Mtanzania aacha mshahara wa Sh400 milioni Marekani

Benjamin Fernandes, aliposhinda tuzo ya kimataifa ya wanafunzi wa Biashara na Uchumi, alipokuwa Chuo Kikuu cha Stanford cha nchini  Marekani. Picha ya Mtandao

Muktasari:

DONDOO

Ni Mwafrika wa kwanza mwenye umri mdogo na Mtanzania wa kwanza kukubaliwa kusoma Shule ya Biashara ya Stanford Graduate School ya Marekani.

Ni sehemu ya klabu ya Waafrika iliyokuwa inafanyia kazi mradi wa teknolojia ya fedha ambao ulikuwa uanzishwe Tanzania.

Januari mwaka jana, aliteuliwa na jarida la TRUE Africa kuwa mmoja wa Waafrika 16 wanaoongoza mabadiliko.

Muda mfupi baadaye, kampuni ya usafiri wa anga ya FastJet ikatumia kazi zake kwenye jarida lake. Katikati ya mwaka jana, alitokea katika vipindi kadhaa vya televisheni vilivyorushwa moja kwa moja kama CNBC ya Marekani.

Dar es Salaam.  Kwa uamuzi huu, huwezi kuhoji kiwango cha uzalendo cha Benjamin Fernandes, Mtanzania wa kwanza kuhitimu shahada ya uzamili Chuo Kikuu cha Biashara Stanford nchini Marekani.

Fernandes, ambaye awali alikuwa mtangazaji wa televisheni, ameeleza siri ya kukataa mshahara wa Sh425 milioni kwa mwaka na  badala yake kurudi Tanzania kujenga Taifa.

Baada ya kumaliza masomo yake Marekani, Fernandes alikuwa akifanya kazi katika taasisi ya tajiri namba moja duniani, Bill Gates iitwayo Bill and Melinda Gates Foundation. Sasa ameamua kuacha kazi yenye mshahara mnono na kurejea nchini kusaidia vijana.

Fernandes pia alikuwa akikaa meza moja na mmiliki wa mtandao wa Facebook, Mark Zuckerberg alipokuwa akifanya kazi katika taasisi hiyo ya familia ya Gates.

Akihojiwa na televisheni ya Millard Ayo, Fernandes alisema kampuni mbalimbali Marekani zinamtafuta kwa ajili ya kwenda kufanya kazi kwa ahadi ya mshahara mnono, lakini amekataa kwa kuwa anataka kuwasaidia Watanzania.

“Watu wengi wananiuliza kwanini nimerudi nyumbani. Ni kweli nilikuwa napewa offer (dau) ya Sh425 milioni kufanya kazi kampuni mbalimbali Marekani, lakini huwa nilikuwa nawaambia nimesharudi nyumbani. Mimi motivation (motisha) yangu si hela ila upendo kwa nchi yangu,” alisema Fernandes.

Alisema alifikia uamuzi huo akijua kuna changamoto atakazokutana nazo.

Alisema ana mpango wa kuwatengenezea njia vijana ili elimu yao iwe msaada kwa jamii.

“Nasikitika watu wananipigia simu wananimbia nina vyeti hivi na hivi, mimi sijali sana elimu yako. Kapige kazi kwa bidii na hiyo kazi itakuheshimu,” alisema Fernandes.

Alieleza asilimia 70 ya watu  ni vijana wenye umri chini ya miaka 25 ambao wanatakiwa kuwa na  mchango katika maendeleo.

Fernandes alisema anataka kuonyesha jinsi teknolojia inavyoweza kuwa msaada kwa kutumia simu za kisasa zinazotumiwa na watu takribani 11.5 milioni nchini.

Aliiomba Serikali kusaidia vijana ili wawe chachu kwa ajili ya mafanikio ya wengine.

“Vijana wanatakiwa watamani kuwa mtu fulani, jambo ambalo linasaidia watoto kukua  na kutimiza ndoto zao,” alisema.

Fernandes alisema endapo atakutana na Rais John Magufuli, atakuwa na mengi ya kumwambia  hasa maendeleo ya Taifa.

“Kwa mfano, nitamshauri Rais kuimarisha mahusiano mazuri na sekta binafsi, biashara na Serikali kuzingatia sheria ili kukuza uchumi na kufanya biashara kuwa nyingi nchini.

Alisema teknolojia bado haijapewa kipaumbele ili kusaidia wanaoishi vijijini na kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu kwa watoto wadogo walio na umri chini ya miaka 10 wanaoweza kuwa chachu ya maendeleo.

“Kitu cha nne ningeshauri Serikali iwasikilize wawekezaji wa nje ili sisi kama nchi tufaidike. Kingine ni nidhamu ambayo Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inazingatiwa hivyo ahakikishe vijana wanakuwa na nidhami,” alisema Fernandes.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Hamis Mwinyimvua alisema ni jambo zuri kwa Watanzania wanaosoma nje ya nchi kurudi na kuleta ujuzi wao nchini.

“Kama amejisomesha kwa fedha zake, anaweza kurudi au kuamua kubaki, lakini kikubwa anaweza kufanya kama wafanyavyo diaspora (wazawa wanaoishi nje), fedha wanazopata zinatumwa Tanzania na zinatumika kwa maendeleo,” alisema.