Magufuli awaweka roho juu wakuu wa mikoa na wilaya

Rais John Magufuli

Muktasari:

Pia amesema wale waliotakiwa kutoa maelezo kuhusu miradi iliyotajwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika uzimaji wa Mwenge wazingatie agizo lililotolewa, asema wanafanya utani kwa Mwenge ulioasisiwa na Mwalimu Nyerere

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza wakuu wa mikoa na wilaya katika halmashauri tano nchini zilizofanya udanganyifu kwa miradi iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka jana, wajieleze kabla ya kuchukuliwa hatua.

Pia, Rais Magufuli amewataka wakuu wa mikoa na wa wilaya zote ambazo zimekutwa na miradi yenye dosari kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kutoa maelezo ndani ya siku 10 na kurekebisha dosari zilizojitokeza.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana alipokutana na kufanya mazungumzo na wakimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka huu waliomtembelea Ikulu jijini Dar es Salaam na kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu kutoa siku 10 kwa halmashauri 64 ambazo Mwenge wa Uhuru ulishindwa kuzindua au kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo iliyokutwa na dosari.

Rais Magufuli akisisitiza juu ya maagizo ya Waziri Mkuu, aliwataka viongozi wa mikoa na wilaya husika kufanya hivyo sasa na kueleza kwa nini wanaudanganya Mwenge ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Waziri Mkuu, nataka yale maelezo ya kina watoe sasa, kwa nini wanadanganya Mwenge, kwa nini wanamdanganya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni kiini na mwanzilishi halali wa Mwenge huu,” alisema Rais Magufuli.

Awali, Waziri Mkuu alisema mwenge huo, chini ya Charles Kabeho ulikimbizwa katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji 195 hapa nchini.

Majaliwa alisema tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu walikuwa wakifanya ukaguzi wa kina wa miradi ya maendeleo ili kubaini ubora na manufaa ya mradi husika kwa wananchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema katika mbio hizo, jumla ya miradi 1,432 yenye thamani ya Sh660.6 bilioni ilizinduliwa, kufunguliwa na kuwekwa mawe ya msingi wakati miradi 80 iliyopo katika halmashauri 64 ilikutwa na dosari mbalimbali.

Waziri Mhagama alibainisha kuwa dosari hizo ni pamoja na ubora hafifu wa miradi na kukosekana kwa uhalisia wa thamani ya mradi na walikagua miradi 94 iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka jana na kubaini miradi mitano kati yake haijafanyiwa kazi.

“Tumeamua kuboresha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kuwatumia wakimbiza Mwenge kubaini ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma katika miradi pamoja na kuchukua hatua wakiwa hukohuko kwenye miradi,” alisema Mhagama.

Juzi, wakati wa kilele cha mbio hizo, Mhagama alisema miradi 80 imeisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh27 bilioni.

Alisema wakimbiza Mwenge hao pia walifanya ukaguzi wa miradi ambayo imewahi kuzinduliwa wakati wa Mwenge na viongozi mbalimbali wakabaini miradi 94 yenye thamani ya zaidi ya Sh109 bilioni iliyozinduliwa mwaka jana, ilionekana kutoendelezwa.

Mhagama alitaja baadhi ya halmashauri ambazo zimehusika katika ubadhirifu wa miradi ya maji, umeme na elimu kuwa ni Nyang’wale, Mbogwe, Mbeya, Makete, Njombe, Nyasa, Mbinga, Madaba, Tunduru, Kigamboni, Kinondoni, Morogoro, Chamwino na Singida.