Mchango wa utafiti wa kahawa katika uzalishaji na ubora wa kahawa Tanzania

Muktasari:

Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) ni taasisi inayomilikiwa na kusimamiwa na wadau wa kahawa (ikiwa ni pamoja na Serikali) kwa lengo kubwa la kuchangia kuboresha tasnia ya kahawa Tanzania kwa kuweka mkazo katika dhima ya wadau wa kahawa kwamba “Utafiti ndio uhai wa wakulima wa kahawa.”

Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) ni taasisi inayomilikiwa na kusimamiwa na wadau wa kahawa (ikiwa ni pamoja na Serikali) kwa lengo kubwa la kuchangia kuboresha tasnia ya kahawa Tanzania kwa kuweka mkazo katika dhima ya wadau wa kahawa kwamba “Utafiti ndio uhai wa wakulima wa kahawa.”

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TaCRI, Dk Deusdedit Kilambo anasema lengo la TaCRI ni kuwa na tasnia ndogo ya kahawa yenye faida na endelevu Tanzania na kuhakikisha kuwa teknolojia muafaka za kulima kahawa zinapatikana na kusambazwa ili:

• Kuongeza tija,

• Kuongeza ubora,

• Kupunguza gharama za uzalishaji,

• Kuongeza ushindani wa kahawa ya Tanzania kwenye soko la dunia,

• Kuongeza kipato na riziki kwa wakulima wa kahawa,

• Kuongeza mchango wa kahawa kwenye pato la taifa.

Dk. Kilambo anasema, katika kufanikisha malengo yaliyoainishwa, TaCRI inatekeleza mikakati ifuatayo:-

Mikakati ya kufufua sekta ya kahawa Tanzania

Mkakati wa muda mfupi

• Kukarabati mibuni ya zamani kwa kulengeta na kuzingatia Amri 8 za kuongeza tija

• Kukarabati mibuni ya zamani ni lazima kuende sambamba na kukarabati mashamba kwa ujumla na kuzingatia kanuni za kilimo bora cha kahawa.

Mkakati wa kudumu

Kuongeza ubora wa kahawa kwa kuzingatia amri 10 za kuongeza ubora na hasa kuhamasisha wakulima kukoboa kahawa katika ngazi ya kijiji au kaya.

Mkakati wa muda mrefu

Kubadilisha mibuni yote inayoathiriwa na magonjwa wa mnyauko fuzari, chulebuni na kutu ya majani na kupanda aina mpya bora za Arabika na Robusta zinazohimili magonjwa.

TaCRI katika kutekeleza mikakati ya kuendeleza zao la kahawa

“TaCRI imekuwa ikifanya kazi kwa kufuata mikakati ya utekelezaji ya miaka mitano mitano – 5 years strategic action plans (SAPs). Mikakati hii imekuwa ikiandaliwa na wataalamu washauri (Consultants) kwa kutumia njia shirikishi na hasa kwa kushirikisha wadau wa kahawa katika ngazi mbalimbali,” anasema Dk. Kilambo.

“Hadi sasa tumeshatekeleza mikakati mitatu (2003-2007/8; 2008/9-2012/13 na 2013/14 - 2017/18) na sasa tunaendelea kutekeleza mkakati wa nne 2018/19-2022/23). Mikakati yote inalenga kutatua changamoto za zao la kahawa na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za wadau wa kahawa Tanzania,” anasema Dk Kilambo.

