CUF watunishiana misuli kumng’oa Lipumba

Mkurugenzi wa habari na uhusiano kwa Umma wa CUF, Abdul Kambaya akisisitiza jambo wakati wa mkutano na  waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni mkuu wa kitengo cha fedha na uchumi, Thomas Malima. Picha na Said Khamis

Muktasari:

“Wasiangaike na Chadema, wao ndiyo waliovamia ofisi kwa nguvu kinyume cha taratibu.Naomba wanaCUF wasibabaishwe na maneno ya Kambaya.” 

Salim Bimani

Dar es Salaam. Hofu ya kumng’oa Profesa Ibrahim Lipumba kutoka ofisi za makao makuu ya CUF zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam inazidi kutanda.

Profesa Lipumba aliingia katika mgogoro na chama hicho baada ya kufuta barua ya kujiuzulu uenyekiti mwaka mmoja baada ya kujivua uongozi na kwenda nje ya nchi kwa mapumziko.

Mkutano Mkuu haukukubaliana na kitendo hicho na badala yake ukakubaliana na barua yake ya kujiuzulu, lakini Msajili wa Vyama vya Siasa ameweka msimamo kuwa anamtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti.

Profesa Lipumba alirejea ofisi za CUF zilizopo Buguruni, wakati katibu mkuu wa chama hicho, Maalimu Seif Sharif Hamad akiendesha shughuli za chama kisiwani Unguja ambako ndiko makao makuu.

Kikundi kinachomuunga mkono Profesa Lipumba kinadai kuna vijana ambao wanajiandaa kuvamia ofisi ya Buguruni ili kumtoa mwenyekiti huyo, wakati upande wa Maalim Seif umesisitiza ni lazima Profesa Lipumba aondolewe.

Mkurugenzi wa habari, uenezi na mahusiano kwa Umma, Abdul Kambaya aliwaambia wanahabari kwamba kundi hilo la vijana linatoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mara na Dar es Salaam.

Alidai kuwa kundi hilo linagharimiwa malazi na chakula na kiongozi mmoja wa chama cha  upinzani na kwamba wanashirikiana na genge la Maalim Seif, Nassor Mazrui, Ismail Jussa na Julius Mtatiro ambao alidai hawana uhalali wa kuiongoza CUF.

“Taarifa za uhakika zinatueleza wakati wowote kuanzia leo (jana) mpango huu utatekelezwa. Kwa sauti isiyo ya shaka tunatoa angalizo kwa wote waliojiandaa kutimiza lengo hili wakishirikiana na Chadema,” alisema Kambaya.

Kambaya alidai kuwa kundi hilo litavalishwa nguo na bendera za CUF na litakusanyika na kuelekea katika kikao cha mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea kisha kuelekea kuvamia ofisi hizo kwa kutumia malori.

“Katika kikao hicho, Mtolea amewaalika wabunge mbalimbali wa Chadema ili kushiriki na kujadili masuala ya CUF. Tunajua Mtolea ana haki ya kufanya kikao lakini tunamwambia kama anafanya kikao ajadili maendeleo ya jimbo lake  na si kujadili mgogoro wa CUF kwa  sababu yeye si kiongozi,” alisema Kambaya.

Alidai kuwa kikao hicho pia kitahudhuriwa na wabunge wa Chadema wakiongozwa na meya wa Ubungo, Boniface Jacob.

Akizungumzia kauli hiyo, Mtolea alisema Kambaya anahangaika na hajitambui na kwamba, yeye ni kiongozi wa wananchi.

“Ni kweli Jumapili (kesho) nina kikao cha ndani katika jimbo langu. Niwaalika wadau mbalimbali wakiwamo wanachama wa CUF ambao ni wadau wangu muhimu,” alisema.

“Mtu hawezi kunipangia ajenda za kuzungumza, kwa sababu mimi ni mbunge nafanya kazi zangu kibunge zaidi. Hakuna mbunge wa Chadema niliyemwalika kama anabisha Kambaya aje kuhudhuria hata wewe (mwandishi) nakualika.”

Hata hivyo, Kambaya alisema tayari wametoa taarifa polisi kuhusu kuwapo kwa kikundi hicho, lakini kamanda wa polisi wa Ilala,Salum Hamduni alisema bado hawajapa taarifa rasmi kutoka CUF hizo.

Naye Jacob alisema  ikitokea CUF upande wa Maalim Seif inataka msaada yupo tayari kusaidia.