Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wizara yazindua nyenzo za bajeti inayozingatia usawa wa kijinsia

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik Akil na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Anna Athanas Paul wakizindua nyenzo za bajeti inayozingatia usawa wa kijinsia (GRB). Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Katika jitihada za kuimarisha usawa wa kijinsia, Serikali imepanga kutumia Sh449.799 bilioni.

Unguja. Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik amesema bajeti ndiyo nyenzo kuu inayotumiwa na Serikali kutekeleza sera na mipango ya maendeleo.

Hivyo, amesema ni muhimu kuhakikisha uamuzi wa matumizi ya rasilimali unazingatia mahitaji ya wananchi wote ili maendeleo yawe jumuishi na yenye manufaa kwa kila mmoja.

Dk Malik ameyasema hayo leo Alhamisi, Juni 25, 2026, wakati wa uzinduzi wa nyenzo za Bajeti Inayozingatia Usawa wa Kijinsia (GRB) uliofanyika katika Ukumbi wa Wazee, Amani, Mjini Unguja.

Nyenzo zilizozinduliwa ni pamoja na mwongozo wa tathmini ya athari za kijinsia kabla ya utekelezaji wa miradi na programu, mwongozo wa bajeti inayozingatia jinsia kuanzia hatua ya upangaji hadi ufuatiliaji wa matokeo, mwongozo wa bajeti inayozingatia jinsia kwa Baraza la Wawakilishi pamoja na mwongozo wa ukaguzi unaotilia mkazo masuala ya kijinsia na orodha za ukaguzi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Malik amesema nyenzo hizo zitasaidia kuimarisha ubora wa maamuzi ya Serikali kwa kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha ugawaji wa rasilimali unazingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya wananchi.

Amesema hatua hiyo itawezesha bajeti za Serikali kujibu kwa ufanisi mahitaji ya wanawake na wanaume katika maeneo mbalimbali ikiwemo uzalishaji, ajira, elimu bora, huduma za afya, lishe, ulinzi na upatikanaji wa huduma jumuishi.

“Matokeo yake ni kwamba bajeti za Serikali zitakuwa na uwezo wa kujibu mahitaji ya wanawake na wanaume katika shughuli za uzalishaji na ajira, upatikanaji wa elimu bora, huduma za afya, lishe na ulinzi pamoja na huduma jumuishi,” amesema.

Aidha, amesema kupitia nyenzo hizo, Zanzibar itaweka msingi imara wa kuhamisha ajenda ya usawa wa kijinsia kutoka kuwa suala la kisera pekee na kuifanya kuwa sehemu ya mifumo rasmi ya upangaji wa bajeti, usimamizi na uwajibikaji wa Serikali.

Dk Malik amesisitiza kuwa uzinduzi huo ni mwanzo wa hatua mpya ya utekelezaji, akizihimiza wizara, idara, taasisi za Serikali na wadau wengine kuhakikisha nyenzo hizo zinatumika kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Anna Athanas Paul amesema nyenzo hizo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya wizara yake katika kuendeleza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake na ustawi wa makundi mbalimbali ya jamii.

Amesema matumizi ya nyenzo hizo yataimarisha uwezo wa wizara na wadau wengine kuhakikisha masuala ya kijinsia yanazingatiwa katika mipango, bajeti na utekelezaji wa programu za maendeleo.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), Katherine Gifford amesema uzinduzi huo ni kichocheo muhimu cha kuharakisha mabadiliko ya kitaasisi na kuimarisha uwajibikaji katika kutimiza ahadi za usawa wa kijinsia.

Amesema mafanikio ya nyenzo hizo hayatapimwa kwa uwepo wake pekee, bali kwa namna zitakavyotumika kuboresha sera, ugawaji wa rasilimali, utoaji wa huduma na hatimaye kuinua maisha ya wananchi wa Zanzibar.