Mafunzo ya askari wanyamapori Chuo cha Pasiansi yana manufaa makubwa kwa taifa


 Mafunzo ya askari wanyamapori Chuo cha Pasiansi yana manufaa makubwa kwa taifa

Kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi na ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori, Serikali ya Tanzania ilianzisha chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, kilichopo Jijini Mwanza mwaka 1966 ili kuzalisha askari wanyamapori wenye ujuzi na mbinu za kupambana na vitendo vya ujangili.

 Rasilimali ya wanyamapori ni miongoni mwa vyanzo muhimu katika kukuza pato la Taifa letu kutokana na kuwa kivutio kikubwa cha watalii. Takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonyesha kwamba sekta ya utalii inachangia katika pato la taifa kwa asilima 17.6 na ni moja ya sekta ambazo zinaliingizia taifa fedha za kigeni kwa asilima 25.

Mwaka 2017 pekee sekta ya utalii iliripotiwa kuingizia Serikali ya Tanzania kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 2.3. Kila mwaka nchi yetu hupokea wageni wengi na hivyo kuchangia katika kukusanya kiasi kikubwa cha fedha za kigeni ambazo hutumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Takwimu zinabainisha kwamba mwaka 2017 pekee Tanzania ilipokea jumla ya watalii milioni 1.3, idadi ambayo ina tofauti ndogo kwa upande wa Kenya ambayo ilipokea watalii milioni 1.4 kwa mwaka huo. Pamoja na kuwa rasilimali muhimu katika kukuza uchumi, bado wanyamapori na mazingira yao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazopelekea hata kutoweka kwao.

Ili kunusuru uhai wa viumbe hawa kwa faida yetu ya sasa na ya vizazi vijavyo, jitihada za pamoja ni jambo la lazima. Kutokana na umuhimu wa wanyamapori, duniani kote Machi 3 kila mwaka huadhimishwa kama “Siku ya Wanyamapori Duniani”. Kwa mwaka huu, kauli mbiu ya maadhimisho ni “Saidia kuendeleza uhai duniani” (Sustaining all life on earth).

Hii ni siku muhimu ya kuzitambua changamoto zinazowakabili wanyamapori na mazingira yao na kutafakari namna sahihi ya kuzikabili. Siku ya leo tunakumbushwa katika siku hii kupiga vita vitendo vya ujangili na shughuli nyingine za binadamu zinazoathiri maisha ya wanyamapori duniani.

Siku ya wanyamapori duniani ni matokeo ya kikao cha sita cha Bunge la Umoja wa Mataifa (Unga) cha mwaka 2013 kilichoitambua siku ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyopo hatarini kutoweka (Cites), uliopitishwa mwaka 1973 nchini Marekani, lengo la siku hiyo ni kuongeza uelewa wa watu juu ya faida lukuki zinazotokana na raIslimali ya wanyamapori.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa wanachama yaliyoridhia mkataba huu tangu mwaka 1979. Kama wadau wa uhifadhi tunapaswa kuitumia siku hii kujitathmini tulipo kiuhifadhi ili kuhakikisha ujangili unatokomezwa na maisha ya wanyamapori yanaendelea kushamiri kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika taarifa yake ya Juni 2017, Taasisi ya stadi za maendeleo ya nchini Uingereza (IDS) inayojishughulisha na masuala ya utafiti ilibainisha kwamba mchango wa sekta ya wanyamapori Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mwaka ulikuwa dola za Kimarekani bilioni 108 katika kipindi cha mwaka 2016 kiasi ambacho kinakadiriwa kuongezeka hadi kufikia dola bilioni 178.5 ifikapo mwaka 2027.