Programu za utafiti katika kue-ndeleza zao la kahawa

Dk. Kilambo anasema tuna programu nne za utafiti ambazo zinafanya kazi ya kutatua changamoto ziliko kwenye tasnia ya kahawa kama ifuatavyo:

  1. Programu ya kuendeleza zao la kahawa (Coffee improvement programme)

Inahusika na kufanya utafiti wa kuendeleza zao la kahawa. Kupitia programu hii, TaCRI imetoa aina19 bora za kahawa aina ya Arabika na 4 aina ya Robusta ambazo hazishambuiwi na magonjwa ya chulebuni (CBD) na kutu ya majani (Coffee Leaf Rust) kwa upande wa Arabika; na mnyauko fuzari (CWD) kwa upande wa Robusta, zina ladha au muonjo wa hali ya juu kama aina za zamani au hata zaidi, zina tija ya hali ya juu (hata zaidi ya maradufu ya aina za zamani) na humpunguzia mkulima gharama za uzalishaji kwa asilimia 30-50% na hivyo kumuongezea kipato. Aina hizi mpya ni mafanikio ya kipekee kwani ni mkombozi na chimbuko kubwa la mapinduzi ya kijani na ndizo zitakazo changia katika kuongeza uzalishaji, kuongeza ubora, kumuongezea mkulima kipato.

Pia, TaCRI imetafiti na kupendekeza teknolojia muafaka za kuzalisha miche ya aina bora chotara ambazo ni

(1) Kuzalisha miche kwa njia ya vikonyo (clonal propagation),

(2) Kupachikiza (Grafting),

(3) Kuzalisha mbegu chotara (F1 hybrid seeds) na

(4) Kuzalisha miche kwa njia ya chupa (tissue culture au somatic embryogenesis).

 

  1. Programu ya uogezaji tija na uboreshaji wa zao la kahawa (Coffee productivity and quality improvement programme)

Kupitia programu ya uogezaji tija na uboreshaji wa zao la kahawa, TaCRI imekwisha ainisha teknolojia sahihi zinazotekelezeka za kuongeza tija na ubora. Tija kwa mti na kwa eneo ni muhimu sana ili kumuongezea mkulima kipato.

Tayari tunazo teknolojia za kuongeza tija kama vile amri nane ambazo zinajumuisha matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu na wakulima wengi wamesha pokea teknolojia hizi na mashamba mengi yamekarabatiwa na tija imeongezeka.

Ubora wa kahawa ni muhimu sana ili tuweze kupata bei nzuri kwenye soko la dunia hivyo basi ni muhimu kuzingatiwa. Tunazo teknolojia za kuongeza ubora kama vile amri kumi ambazo mkulima akizifuata atazalisha kahawa yenye ubora wa hali ya juu na hivyo kupata bei nzuri kwenye soko kwani bei nzuri ipo kwa kahawa iliyo na ubora wa hali ya juu.

Maabara ya kisasa iliyoko kwenye pro-gramu hii imekuwa ni msaada mkubwa kwa kufanya uchan-ganuzi wa udongo na mimea na kutoa ushauri unaofaa katika kuongeza tija ya zao la kahawa.

  1. Programu kabambe ya usambazaji wa teknolojia na mafunzo (Technology transfer, advocacy and training)

Kupitia programu ya usambazaji wa teknolojia na mafunzo, tunao mkakati wa kuwezesha wakulima na wadau wengine kwa kutoa mafunzo kwa kutumia njia shirikishi (participatory village based training) na kuweka mkazo kwenye vikundi na mafunzo kwa wafundishaji (training of trainers).

Njia hii shirikishi ya kuweze-sha wadau kupitia mtandao wa vikundi imeonyesha mafanikio makubwa sana katika kusambaza teknolojia. Vilevile taasisi imebuni njia ya kutumia wakulima wahamasishaji (farmer promoters) katika kusambaza teknolojia.

Njia hii ambapo mkulima baada ya kufundishwa na wataalamu huchukua jukumu la kuwafundisha wakulima wenzake, imeonyesha mafanikio makubwa sana na mahitaji ya teknolojia yamekuwa makubwa kwenye maeneo ambayo wakulima wahamasishaji wanafanyakazi za ugani. Kupitia programu ya usambazaji teknolojia.

