Watendaji kada ya afya Z’bar sasa kupimwa kwa ubora wa huduma
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mngereza Mzee Miraji akizungumza wakati kikao cha kutathimini na kusonga mbele katika kutoa huduma bora Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Hatua hiyo inalenga kuimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za rufaa baada ya kuimarika kwa ujenzi wa miundombinu.
Unguja. Baada ya uwekezaji katika miundombinu, vifaa na fedha katika sekta ya afya, Wizara ya Afya Zanzibar imesema sasa jukumu lililobaki kwa viongozi ni kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha matokeo, huku watendaji wake wakipimwa katika utoaji wa huduma.
Kauli hiyo imetolewa leo, Juni 29, 2026, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mngereza Mzee Miraji, wakati wa kikao cha kutathmini na kupanga hatua za kusonga mbele katika utoaji wa huduma bora za afya, kilichoandaliwa na wizara hiyo kwa kushirikiana na PharmAccess na kuwakutanisha viongozi na wadau wa sekta ya afya Zanzibar.
“Kuanzia sasa hatutapimwa kwa idadi ya hospitali tulizojenga, bali tutapimwa kwa ubora wa huduma zinazotolewa ndani ya majengo haya.
“Kinachofuata, tusije kulaumiana kwa kuwa tunataka mabadiliko. Hatutaki tufanye mambo yaleyale halafu tupate matokeo tofauti. Lazima tukubaliane kuwa tunasimamia pia suala la ubora,” amesema.
Amesema kuanzia Julai mosi, ngazi ya utawala haitakuwa na mjadala na mtumishi yeyote wa kada hiyo atakayekwenda kinyume na maelekezo hayo, wakianzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mkoa hadi rufaa.
Dk Mngereza amesema katika kipindi hiki kuelekea mwaka 2030, wanataka kila idara na kurugenzi ijipange katika maeneo matano, ikiwamo kuimarisha ubora wa huduma na usalama wa mgonjwa katika nyanja zote.
Pia, amesema kuna suala la kuimarisha mifumo ya rufaa kati ya hospitali za wilaya, mkoa na rufaa kwa sababu huduma bora zinaanzia ngazi ya msingi.
“Hatutakuwa na justification (uthibitisho) ya changamoto za wajawazito kwa kisingizio cha kukosa taarifa, kwa sababu kuna mfumo wa jamii ni afya. Unaweza kufanya rufaa katika vituo vinavyofuata kupitia wahudumu wa ngazi ya jamii, ambao wanafanya kazi zao. Hivyo, hatutegemei wajawazito wapate changamoto na sisi hatuna taarifa,” amesema.
Pia, amesema jambo lingine wanaloliimarisha ni uwajibikaji na usimamizi wa utendaji ili viongozi wawe viongozi wa matokeo.
“Wewe ni nesi, sijui mkunga au mtaalamu yeyote; kwa nafasi yako, amka asubuhi ukawahudumie watu, na si kupiga porojo,” amesema.
Kwa mujibu wa mtendaji mkuu huyo wa wizara, taarifa za mahudhurio zinazopelekwa ofisini kwake zinaonesha wataalamu wanahudhuria siku 14 kati ya 30 za mwezi, jambo ambalo si sawa.
Hata hivyo, amesema kuna haja ya kufanya uamuzi kwa kutumia takwimu na si hisia, kwani kufanya hivyo kunaweza kuathiri utendaji au kusababisha uamuzi usiofaa.
Meneja wa Mradi kutoka PharmAccess, Dk Faiza Abasi, amesema wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya Afya tangu mwaka 2020, na eneo moja la ushirikiano ni kuboresha huduma za afya katika vituo vyote vya afya kuanzia zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya hadi mikoa.
“Na katika ushirikiano huu, lengo ni kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa katika hospitali ni huduma zilizo katika kiwango cha juu,” amesema Dk Faiza.
Amesema walipoanza walitengeneza miongozo inayoelekeza jinsi watakavyoweza kupima ubora wa huduma za afya.
“Ubora huu tunaupima katika ngazi mbalimbali, tunaanza katika ngazi ya kwanza, ya pili, mpaka ya tano, kama vile tunavyopima ubora wa hoteli. Hata huduma za afya tunazipima hivyo hivyo, na kwa Zanzibar hakuna kituo cha afya ambacho kimefikia ngazi ya tano; vingi vipo kuanzia ngazi ya kwanza hadi ya tatu,” amesema.