Fedha hizi ni matokeo ya safari za watalii pamoja na utalii kwa ujumla wake. Uvamizi wa makazi ya wanyamapori unaosababishwa na ongezeko kubwa la watu duniani kwa ajili ya shughuli za kilimo na makazi, biashara ya mazao yatokanayo na wanyamapori, ukataji ovyo misitu usiodhibitiwa, uingizaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwa ajili ya kupata malisho pamoja na ongezeko la umaskini ni miongoni mwa sababu kubwa ambazo zimekuwa zikitajwa na wanaharakati wa uhifadhi kuwa sababu zinazopelekea kupungua au kutoweka kwa bioanuai wakiwemo wanyamapori na mimea ya aina mbalimbali.

Mathalan kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2003 hadi 2018, Cites kupitia programu yake ya Mike yenye jukumu la kufuatilia mauaji ya tembo ilirekodi mizoga 19,000 ya tembo katika nchi mbalimbali barani Afrika. Taarifa za utafiti zinaonyesha pia wakati wa kongamano la nchi wanachama wa Cites lililofanyika nchini Thailand mwaka 2013, Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa mataifa manane zikiwemo pia nchi za Kenya, Uganda na China yanayoongoza kwa biashara haramu ya meno ya tembo duniani.

Watafiti wana wasiwasi kuhusu maisha ya wanyamapori siku za usoni hususan tembo ambao wanauawa sana na majangili. Mashirika ya WWF na IUCN yanaripoti kuwa bara la Afrika kwa sasa linakadiriwa kuwa na idadi ya tembo wapatao 415,000. Hata hivyo takwimu za mwaka 2017 kwa mujibu wa Cites na Vyuo Vikuu vya York (Uingereza) na Freiburg (Ujerumani) zinaonyesha kwamba takriban tembo 10,000 hadi 15,000 huuawa na majangili kila mwaka.

Taarifa zinabainisha kwamba, kukithiri kwa vitendo vya ujangili kumesababisha idadi ya tembo kupungua kwa asilimia 20% barani Afrika kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Kwa upande wa Afrika tembo amekuwa akitumika sana katika kupima hali ya uhifadhi katika nchi zenye tembo (keystone species). Hivyo, ujangili wa tembo unapopungua hali ya kiikolojia huwa nzuri.

Ujangili kwa ajili ya meno ya tembo ndiyo sababu kubwa ya kupungua kwa tembo duniani kote. Itakumbukwa tukio la biashara haramu ya meno ya tembo lililomhusisha mfanyabiashara wa kike wa Kichina Yang Fang Glan maarufu kama “Queen of Ivory” mwaka 2019 aliyetiwa hatiani na mahakama nchini Tanzania kwa kusafirisha meno 860 ya tembo kwenda barani Asia, idadi inayosemekana kutokana na tembo zaidi ya 350. Jitihada za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na vitendo vya ujangili ambavyo ni tishio kwa maisha ya wanyamapori.

Kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi na ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori, Serikali ya Tanzania ilianzisha chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, kilichopo Jijini Mwanza mwaka 1966 ili kuzalisha askari wanyamapori wenye ujuzi na mbinu za kupambana na vitendo vya ujangili.

Uanzishwaji wa chuo hiki unatajwa katika kifungu cha 96 (1) cha Sheria ya Wanyamapori namba 05 ya mwaka 2009. Takwimu za udahili zinaonyesha kwamba tangu kuanzishwa kwake miaka 53 iliyopita, chuo cha Wanymapori Pasiansi kimeweza kuzalisha wahitimu wapatao 5,702. Kwa sasa chuo kina uwezo wa kudahili wanachuo 400 kwa mwaka.

Ili kuendelea kudhibiti ubora wa mafunzo yatolewayo na chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, chuo hiki kilisajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Vyuo vya Ufundi (Nacte) mwaka 2002 na kupata Ithibati mwaka 2007 hadi sasa.

Chuo kimesajiliwa kutoa mafunzo katika ngazi ya 4 na 5 (National Technical Award level 4 and 5) kwa kozi za Usimamizi Wanyamapori na Himasheria (Wildlife Manage-ment and Law Enforcement). Chuo kina tekeleza Mpango Mkakati wake wa pili wa mwaka 2019/2020 hadi 203/2024, moja ya lengo kuu katika Mpango Mkakati huo ni kuboresha mafunzo na kupanua kozi zitolewazo na chuo ifikapo mwaka 2024.

Hivyo, kwa kushirikiana na wadau na ushauri wa Nacte, tayari chuo kimeandaa mitaala ya kozi mpya ya kuhusu Askari Mhifadhi Wanyamapori kuongoza watalii na usalama wao (Tour Guiding and Safety). Kozi hii mpya imeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuzalisha wataalam watakaokidhi matarajio ya watalii huku wakihakikisha usalama wao.

Kozi imepangwa kuanza kutolewa mwaka 2020/2021.Ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika tasnia ya wanyamapori, Serikali ilitoa tamko la kubadilishwa kwa mfumo wa taasisi zinazojihusisha na uhifadhi wanyamapori nchini kutoka mfumo wa kiraia na kufuata mfumo wa jeshi usu.

Tangu kuanzishwa kwake, Chuo cha Wanyamapori Pasiansi kilipewa jukumu la kuwandaa vijana Watanzania katika mfumo wa jeshi usu kwa kutoa mafunzo yenye weledi katika tasnia ya usimamizi wanyamapori. Kwa sasa Chuo kina kambi ya kudumu ya mafunzo kwa njia ya vitendo Fort Ikoma kwenye ukanda wa Ikolojia ya Serengeti.

Kambi hiyo ina miundombinu muhimu kama vile mabweni, madarasa na umeme. Nafasi ya Chuo cha Wanyamapori Pasiansi katika kusimamia rasilimali ya wanyamapori ni kuhakikisha inazalisha askari wahifadhi wanyamapori waadilifu na wenye ujuzi wa kutosha katika kukabiliana na vitendo vya ujangili. Ni wahitimu ambao wapo tayari kutekeleza majukumu yao kwa kusimamia sheria za wanyamapori ipasavyo na pia kuwa karibu na wananchi kwa kuwapatia elimu na hivyo kuwafanya kuwa sehemu ya uhifadhi badala ya kutumika kama chanzo cha ujangili.

Kwa msingi huo, Chuo cha Wanyamapori Pasiansi kinatekeleza madhumini ya Siku ya Wanyamapori Duniani kwa vitendo jukumu ambalo linakwenda sambamba na kutambua Malengo ya Maendeleo Endelevu yanayoazimia kukabiliana na tatizo la ongezeko la umaskini katika jamii, kuwa na matumizi sahihi ya maliasili zetu na kuhakikisha wanyamapori na mazingira yao wanaendelea kuwa salama kwa manufaa ya watanzania wote.

Wahitimu wa chuo hiki, wengi wao wamekuwa wakiajiriwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa), Halmashauri za Wilaya nchini na katika taasisi binafsi zinazojihusisha na uongozaji wa watalii.

Licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, askari wanyamapori wanatazamwa kama kundi la kawaida sana. Baadhi ya askari wanyamapori wamekuwa wakiripotiwa kupoteza maisha yao wakati wakilinda rasilimali za nchi.

Aidha kwa kushambuliwa na wanyamapori wakali au kwa kuuawa na majangili, mbali na changamoto hiyo tunashuhudia idadi ya watalii inayosababishwa na uwajibikaji wa askari hawa ikizidi kuimarika. Mafanikio haya tunaweza kuyapima kutokana na kuongzeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi zetu, kupatiwa huduma nzuri na kuhakikishiwa usalama wao.

Kuwepo kwa shauku kubwa ya Serikali ya kuwa na taifa lenye uchumi wa viwanda ni wazi kwamba suala la kuzalisha askari wanyamapori wa kutosha litabaki kuwa suala lenye umuhimu wa kipekee. Katika mtazamo huo tutakubaliana kwamba suala la kuwa na vyuo bora kwa ajili ya kuwandaa askari wanyamapori wenye mafunzo na ujuzi stahiki nchini linapaswa kupewa kipaumbele.

