Mtoto aliyetekwa kimafia Dar afikisha siku 60, akosa mitihani

Muktasari:

Tayari siku 60 zimepita huku mtoto Idriss Ally (13) aliyetekwa kimafia akiwa hajapatikana jambo ambalo linaendelea kuwatia huzuni wazazi na wanafunzi wenzake ambao baadhi yao walihoji kama angeweza kufanya mitihani ya kumaliza mwaka.

Dar es Salaam. Idrissa Ally (13), mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Princes Gate jijini Dar es Salaam hadi jana mchana alikuwa ametimiza siku 60 tangu alipotekwa kwa staili ya ‘kimafia’ akiwa anacheza na wenzake na kumfanya akose mitihani ya mwisho wa mwaka.

Wakati mwalimu mkuu wa shule hiyo, Mussa Idrissa akisema mitihani ilianza Novemba 19 kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, pili, tatu, tano na sita, Ally Idd, baba mzazi wa Idrissa amesema wanaendelea na maombi ili mwanaye arudi salama.

Idrissa alitekwa Septemba 26 saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti wilayani Kinondoni.

Alichukuliwa na dereva mwanaume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST, ambaye alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo na kumuingiza mlango wa nyuma wa gari na kuondoka naye.

“Bado Idrissa anakumbukwa na wanafunzi wenzake, nakumbuka wakati tunawatangazia kuanza kwa mitihani hii, mmoja wa wanafunzi anayeitwa Amran alimuuliza mwalimu wake wa darasa kama Idrissa atakuja kufanya mtihani,” alisema Mussa.

“Mwalimu akamjibu kuwa Idrissa atafanya mitihani kama kawaida.”

Mwalimu Mussa alisema mitihani inatarajiwa kumalizika kesho na kwamba Idrissa amekosa kufanya mitihani ya Hisabati, Kiswahili, Haiba ya Michezo, Kiingereza na Uraia.

Alisema baada ya kukamilika kwa mitihani hiyo, wanafunzi hao watafanya marudio ya masomo yao kisha kufunga shule Desemba 7 na kufungua Januari 7, mwakani.

“Bado tunazidi kumuomba Mungu ili mwanafunzi huyu (Idrissa) arudi shuleni na kurejesha amani katika familia yake. Ni changamoto kubwa kwa sababu hatujui yuko wapi na kina nani wamemchukua,” alisema mwalimu huyo.

Kwa nyakati tofauti Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekuwa akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio la kutekwa kwa mwanafunzi huyo, kubainisha kuwa polisi bado wanaendelea na uchunguzi.

Lakini, Idd ambaye ni baba mzazi wa Idrissa alisema ni miezi miwili sasa tangu mwanaye atekwe na kwamba wanachokifanya sasa ni kuzidisha maombi ili arejee akiwa salama.

Mtoto mwingine, Shaaban Ngunda mwenye umri wa miezi sita aliyepotea Novemba 6 katika mazingira ya kutatanisha maeneo ya Mbagala Charambe, Temeke , jijini Dar es Salaam alifikisha siku 19 jana.

Mama mdogo wa Ngunda, Siri Nongwa aliliambia Mwananchi kuwa bado mtoto huyo hajaonekana tangu alipochukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwa mtu aliyemtaja kwa jina la Mama Rose, anayeishi mtaa wa Ubungo Mbagala Charambe.

Siri alisema ingawa suala hilo bado linafanyiwa uchunguzi na polisi, familia ipo katika mkakati wa kuomba kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuomba kusaidiwa kumpata mtoto huyo.

Soma zaidi: