Ushirikiano kwa vitendo: Umoja wa Ulaya Tanzania unaadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza umaskini

Muktasari:

Umoja wa Ulaya (EU) unaunga mkono kikamilifu ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika wenye ujasiri na unaolenga kujenga mustakabali wa pamoja na wa angavu kwa watu wote.

Leo, tarehe 17 Oktoba 2020 ni Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Umaskini. Siku hii ni ukumbusho mzuri wa malengo makubwa yanayoongoza kazi zetu: kusaidia watu kujinasua kutoka kwenye mzigo wa umaskini uliokithiri na kuishi maisha ya heshima.Utokomezaji wa umaskini ni muhimu katika kuwa na jamii yenye amani na umoja.

Kutokomeza umaskini ni lengo kuu la ajenda ya mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu, ambayo Umoja wa Ulaya (EU) unaunga sana mkono. Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni mshirika wa muda mrefu wa Tanzania. Tunafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau wengine katika utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini.Tuna matumaini.

Tathmini ya Umaskini Tanzania Bara ya mwaka 2019 inabainisha kuwa umasikini umepungua kwa asilimia nane ndani ya miaka 10 iliyopita, kutoka asilimia 34.4 mwaka 2007 hadi asilimia 26.4 mwaka 2018.

Kuhamasisha maendeleo ya jamii bila kumuacha mtu yeyote nyuma

Umaskini una sababu kuu na huathiri watu kwa njia nyingi. Kwa hivyo, lazima tuwe na mtazamo jumuishi unaozingatia jamii nzima. Hii ni pamoja na sheria ambayo uahidi kutoa kipato cha kima cha chini, elimu ambayo huondoa vizazi vijavyo kutoka kwenye mzunguko wa umaskini, na mifumo ya afya inayowafikia watu wote, kutaja vitu vichache.Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na nchi wanachama hufanya kazi pamoja kama #TeamEurope, wakitumia sera na malengo ya pamoja katika kuchangia maendeleo endelevu ya Tanzania. Tukichukua hatua ili kufikia ahadi ya ajenda hii ya Maendeleo Endelevu, tutajenga kwa pamoja dunia ambayo ndani yake hakuna mtoto atakayekua katika umaskini uliokithiri.

Wakulima wadogowadogo vijijini watapata urahisi wa kufikia masoko na mikopo ili waweze kukuza biashara zao na kusaidia familia zao. Watoto maskini ambao hapo awali walitengwa katika jamii wataweza kupata kitambulisho cha kisheria na kupata huduma za kijamii na za kiuchumi. Wasichana wataepuka athari zinazosababishwa na ndoa za utotoni na ukeketaji. Nchi kama Tanzania zitaweza kupanua uchumi wao na viwanda kwa njia zilizo safi na endelevu.

Kuelekea katika Mkakati wa Afrika, Kamisheni ya Ulaya hivi karibuni imetangaza “Ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya kwa Uwekezaji Endelevu na Ajira” mpya. Mkakati huu unaendeleza ahadi za kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na EU na utasababisha kutengenezwa kwa ajira hadi milioni 10 barani Afrika katika miaka mitano ijayo pekee.

Mpango wa Uwekezaji wa Nje wa Ulaya ni jiwe la msingi la muungano huu mpya. Unalenga kuhamasisha uwekezaji barani Afrika kwa kuchochea uwekezaji mwingi zaidi wa umma na wa kibinafsi.Vipaumbele vya Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania ni pamoja na utawala bora na maendeleo, kilimo na nishati. Utawala bora na maendeleo kuzingatia masuala ya msingi ambayo ni ya muhimu zaidi kuisukuma Tanzania katika mchakato wake wa mabadiliko.

Ruzuku zimetolewa kwa miradi ambayo inalenga ukuaji wa uchumi wenye manufaa kwa watu maskini ili kutekeleza mazungumzo jumuishi juu ya utawala wa kiuchumi na wa kifedha nchini Tanzania.Ili kutokomeza umaskini na njaa kali, sekta ya kilimo ina jukumu muhimu la kutekeleza.

Ina uwezo wa kukuza na kutengeneza ajira katika mifumo ya chakula. Kwa hiyo, Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania unasaidia mikakati kadhaa chini ya mipango mbalimbali. Kwa mfano, mpango wa AGRI-CONNECT unakuza uzalishaji na ushindani wa sekta ya kilimo kwa kulenga baadhi ya mazao maalum, wakati Programu ya Kuboresha Ufikiaji wa Soko la EU-EAC inasaidia biashara ndogo na za kati kuboresha ubora wa bidhaa zao kwa kuzilinganisha na viwango vya kimataifa na kuwezesha bidhaa zao kuuzika kwa usalama.

Miradi ya nishati ambayo husaidia upatikanaji wa umeme, haswa katika maeneo ya vijijini, ambayo inakuza nishati mbadala na matumizi bora ya nishati, inakusudia kujumuisha kaya zote. Miongoni mwa miradi mingine, hii ni pamoja na mradi wa uzalishaji na usambazaji wa umeme katika kata ya Ikondo, Njombe ambao unakusudia kukuza maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi huko Ikondo kwa kutoa huduma za kisasa za nishati; na mradi wa usimamizi wa maji katika Ziwa Victoria ambao umebadilisha jamii zinazozunguka ziwa hilo, ikiwemo wakazi 250,000 katika mkoa wa Mwanza wanaofaidika na kuboreshwa kwa maji na usafi wa mazingira.Kwa mwaka 2020, Ulaya na Afrika wameweka ajenda kubwa ya kujenga ushirikiano wenye nguvu zaidi kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Afrika. Janga la Covid-19 linaloendelea limedhihirisha zaidi umuhimu wa jambo hilo na kwamba tunahitaji kuchukua hatua pamoja, kuwa na mshikamano pamoja na uelewa ili kukabiliana na changamoto hii ya ulimwengu.

Umoja wa Ulaya (EU) unaunga mkono kikamilifu ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika wenye ujasiri na unaolenga kujenga mustakabali wa pamoja na wa angavu kwa watu wote. Nina hakika inawezekana kuondoa umaskini uliokithiri ulimwenguni ndani ya kizazi chetu. Umoja wa Ulaya (EU) unaendelea kujitolea kuhakikisha tunafanya kila linalowezekana kufikia lengo hili kubwa.

Mhe. Balozi Manfredo Fanti Ujumbe wa EU kwa Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)