VIDEO: Mbowe: Siondoki Chadema kwa kelele za watu

Muktasari:

Kumekuwa na shinikizo la kumtaka Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe ajiuzulu nafasi huyo, japo yeye amepuuza habari hizo akisema hataondoka Chadema wala hatadhoofika kiasi cha kumpigia mtu yeyote magoti

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema hataondoka katika nafasi hiyo ya uongozi kwa kelele za watu bali waliomchagua ndiyo wana wajibu wa kumwondoa.

Mbowe amesema hayo leo Septemba 19, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Amesema chama hicho kufanya vibaya sababu si yeye, β€œNa mimi niliwekwa na wanachama, wakitaka wataniondoa lakini siondoki kwa kelele za watu.”

Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amesema kamwe hatakuja kukipigia magoti chama tawala cha CCM.

Amesema hata siku moja CCM haitafurahi kumuona anakuwa na nguvu kwenye chama, lengo lao ni kuona anakuwa dhaifu.

"Sitokuja kuwapigia magoti hata siku moja, kila anayetoka wanamuambia anitaje mimi kwa sababu lengo lao ni kunidhoofisha."

"Wanasema tumeshindwa kwa sababu mimi ni Mwenyekiti, Mbowe alikwenda kupiga kura Monduli, kupiga kura Ukonga? Amehoji.

Mbowe amesema kazi ya kuwa kiongozi wa chama si nyepesi ni ya ujasiri na utume wenye misalaba ambayo si kila mtu anaweza kuibeba

Amesema madaraka hayo amepewa na wanachama na kuondoka ataondoka kwa amri yao, lakini kwa maoni ya walioko CCM haondoki. Amefafanua kuwa kelele za nani kaondoka Chadema haziwatoi kwenye reli.

"Kumbuka kila anapotoka diwani mmoja Chadema maelfu wanaingia, wapo wengi na tutawaibua utakapofika uchaguzi mkuu," amesema Mbowe.