Bila kuwa na nguvu kazi ya kutosha hatuwezi kuyafikia malengo ya uchumi wa viwanda. Ongezeko la umaskini na mahitaji ya mazao yatokanayo na wanyamapori katika mataifa kadhaa ya Asia kumekuwa kichocheo cha kukithiri kwa wimbi la ujangili barani Afrika.

Kwa taswira ilivyo hivi sasa ipo tofauti ya kimasilahi miongoni mwa askari wahifadhi wanyamapori wanaofanya kazi katika mashirika/taasisi za uhifadhi nchini, wapo askari wanaolipwa kidogo kulinganisha na askari wengine.

Ni wazi kwamba mazingira ya kazi kwa askari wahifadhi wanyamapori (bila kuangalia tofauti za kisera za waajiri) ni magumu na hatarishi, hivyo suala la kulipwa sawa na kuboreshewa mazingira ya kazi kwa ujumla ni la muhimu badala ya kutofautishwa kimaslahi.

Kwa sasa askari hawa wana imani na mfumo wa jeshi usu uliotangazwa rasmi na Serikali mwaka jana katika Hifadhi ya Taifa Serengeti. Wanaamini kwamba mfumo wa jeshi usu itakuwa njia sahihi ya kuondoa kasoro za kimasilahi zilizopo miongoni mwao, kuwaongezea mbinu bora za kijeshi katika kukabiliana na uharifu wa ujangili na hivyo kuwa kichocheo cha kuwatia moyo na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya uhifadhi tofauti na ilivyo sasa.

Mbali na kuwepo kwa kozi za muda mrefu, Chuo cha Wanyamapori Pasiansi kinatoa pia mafunzo ya muda mfupi kwa wale wanaotoka katika mifumo ya kiraia na pia mafunzo maalumu kwa watumishi wanaotoka katika sekta za jeshi usu. Chuo kimekuwa kikipokea pia wanafunzi kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile “Carbon Tanzania”, “Tuungane Program” na Hifadhi Mazingira Karatu (Himaka).

Mfunzo ya muda mfupi hutolewa kuanzia wiki mbili hadi miezi sita. Elimu juu ya tabia za wanyamapori huwasaidia wahitimu wa chuo hiki kufanya kazi zao kwa ujasiri bila kuwa na hofu ya kushambuliwa na wanyama wakali. Kwa kufahamu tabia za wanyamapori, humsaidia askari kufahamu shughuli na mahitaji mbalimbali ya wanyama na mahali walipo kwa nyakati tofauti tofauti.

Hii ni muhimu wakati wa kupanga doria ili kuwa rahisi kuyakabili maeneo yanayoweza kuvamiwa na majangili katika vipindi mbalimbali vya mwaka na pia kuwa rahisi kufuatilia na kukabiliana na tatizo la migogoro baina ya wanyamapori na binadamu.

Ili kuendelea kutoa mafunzo ipasvyo, Chuo cha Wanyamapori Pasiansi bado kinahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa uhifadhi ili kuboresha mazingira yake ya ufundishaji. Aidha waajiri nchini ni vizuri wakitoa fursa ya ajira kwa wahitimu wa Chuo cha Wanyamapori Pasiansi kwa kuwa wameandaliwa kikamilifu, kwa kufuata misingi ya uzalendo, uvu-milivu, uadilifu na ujuzi wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao ya uhifadhi.

Pia, kwa kila Mtanzania “Siku ya Wanyamapori Duniani” tuitumie kama chachu ya kutambua faida za wanyamapori katika taifa letu. Tunao wajibu wa kuwahifadhi, kuwatunza na kulinda mazingira ya wanyamapori. Aidha, ni jambo la muhimu pia tutambue dhamana waliyonayo askari wanyamapori katika kulinda rasilimali ya wanyamapori na mazingira yao. Tunapaswa kuwapatia ushirikiano askari wanyamapori kwa kuwapatia taarifa za wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili ili kuhakikisha uhai wa wanyamapori unaendelea kuwepo kwa faida ya taifa letu.