Tumeanzisha mtandao wa vituo vidogo kwenye kila kanda (TaCRI substations), ili huduma za kitafiti ziweze kuwafikia wadau wengi kawa haraka zaidi, TaCRI ina vituo vidogo vya utafiti vilivyoko kwenye kanda zinazolima kahawa kama ifuatavyo: Lyamungu, Moshi; Ugano Mbinga Ruvuma; Mbimba Mbozi Songwe; Maruku Bukoba Kagera; Mwayaya Buhigwe Kigoma na Sirari Tarime Mara. Vituo vidogo vimekuwa vyenye mafanikio makubwa sana katika kusambaza teknolojia.

  1. Riziki na uhakika wa kipato cha mkulima (Livelihoods and income security)

Programu inahusika na kuelezea uchambuzi wa mifumo mbalimbali na riziki katika maeneo yanayozalisha kahawa nchini. Pia, kuweka vipaumbele katika vikwazo vinavyoathri kuongeza tija na faida na kupendekeza suluhisho la nini kifanyike.

Baadhi ya mafanikio katika kufufua tasnia ya kahawa mpaka sasa

Dk Kilambo anaeleza kuwa, taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), imeendelea na mkakati wake wa kuanisha teknolojia zitakazochan-gia katika kuongeza tija na ubora wa kahawa na kupun-guza gharama za uzalishaji ili kuboresha kipato kwa waku-lima na tumepata mafanikio yafuatayo:

Taasisi imeendelea kutafiti aina za kahawa zenye tija kubwa zaidi, ukinzani kwa magonjwa na ubora unaokubalika na soko la ndani na nje ya Tanzania.

Aina 38 za Arabika zina-fanyiwa utafiti, ambapo aina sita (6) zinaonyesha uwezo mkubwa wa ukinzani kwa magonjwa, tija kubwa zaidi ya tani mbili kwa hekta na mwonjo unaokubalika na soko la ndani na nje ya nchi.

Utafiti wa kuzalisha mbegu chotara (hybrid seed production) umekamilika, lengo ni kuzalisha tani 2 (sawa na miche milioni 8) kuanzia mwaka 2019/20. Njia hii ikiweza kufanya kazi itaweza kuharakisha uzalishaji wa miche aina bora!

Kilo moja ikioteshwa na kutunzwa vizuri huweza kuzalisha miche 4,000.TaCRI imefungasha na kusambaza vipeperushi (leaf-lets) 185,707 juu ya kilimo bora cha kahawa.

Vipeperushi kuhusu changamoto mpya kama vile jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wadudu waharibifu wanaotoboa matunda na matawi ya kahawa vinahitajika na vinatayarishwa na Taasisi.

TaCRI imetoa vitabu vipya: Kanuni Bora za Kilimo cha Arabika (toleo lililoboreshwa), na pia Kanuni Bora za Kilimo cha Robusta (toleo jipya) na Mtaala wa Mafunzo ya Kilimo Bora cha Kahawa kwa Lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Vitabu hivi na mtaala uliotolewa utasaidia sana katika mafunzo ya wagani na wakulima wa kahawa.

“Taasisi imeendelea kutekeleza kwa kasi zaidi Ilani ya CCM kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, ambayo pamoja na maelekezo mengine, aya ya 22, (d), (i), inalezea kwamba CCM inaitaka Serikali, kuboresha mfumo wa utafiti ili uweze kugundua na kutathmini aina bora za mazao mbalimbali zenye sifa ya kutoa mavuno mengi na zinazostahimili mabadiliko ya tabia nchi,” anasema Dk Kilambo.

Anasema, TaCRI imetekeleza azma hii kwa kutoa aina bora za kahawa zenye ukinzani kwa magonjwa, tija kubwa na ubora unaokubalika na soko la ndani nan je ya nchi.

Tunashukuru kwa mwongozo tunaopata kupitia Waziri wetu wa Kilimo Mheshimiwa Japhet Hasunga (MB), pia Manaibu wake Waheshimiwa Omari Mgumba (MB) na Hussein Bashe (MB).

Pia Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wa Wizara. Tunashukuru pia kwa Bodi ya Kahawa kwa Ushirikiano mzuri.