Zanzibar kuandaa mwongozo matumizi nishati safi

Mwakilishi wa Chonga, Suleiman Masoud Makame akizungumza barazani kuhusu mipango ya serikali ya kupambana na nishati chafu
Muktasari:
- Hayo yamebainishwa leo Jumanne Mei 27, 2028 wakati mawaziri wa SMZ walipokuwa wakijibu hoja za wawakilishi.
Unguja. Katika kupambana na uharibifu wa mazingira na kulinda afya za wananchi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inaandaa mwongozo maalumu wa matumizi ya gesi asilia hatua itakayosaidia utunzaji wa mazingira kutokana na matumizi ya nishati chafu ikiwamo kuni na mkaa.
Pia, Serikali ipo kwenye mchakato kutafuta wawekezaji kufunga mitambo kisiwani hapo kwa ajili ya gesi ya magari kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Mei 27, 2025 wakati mawaziri wa SMZ walipokuwa wakijibu hoja za wawakilishi.
Mwakilishi wa Ziwani, Suleiman Makame Ali amesema kumekuwapo na ukataji miti ovyo huku akihoji ni kwa namna gani Seriklai inajipanga kuondoa tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wananchi wa hali ya chini kuepukana na matumzi ya nishati chafu.
Mwakilishi mwingine wa Chonga, Suleiman Masoud Makame amesema kuna uharibifu mkubwa wa ukataji wa miti na kusababisha uharibifu kwa kukosa elimu ya matumizi ya nishati safi.
Naye mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman ameuliza lini Serikali itaanza kutumia gesi kwenye magari kama inavyotumika Tanzania bara kupunguza uchafuzi wa mazingira unaosabaishwa na mafuta.
Akijibu sehemu ya hoja hizo, Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui amesema wizara ipo kwenye mchakato wa kuandaa mwongozo wa matumizi ya gesi na hivi karibuni utazinduliwa.
“Hili ni tatizo na wananchi wengi wanaathirika na matumizi ya nishati chafu kwa hiyo matumizi ya gesi ni muhimu na tupo kwenye mchakato kumalizia mwongozo wa matumizi ya gesi hivi karibuni tutauzindua,”amesema Waziri Mazrui.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema Serikali ipo kwenye mchakato kutafuta wawekezaji kufunga mitambo ya gesi kwa ajili ya magari.
“Serikali ipo kwenye mazungumzo na kampuni ya kutengeneza magari ya gesi na tunatarajia kumpa eneo kule Dunga Zuze Mkoa wa Kusini Unguja, ataweka mitambo pale kwa ajili ya kuunganisha gesi kwenye magari ili kulinda mazingira yetu,” amesema.
Amesema kupitia mradi wa mazingira wa Green Legacy elimu zaidi itatolewa kwa watumiaji wa nishati hizo ili kuacha utumiaji wa kuni na mkaa, jambo litakalosababisha wauzaji hao kukosa soko na kujishughulisha na shughuli nyingine kwa kutumia fursa zinazopatikana nchini.
Akisisitiza jambo hilo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema zinaandaliwa sera na sheria ambazo zitatoa mwongozo kwa ajili ya kubainisha maeneo maalumu ya kuuza gesi.
Amesema kwa sasa Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Zura), wanadhibiti bei katika uingizaji wa gesi nchini na hizo zote ni jitihada za Serikali kusaidia upatikanaji wa bei rafiki kwa wananchi.