wa vijana kushirikishwa katika maendeleo kwa lengo la kuongeza uwajibikaji serikalini.

 Ameyasema hayo leo Novemba 20 wakati akizungumza na Mwananchi Digital Zanzibar kuhusu mradi wa vijana wanaoutekeleza kwa ushirikiano na shirika la Forum CV la nchini Sweden katika wilaya nne za Unguja na Pemba kwa kipindi cha miezi 18.

Amesema katika mradi huo vijana wapatao 110 watajengewa uwezo kwa lengo la kuongeza uelewa na uwajibikaji ambao utasabishwa na vijana hao.

“Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa ndiyo maana sisi tunawejengea uwezo tukiamini tunapanda mbegu nzuri na tayari kuna vijana miongoni mwao wameanza kufuatilia vyema maendeleo ya miradi katika maeneo yao wanayoishi,” amesema.

Miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo, Hamad Shehe kutoka Wilaya ya Micheweni Pemba amesema kuna mafanikio makubwa ambayo amepata tangu kuanza mafunzo hayo.

Amesema kwa sasa ana uwezo mkubwa wa kudadisi mambo mengi ambayo akiona hayaendi sawa na kutafuta njia bora za kutatua changamoto pale wanapoona pamekwama.

Naye Khadija Abdalla amesema kupitia mafunzo hayo ameweza kufuatilia miradi ya maendeleo ikiwemo upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwenye eneo analoishi.

Amesema baada ya tatizo hilo kuwepo kwa muda mrefu kijijini kwao aliwaona wahusika kuwaeleza kwa undani zaidi shida wanayopata wannachi kutokana na kukosa huduma ya maji.

“Kufuatilia kwangu kulikwamua tatizo hili na hivi sasa kwa muda wote wananchi wameondokana na chagamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama,” amesema.