Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar yaanza kukusanya takwimu za uwiano wa kijinsia

Mwenyekiti wa Baraza la Watu wenye ulemavu Zanzibar, Salma Saadat akizungumza wakati wa kuzindua mpango wa uiusanyaji wa takwimu za kijinsia katika nafasi za uamuzi ngazi ya chini hadi Taifa kwa taasisi za serikali, binafsi na asasi za kiraia Zanzibar

Muktasari:

  • Zanzibar imeweka mikakati madhubuti na shirikishi ya kukusanya na kuchambua takwimu za uwiano wa kijinsia katika nafasi za uongozi na maamuzi kuanzia ngazi ya jamii, taasisi hadi Taifa ili kukuza usawa wa kijinsia na ushiriki jumuishi.

Unguja. Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar, wameanza kuandaa na kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za kijinsia katika taasisi za Serikali, binafsi, asasi na mashirika mbalimbali kuanzia ngazi za chini hadi Taifa.

Hatua hiyo inalenga kupata takwimu katika taasisi hizo na kuangalia uwiano wa wanawake katika nafasi za uongozi, kwenye nafasi za uamuzi, jambo linalotajwa iwapo likifanikiwa, litaleta tija na kuongeza chachu ya kuwa na usawa kwenye nafasi hizo.

Kwa kipindi kirefu, wadau wamekuwa wakihamasisha ushiriki wa wanawake kushiriki katika nafasi za uamuzi, lakini hakukuwa na takwimu halisi zinazoonyesha kiwango cha ushiriki wao,  hivyo mpango huo unakwenda kutambua hilo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, kwa sasa hakuna takwimu halisi zinazoonyesha uwiano wa wanawake na wanaume, siyo tu katika taasisi za Serikali, bali hata kwenye mashirika binafsi, asasi na sekta binafsi.

Akizungumza wakati wa kuzindua mpango huo wa kukusanya takwimu hizo uliowakutanisha wadau kutoka taasisi za Serikali, binafsi na asasi za kiraia jana Julai 5, 2025, Mkuu wa Divisheni ya Jinsia na Ajira OCGS, Sabrina Raphael Daima, amesema kupatikana kwa takwimu hizo kutasaidia katika utungaji wa sheria na sera zinazoangazia masuala ya jinsia, hususan kwenye taasisi.

“OCGS imejipanga kuhakikisha kila mwaka inatoa takwimu hizi za kijinsia katika taasisi zote. Hata bajeti zetu zimeelekezwa zipangwe kwa kuangalia jinsia, kwa hiyo hiyo ni mipango inayosisitizwa,” amesema.

“Kwa hiyo, tunawezaje kuweka mipango ya bajeti ya usawa wa kijinsia bila kuwa na takwimu? Lazima kwanza tuweke mipango ya kuwa na takwimu hizi, na ndizo zitakazosaidia katika kupanga mipango ya maendeleo,” amesema Sabrina.

Naye Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Tamwa ZNZ, Mohamed Khatib Mohamed, amesema tangu kuanza kwa mradi wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi (SWILL), changamoto kubwa ilikuwa ni mifumo dume. Ingawa bado ipo, lakini kuna hatua zimefikiwa za mabadiliko.

“Changamoto kubwa hakuna takwimu, kwa hiyo, bila ya kuwapo takwimu za kiutafiti inakuwa shida kushughulikia tatizo hili. Baada ya kufanyika mpango huu wa ukusanyaji wa takwimu, utaonyesha uhalisia wa usawa wa kijinsia kwenye taasisi zetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Salma Saadat, amesema kuna mambo mengi yanayowarejesha nyuma wanawake katika kuingia kwenye usawa, ikiwa ni pamoja na uwezo mdogo wa kifedha na kutolewa lugha za kukatisha tamaa na kunyanyapaliwa.

Naye Mtakwimu kutoka Wizara ya Afya, Khamis Khamis, amesema kwa muda mrefu kulikuwa na pengo kubwa la kijinsia katika sekta mbalimbali.

“Taarifa hizi kwa muda mrefu hazikuwepo na mpaka sasa hazipo. Zipo za juu kabisa, lakini katika ngazi ya kati na chini huzipati. Utapata mawaziri, makatibu wakuu na wakurugenzi. Zikipatikana zitasaidia, maana tunataka tuwe na uwiano wa kijinsia, na zikipatikana zitasidia kutunga sera,” amesema.

Ofisa Programu kutoka Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu (Juwauza), Rehyani Khamis, amesema wanawake kwa kiasi kikubwa hawaingii kwenye uongozi, lakini kupitia mpango huo, wanategemea kuona wanawake wakiongezeka katika ushirikishwaji na masuala ya uongozi.

Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Abdallah Hussein Mgongo, amesema kuanzishwa kwa mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya chini hadi taifa ni jambo jema, litakalowezesha kuona namna gani wanapiga hatua za maendeleo.

“Ili kuboresha mfumo huu, maana yake elimu inahitajika zaidi kwa ngazi zote. Kuna haja hata ngazi za shehia wananchi wafikiwe.

“Baada ya muda mrefu sasa kuhamasisha wanawake washirikishwe, ni muda sasa kuona takwimu zinasemaje katika ushirikishwaji huo,” amesema.